Jumatatu, 18 Desemba 2017

DKt.MAGUFULI- AFUNGUA MKUTANO MKUU WA TISA WA CCM TAIFA, CHEYO, SHIBUDA NA MREMA WAKIRI KUWA CCM NI GARI KUBWA


 MWENYEKITI wa CCM Taifa Dkt. John Pombe Magufuli  akifungua Mkutano Mkuu wa Tisa wa Chama cha Mapinduzi unaofanyika katika ukumbi wa JK Dodoma.



NA IS-HAKA OMAR, DODOMA.

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Dkt.John Pombe Magufuli amesema vitendo vya rushwa ni sawa na ugonjwa wa kansa na isipodhibitiwa itaendelea kusababisha madhara makubwa kwa Chama na serikali.

Pia, ameeleza kwamba kila mwananchi kwa nafasi yake wanatakiwa kushiriki kikamilifu katika mapambano ya vita hiyo kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu kwa Watanzania wote.

Kauli hizo amezitoa wakati akiwahutubia mamilioni ya Wanachama wa CCM na wananchi wa ujumla katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Tisa wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Uliofanyika katika Ukumbi wa JK Dodoma.

Kupitia hotuba yake Dkt.Magufuli amesema endapo vitendo vya rushwa, ufisadi na makundi ya kuhatarisha uhai wa chama visipodhibitiwa mapema vinaweza kukigharimu chama na hatimaye kikashindwa kusimamia misingi yake.

Ameeleza kwamba ili nchi iweze kupiga hatua za haraka za maendeleo ni lazima kupigwe vita vitendo vyote vinavyobinya ustawi wa maendeleo kwa wananchi wote.

"Rushwa imetutafuna kwa muda mrefu sasa tumeamua tena kwa dhati kupambana na vitendo hivyo ili kurejesha heshima katika taasisi yetu ambayo ni tegemeo kwa wananchi wote",amesisitiza Dkt.Magufuli na kuongeza kuwa CCM ni lazima irudi katika misingi yake ambayo ni ya kuwahudumia wananchi kwa ufanisi bila ya kujali tofauti zao za kisiasa.

Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa alisema katika juhudi za chama hicho kujiimarisha kisiasa kimekuwa kikitekeleza kwa vitendo ilani yake ya uchaguzi hali ambayo wananchi mbali mbali wamehamasika na kujiunga na CCM.

Amesema mbali na viongozi wa vyama vya upinzani waliojiunga na Chama hicho bado kinaendelea kufanyia kazi maombi mengi ya wanachama wa vyama vya upinzani wanaotaka kujiunga na CCM ili kupokea wanachama halisi ambao sio mamluki wa kuivuruga taasisi hiyo.

Amewataka viongozi wa CCM  waliochaguliwa kuanzia ngazi za mashina hadi taifa kusimamia misingi ya chama hicho kwa kuhakikisha kinarudi mikononi mwa wanachama na sio kundi dogo la watu wenye fedha na wanasiasa maarufu wanaojali maslahi yao badala ya maislahi ya nchi.

“ Ndugu zangu tushirikiane kukijenga chama chetu kwani ni kikongwe na kilichopita katika vipindi tofauti vya kisiasa hivyo kila mmoja wetu kwa viongozi na wanachama sote tunawajibika kukilinda na kukipigania kwa nguvu zote.

Kwani ilifikia wakati kama huna fedha huwezi kugombea nafasi yoyote ya kisiasa jambo ambalo sio utamaduni wa CCM, na tabia hiyo ilitoa nafasi kwa wenye fedha kutumia rushwa kupata uongozi. Lakini namshukru sana Rais mstaafu Kikwete kwani  kama ngekubali kununuliwa na wala rushwa mimi nisingepata nafasi ya kuwa Rais.”, amefafanua Magufuli.

Akizungumzia hali ya kisiasa alisema CCM imekuwa ikishinda kwa kishindo na kutolea mfano uchaguzi mdogo uliofanyika hivi karibuni Tanzania bara katika kata 43 na CCM ikashinda kata 42 kuwa ni hatua muhimu kwa chama hicho kujipanga zaidi kuelekea uchaguzi mkuu wa dola ujao.

Dkt. Magufuli ameeleza kwamba katika juhudi za kurejesha chama katika misingi yake wamejiwekea vipaumbele  ambavyo ni pamoja na kuzifanyia mabadiliko Katiba ya CCM na Kanuni zake ili ziendane na wakati wa sasa kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Ameyataja mabadiliko hayo kuwa ni pamoja na kupunguza idadi ya Wajumbe wa vikaa vikuu vya Chama sambamba na kupunguza idadi ya vikao kwa lengo la kuwa na wajumbe wachache  watakaoweza kuleta ufanisi ndani ya Chama hicho.

Aidha amesema pamoja na mikakati ya kukijenga upya chama cha Mapinduzi bado viongozi na wanachama wana jukumu la kutekeleza kwa vitendo sera ya ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya viwanda na kuhakikisha ifikapo mwaka 2020, Chama kinamiliki japo kiwanda kimoja cha kuingiza kipato ndani ya taasisi hiyo.

“ Ni aibu kubwa kuona Chama chetu kila kipindi cha uchaguzi tunakuwa omba omba wakati sisi ndio tunaoongoza nchi na Mwenyezi mungu ametujalia rasilimali nyingi, lakini tunashindwa kuzisimamia.”, amesema  Dkt. Magufuli.

Amesema baada ya chama hicho kufanya uhakiki wa mali zake kimebaini kwa Tanzania  nzima kinamiliki viwanja 5000, rasilimali ambazo zikisimamiwa vizuri zitaweza kuingiza fedha nyingi ndani ya taasisi hiyo.

Akizungumzia mfumo wa vyama vingi amesema maendeleo hayana Chama  ila maendeleo  ya kweli yataletwa na Chama cha Mapinduzi.

Amevisifu baadhi  ya vyama vya siasa vinavyoweka mbele uzalendo wa nchi kwa kuunga mkono mambo mema yanayotekelezwa na serikali zote mbili ya Tanzania bara na Zanzibar.

Mapema akizungumza  Katibu  Mkuu wa CCM Taifa, Abdulrahman Omar Kinana  amesema  sababu ya Chama cha Maoinduzi kupendwa na wananchi na hatimaye wakakipa ridhaa ya kuongoza dola ni kuimarika kwa Demokrasia ndani  ya taasisi hiyo inayotoa uhuru mpana kwa kila mwanachama kuchagua na kuchaguliwa bila vikwazo.

Amesema  awamu mbali mbali za uongozi uliopita walikuwa wakipambana na vitendo vya rushwa lakini kwa serikali ya awamu ya tano imevunja rekodi kwani inadhibiti ipasavyo rushwa na ufisadi kwa  maslahi ya wananchi wote.

Wakizungumza kwa wakati tofauti kupitia mkutano huo, baadhi ya viongozi wakuu wa vyama vya upinzani wameeleza kwamba CCM kwa sasa imekuwa chama bora cha kisiasa kutokana na kusimamia vizuri sera zake.

Akizungumza Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa Tanzania, John Shibu Magalle, amesema huu sio wakati wa vyama vya siasa nchini kurumbana bali washirikiane na serikali iliyopo madarakani kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Amesema kila mtu katika chama chochote cha siasa hana haki ya kuhamia chama chochote anachotaka hivyo baadhi ya vyama vya siasa vinavyowaita wanachama waliohama ndani vyama hivyo wasaliti watakuwa hawatendi haki katika mfumo wa kidemokrasia.

Shibuda ametumia nafasi hiyo kumuomba Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kuvipatia ruzuku vyama vya upinzani vinavyoonyesha uzalendo wa kuunga mkono serikali kwa maslahi ya nchi.

Naye Mwanasiasa Mkongwe kutoka Chama cha UDP, John Cheyo amekiri kuwa Chama cha Mapinduzi  kimekuwa na uwezo mkubwa wa kiuongozi na utawala bora kuliko vyama vingine vya kisiasa nchini.

“CCM ni chama kubwa na hakuna wa kuling’oa na atakayejaribu kuling’oa atang’oa mwenyewe”, amesema Cheyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TLP, Augusto Lyatonga Mrema, alisema maendeleo yaliyopatikana kwa kipindi kifupi katika utawala wa serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Dkt. Magufuli yanatakiwa kulindwa na kuheshimiwa na wananchi wote.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni