Jumatano, 13 Desemba 2017

DK.SHEIN-VIONGOZI LETENI MABADILIKO YA KIMAENDELEO UMOJA WA WAZAZI TAIFA

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein akihutubia katika ufungaji wa Mkutano Mkuu wa Tisa  wa Umoja wa Wazazi CCM Tanzania uliofanyika jana katika Ukumbi wa JK-Dodoma.


NA IS-HAKA OMAR, DODOMA.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein  ameutaka viongozi wapya waliochaguliwa kupitia uchaguzi wa Umoja wa Wazazi wa CCM Taifa, kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto zinazoikabili taasisi hiyo kwa miaka mingi iliyopita.

Kauli hiyo jana wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Tisa wa Umoja huo uliokuwa ni Maalum kwa ajili ya uchaguzi wa kuwapata viongozi watakaoongoza taasisi hiyo kwa miaka mitano ijayo, amesema Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Bulembo ameonyesha jitihada zake katika kukwamua baadhi ya changamoto, hivyo viongozi wapya walioingia hivi sasa waonyeshe umahiri wao kiutendaji.

Dk. Shein ameeleza kwamba hana hofu na utendaji wa viongozi wapya kwani wengi wao anafahamu uwezo wao kisiasa na kiutendaji, hatua inayompa matumaini ya kuona mabadiliko ya haraka ndani ya Taasisi hiyo.

“Hakika mmechagua viongozi wachapa kazi na wenye uwezo wa kwenda na kasi ya kiutendaji ya CCM na Serikali zake mbili katika kuwatumikia wananchi na kujenga taifa lenye nguvu za kiuchumi”. Amefafanua Dk. Shein.

Aliwasihi wagombea ambao kura zao hazikutosha na wakakosa nafasi za Uongozi kuwa wavumilivu na wasisusie, kwani Chama cha Mapinduzi bado kina nafasi nyingi hivyo wanaweza kuteuliwa kwa nafasi nyingine kwa lengo la kuendeleza umoja na mshikamano ndani ya chama hicho.

Hata hivyo aliwakumbusha kuwa pamoja na majukumu mengine waliokuwa nayo viongozi wapya wa Umoja huo wanatakiwa kujipanga kikamilifu kwa kutafuta wanachama wapya watakaoongeza nguvu za kuunda jeshi la CCM na hatimaye kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.

“ Wakati wa kujiandaa na uchaguzi Mkuu ujao ni sasa na tayari nyinyi mmepata usajili rasmi wa kushiriki kikamilifu katika michakato mbali mbali ya maandalizi ya kukiletea ushindi Chama cha Mapinduzi 2020”., amesisitiza Dk. Shein.

Aidha ameagiza Uongozi huo chini ya Mwenyekiti wake Dkt. Mndolwa kuhakikisha wanayafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. John Pombe Magufuli wakati akihutubia katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Umoja huo jana.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni