Ijumaa, 8 Desemba 2017

ZANZIBAR YAKWEA MLIMA WA MAFANIKO KUKAMILIKA UTAFITI WA MAFUTA NA GESI NJIA YA MTETEMO BAHARINI

 MKURUGENZI Mwendeshaji wa Mamlaka ya Udhibiti Utafutaji na Uchimbaji Mafuta na Gesi Zanzibar, Omar Zuber Ismail (aliekaa), akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na zoezi la utafutaji nishati hizo kwa njia ya mtetemo katika bahari ya Zanzibar, katika hafla iliyofanyika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni.
Na Is-haka Omar, Zanzibar. 


           ZANZIBAR inaendelea kukwea mlima wa mafaniko kwa kukaribia kuvuna Mafuta na Gesi asilia kutoka katika ardhi yake yenyewe iliyokombolewa na Wanamapinduzi ya mwaka 1964, kutoka mikoni mwa utawala wa Kisultani.

 Hakuna wa kujivunia mafanikio haya, yanayoanza kuonyesha dalili za kuwepo kwa neema ya mafuta na gesi visiwani humu bila ya kuwakumbuka na kuwataja waasisi wetu waliomwaga damu zao kwa kutetea haki na utu wa wananchi wa visiwa vya zanzibar. 

Licha ya kuwa matunda na fursa mbali mbali zinazotokana na Sekta hiyo yenye kukuza uchumi wa taifa lolote Duniani bado watakaonufaika ni vizazi vya sasa na vijavyo, vilivyorithi utajiri wa fikikra na busara kutoka kwa wazee wa ASP hadi CCM, inayoongoza dola kwa sasa. 

 Laiti zisingekuwa neema na shufaa za Mwenyezi Mungu mtukufu kuwajalia nguvu wazee wetu chini ya kiongozi wao, ambaye ni shujaa wa kutetea haki za wanyonge Marehemu Mzee Abeid Aman Karume aliyekomboa ardhi ya Zanzibar kutoka mikononi mwa watawala wa kigeni, wenda mpaka sasa tungeendelea kuwa watumwa wa utawala huo.

Miaka mingi imepita Zanzibar kupitia awamu mbali mbali za utawala wake imekuwa ikifanya utafiti mbali mbali wa mafuta na gesi bila ya kuchoka, yaani toka mwaka 1952 hadi 2017 bado safari ya kuyasaka mafuta na gesi inaendelea. 

 Miaka 65 sasa imetimia toka kuanza kutafuta neema ya mafuta na Gesi nchini, umri ambao kwa mujibu wa miongozo ya kiimani kwa dini mbali mbali na utamaduni na mila za nchi yetu zinatuelekeza kwamba mtu akifikia umri huo anakuwa ni mtu mzima anayeelekea uzeeni lakini mwenye busara, hekima na upeo mkubwa kiakili na kimaamuzi.

 Toka wakati huo utafiti unafanywa kwa njia ya vijiti mpaka leo Teknolojia imekuwa na sasa utafiti unafanyika kwa njia za kisasa, chini ya wataalamu na magwiji wa Jiolojia katika uchimbaji wa mafuta na gesi asilia wanaotekeleza majukumu yao.
 Hivi sasa Zanzibar imepiga hatua nyingine muhimu ya kukamilika kwa zoezi la utafiti wa mafuta na gesi kwa njia ya mitetemo (seismic) katika eneo la bahari na mwambao wa visiwa vya Zanzibar.

Akizungumza katika moja ya mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar, Omar Zubeir, amesema zoezi hilo limefanikiwa licha ya kujitokeza kwa changamoto na vikwazo vilivyojitokeza katika utafiti huo. 

 Amesema zoezi hilo limefanikiwa na muelekeo umeonekana unakwenda vizuri ambapo matumaini ya kupatikana mafuta yanaonekana kwa kasi kubwa. 

 Ameongeza kwa kufafanua kuwa zoezi limechukua takribani mwenzi mmoja ambapo lilianza Oktoba 28 hadi Novemba 28 mwaka huu.

 Amesema katika zoezi hilo idadi ya mistari iliyofanyiwa utafiti ndani ya kitalu cha Pemba Zanzibar ilikuwa ni 62, huku idadi ya kilomita zilizofanyiwa utafiti ni 2,482. 

Ameitaja mistari iliyofanyiwa utafiti nje ya kitalu ilikuwa ni minne huku idadi ya kilomita zilizotafitiwa zilikuwa 333.6. 

 Mkurugenzi Omar ameeleza kuwa changamoto zilizojitokeza ni kuwepo wavuvi katika baadhi ya maeneo hali iliyosababisha shughuli za utafiti kusimama kwa muda. 

Amesema baadhi ya wavuvi waliingia katika eneo linalofanyiwa utafiti, hali iliyopelekea nyavu zao kuharibiwa lakini mamlaka hiyo imeahidi kulipa fidia.

 “Tunaomba ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi kwani zoezi hili la utafiti mbali mbali wa mafuta na gesi linawahusu wananchi wote na wa makundi yote yaliyopo katika jamii hivyo tunaomba ushirikiano na kuwa wasikivu pindi serikali inapotoa maelekezo juu ya jambo lolote linalogusa maslahi ya wote. 

 Hatua tulizozichukua ni kuhakikisha mkandarasi analipa fidia kwa uharibifu ulioripotiwa licha ya kuwa hakukua na idadi kubwa ya wavuvi waliojitokeza kulalamika,”anaeleza Mkurugenzi Omar.

 Amesema zoezi la utafiti baada ya kukamilika katika eneo la bahari sasa linatarajiwa kuanza kufanyika katika eneo la nchi kavu kazi ambalo itaanza karibuni na kuchukua zaidi ya miezi saba.

 Ameeleza kuwa utafiti wa mafuta na gesi ni mchakato wa muda mrefu, hivyo wananchi wawe wavumilivu huku wakiamini serikali yao kuwa inafanya juhudi mbali mbali za kuhakikisha zoezi hilo linakamilika kwa wakati.

 Miezi kadhaa iliyopita, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein katika hotuba yake, Dk Shein amesema  baada ya kukamilika kwa kazi ya kutunga Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia, kuanzisha Mamlaka ya Kusimamia na Kuratibu Shughuli za Mafuta na Gesi na kuanzisha kampuni ya mafuta, hatua muhimu inayofuatana ni kuandaa mikataba ya mafuta na gesi asilia.

Dk. Shein amesisitiza kuwepo kwa umakini mkubwa katika kuandaa, kusimamia na kufuatilia mikataba ya mafuta na gesi ili kuepuka ubabaishaji unaoweza kuingiza nchi katika migogoro ya kimaslahi.

Wito huo aliutoa wakati akihutubia Baraza la Eid El Fitr katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwajuni mjini Zanzibar.

 Amesisitiza kuwa mikataba ya mafuta na gesi asilia isitoe mwanya wa kuwanufaisha watu wachache na makampuni yao kwa njia za kijanja, dhuluma, mambo ya ubabaishaji na kutaka kujifunza kwa waliotangulia katika biashara ya aina hiyo. 

 Alisema uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, wataalamu na taasisi zote zinazohusika katika kuandaa mikataba hiyo wafahamu kuwa rasilimali ya mafuta na gesi asilia ni ya Wazanzibari wote.

 Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Abdulla Juma Mabodi anasema utafiti wa mafuta na gesi unatokana na usimamizi mzuri wa sera za Chama cha Mapinduzi(CCM), katika kutanua wigo wa ukuaji wa fursa mbali mbali za kiuchumi nchini.

 Amewashangaa baadhi ya wanasiasa hususani wa upinzani wanaohoji na kulaumu uendeshaji wa zoezi hilo, badala ya kupongeza mafanikio yaliyofikiwa na serikali zote mbili za SMZ na SMT.

Alisema baada ya wapinzani kutumia suala la mafuta na gesi kama sehemu ya kujitafutia umaarufu wa kisiasa, CCM kupitia serikali zake waakamua kutoa baraka zote kisheria kwa Zanzibar kuchakata, kufanya utafiti na kuchimba mafuta. 

 “ Kuna baadhi ya watu wanaendelea kupotosha kuwa Zanzibar haina mamlaka kisheria ya kuchimba mafuta na gesi, jambo ambalo sio kweli kwani Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein tayari alisaini sheria ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi Zanzibar, sheria namba 6 ya mwaka 2016.

 Alisema kitendo cha kutia saini sheria hiyo, hakijavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano kama baadhi ya watu wanavyodai.”, amefafanua Dk.Mabodi. 

Amesema wenye shaka na jambo hilo wakasome vizuri Sheria ya Mafuta Namba 21 ya 2015 iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo imeweka msingi imara wa kisheria wa kutambua rasilimali ya mafuta na gesi asilia ni miongoni mwa mambo yaliyoorodheshwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Akizungumzia sekta ya mafuta na gesi, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha waandishi wa Habari Zanzibar(ZPC) MwinyiMvua Abdi Nzukwi, amevisihi vyombo vya habari nchini kuisaidia serikali kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa sekta hiyo kwa maendeleo ya nchi. 

 Amesema kuwa masuala ya mafuta na gesi asilia yamepotoshwa kwa muda mrefu kutokana na wanahabari na vyombo vya habari kutowekeza katika utafiti, jambo ambalo linafanya wanahabri wengi kukwepa kuandika habari za utafiti au kupotosha jamii kwa lengo ya kuuza habari. 

Hata hivyo alieza kwamba ni wakati mwafaka wa waandishi wa habari kusoma na kujifunza kwa kina masuala ya mafuta na gesi asilia ili wawe na uwezo wa kutoa taaluma sahihi kwa umma. 

Akitoa uzoefu wake raia wa nchi ya Nigeria, Bw. Jacob Odumogo Chinedu alisema ili kuweka nchi katika hali ya utulivu kabla ya kuanza kuchimba rasmi rasilima hiyo,ni lazima serikali ianze mapema kuielimisha jamii kutambua kuwa mafuta na gesi ni kitega uchumi kama zilivyo rasilimali nyingine. 

 Jacob ameeleza kuwa taaluma hiyo itaondosha dhana za baadhi ya watu kuamini kwamba nchi inapochimba mafuta na gesi ni fursa inayoweza kumtajirisha kila mtu na hatimaye kuingia katika vita vya kimaslahi kupitia mgongo wa kisiasa.

Ameongeza kuwa nchi nyingi duniani zinazochimbwa mafuta na gesi asilia zimeshindwa kunufaika na rasilimali hiyo kutokana tamaa za baadhi ya viongozi wa kisiasa kwa kushirikiana na maadui wa nje kutaka kujinufaisha wao badala ya wananchi wote.

Makala hii inaendelea Wiki ijayo.....

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni