Jumamosi, 30 Desemba 2017
BALOZI SEIF ALI IDDI-ATOA NASAHA KWA WABUNGE NA WAWAKILISHI.
MAKAMU wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, ameshtukia mchezo mchafu ambao umeanza kufanywa na baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), ambao wanataka kugombea nafasi za ubunge na uwakilishi, kuanza harakati za kutaka kuhama majimbo yao kwa ajili ya kugombea maeneo mengine baada ya kuharibu maeneo yao.
Amesema atahakikisha anafanya juhudi zote za kukishauri Chama kuhakikisha kuna kuwepo na msimamo thabiti kwa wagombea hao ambao watakaoanza kufanya harakati hizo kukatwa majina yao.
Balozi Seif amesema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa CCM, Mkoa wa Magharibi, ambapo amewataja baadhi ya viongozi hao kuwa hawana msimamo wala nia njema ya kukitumikia chama na wananchikwa ujumla.
"Siasa sio biashara ama sehemu ya kujinufaisha mtu binafsi bali ni jukwaa la kusikiliza na kuratibu kero za wananchi na kuzifanyia kazi..,ni aibu kwa baadhi ya viongozi wetu kukwepa majukumu yao na badala yake wanaanza kutanga tanga huku na kule.
"Ikumbukwe kuwa kufanya hivyo ni kuhatarisha chama na kudhofisha jitihada za CCM katika kutekeleza ilani ya Chama hivyo kila Mbunge ama mwakilishi atakayegombea abaki kwenye jimbo lake husika kama umeharibu katika eneo lako ubaki huko usubirie wananchi waje kukuwajibisha kwa uliofanya,"alisema Makamu huyo wa Pili wa Rais.
Amesema wanachama hao ambao wagombea wa nafasi hizo ufikia uamuzi huo wa kuyakimbia majimbo yao ya zamani na kutaka kuhamia maeneo mengine baada ya kujibaini kutokuwatumikia vyema wanachama na wananchi katika kipindi walichoomba ridhaa ya kuwatumikia kwa vipindi vya awali.
Katika maelezo yake ameongeza kuwa imebainika uwepo wa baadhi ya wawakilishi na wabunge wanaoendelea na majukumu yao ndani ya majimbo yao ukumbwa na matatizo ikiwemo ushawishi, ftina na majungu kwa wale ambao wanataka kugombea nafasi hizo.
Akigusia suala la Uchaguzi ndani ya Chama Balozi Seif amesema Wanachama wenye kufaa kuchaguliwa ndani ya Chama cha Mapinduzi ni wale waliojaa sifa za ziada kupita wengine katika kujenga Umoja na mshikamano kwenye Taasisi hiyo ya Kisiasa.
Ameeleza kuwa sifa hiyo ya Wanachama lazima iendane na uwezo wa Kiongozi huyo wa kuwashawishi wasiokuwa Wanachama kujiunga na Chama katika kukijengea nguvu za kuendeleza ushindi kwenye Uchaguzi mkuu wa Mwaka 2020.
Balozi Seif amesema kazi ya Chama chochote cha Siasa ni kushika Dola. Hivyo kwa Mantiki hiyo CCM katika mabadiliko makubwa yanayoendelea kuyafanya katika kupanga safu za Uongozi kuanzia ngazi ya Shina hadi Taifa kinahitaji Viongozi watakaokiletea ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu huo.
Makamu huyo amefahamisha kwamba Wanachama wanapaswa kuzingatia muelekeo wa Viongozi wa Chama chao katika kuwachagua Wanachama watakaowapeleka huo kwenye chaguzi zilizobakia hata kama watakuwa na sura mbaya.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM amewasihi Viongozi watakaochaguliwa kuwa wabunifu hasa katika kukifanya chama kuwa na nguvu za ziada za kujitegemea kifedha badala ya kusubiri kutembeza bakuli kwa wahisani.
Balozi Seif amewatahadharisha wazi kwamba utegemezi siku zote unawajengea nguvu wale wanaowategemea, jambo ambalo baadhi ya wahisani hao wanaweza kutumia fursa hiyo kukiyumbisha Chama kirahisi.
Ametoa wito kwa Uongozi utakaochaguliwa uelewe fika kwamba utakuwa na jukumu la kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020 kwa kivitendo kama inavyoelezwa katika Sura ya nane.
Awali akisoma Risala ya Mkoa wa Magharibi Katibu wa CCM wa Mkoa huo, Aziza Ramadhan Mapuri, amesema uongozi wa CCM Mkoani humo umepata mafanikio makubwa katika kujenga upendo miongoni mwa Wanachama.
Aziza amesema upendo huo umeuwezesha Uongozi wa Mkoa huo kuisimamia vyema Serikali kwenye ngazi ya Mkoa katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 – 2020.
Mbali na hilo, amesema katika kipindi cha Miaka mitano inayomalizika, CCM Mkoa wa Magharibi umefanikiwa kupata eneo kwa ajili ya Ujenzi wa Ofisi ya Kisasa ya Mkoa itakayoambatana na uwepo wa vitega uchumi vitakachouwezesha Mkoa huo kujitegemea wenyewe na kujiepusha na utegemezi.
Akigusia changamoto zinazoukabili Mkoa huo Katibu huyo wa CCM Mkoa Magharibi amesema uhamiaji holela ambao unasababisah ujenzi holela ndani ya eneo hilo ambalo umeleta athari kubwa hat hususan kimazingira.
Kwa upande Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi,aliyemaliza muda wake, Yussuf Mohamed Yussuf, amesema uchaguzi zilizokuwa zikiendelea ndani ya chama kuanzia ngazi ya Shina hadi Mkoa ni matukio muhimu ya kuendeleza Demokrasia ndani ya Chama.
Yussuf ameeleza kuwa katika kipindi chake cha utumishi wa nafasi hiyo katika kipindi cha miaka 15 ameshuhudia mabadiliko makubwa yaliyofanywa na CCM ndani ya kipindi kifupi jambo ambalo wanastahiki kupongezwa Viongozi pamoja na Wanachama wenyewe.
Amesema Chama cha Mapinduzi kitaendelea kuwa imara na chenye nguvu Tanzania endapo baadhi ya wanachama wake wataondokana na tabia za fitna na ubinafsi na badala yake wakafuata Katiba na Kanuni za CCM, na kuzifanyia kazi nasaha za Mwenyekiti wa Chama hicho Dkt. John Pombe Magufuli na Makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni