MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Dkt.Edimund Benard Mndolwa akiwashukru wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Umoja huo kwa kumchagua ili aongoze kwa miaka mitano ijayo. |
NA IS-HAKA OMAR, DODOMA.
UMOJA wa Wazazi wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) Taifa wamefanikiwa kumpata Mwenyekiti mpya ambaye ni mwanasiasa mkongwe
na msomi wa kada ya Uchumi ambaye ni Dkt. Edimund Benard Mndolwa kufuatia
uchaguzi uliokuwa na ushinsani mkubwa uliofanyika jana katika Ukumbi wa JK uliopo
Dodoma.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Mjumbe
wa Kamati Kuu ya CCM Taifa , Jerry Slaa kwa niaba ya jopo la wasimamizi wa
uchaguzi huo alimtangaza Mwenyekiti huyo mpya kuwa ameshinda kwa
kupata kura 552 sawa na asilimia 68.06 kati ya kura 811 zilizopigwa na
akawashinda wenzake watatu alikuwa akichuana nao.
Wagombea wengine wa nafasi hiyo walikuwa
ni Eng. Burton Lumuliko Kihaka kura 178, Simon George Rubugu kura 59 na Fadhil
Rajabu Maganya aliyepata kura 22.
Kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Umoja
huo aliyeibuka kidedea ni mwanasiasa mpambanaji aliyewahi kugombea nafasi hiyo
katika awamu iiyopita akakosa lakini kwa awamu ya sasa amefanikiwa kuibuka
mshindi ambaye ni Haidar haji Abdallah.
Pia katika nafasi ya NEC Tanzania bara
waliotazwa kushinda ni Nemelock Sokoine, Mohamed nassor kingite pamoja na Paul
Herman Kirigini, ambao wameshinda kati ya wagombea 11 waliokuwa wakiwania
nafasi hiyo. Nafasi zingine za NEC kutoka Zanzibar ni Suleiman Juma Kimea
pamoja na Amina Ali Mohamed walioshinda kati ya wagombea wanne waliokuwa wapo
katika kinyang’anyiro hicho.
Kwa upande wa Baraza Kuu Zanzibar
walioshinda ni Habiba Mohamed, Ali Issa Ali pamoja na Cristina Anton
waliochaguliwa kuwawakilisha Wana CCM katika baraza hilo.
Kwa upande wa Baraza Kuu kwa Tanzania bara
ni Lulu Mtemvu, Stephan Hilary Maji Marefu pamoja na Sudi Kassim Sudi.
Kwa nafasi ya uwakilishi wa UWT
aliyeshinda ni Nuru Kassian Baimanga kati ya wagombea wenzake wawili aliokuwa
akishindana nao. Hata hivyo katika nafasi ya uwakilishi wa UVCCM aliyeshinda ni
Omar Ajili Kalolo kati ya wagombea wenzake
watano aliokuwa akishindana nao.
Matokeo hayo yametangwazwa mbele ya
viongozi mbali mbali akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed
Shein, Katibu Mkuu wa CCM Taifa , Abdulrahman Omar Kinana, Naibu Katibu Mkuu wa
CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi pamoja na Mwenyekiti Mstaafu wa Umoja wa
Wazazi wa CCM Tanzania Abdallah Bulembo.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa
mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti na kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Dkt.
Edimund Benard Mndolwa ametoa shukrani zake kwa wajumbe wote wa Mkutano huo na
kuahidi kuendeleza mambo mema yaliyoachwa na mtangulizi wake.
Akitaja vipaumbele vyake alieleza kuwa
atahakikisha anatatua kwa haraka changamoto ya mishahara kwa watumishi wa Umoja
huo sambamba na kumaliza madeni yanayoikabili taasisi hiyo.
“ Mmenichagua nikutumkieni name
nakuahidini kuwa sitowaangusha bali nitatumia nguvu na elimu niliyonayo katika
masuala ya uchumi kufanya mageuzi ya kiuchumi yatakayowanufaisha wanajumuiya
wote bila ubaguzi”, amesema Dkt. Mndolwa.
Pia ameeleza kuwa atakuwa mstari wa mbele
kuendeleza mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi Ndani na nje ya
umoja huo.
Ameitaja dhamira ya kuwania nafasi hiyo
kwamba ni kukitumikia Chama cha Mapinduzi kwa uadilifu na utii sambamba na
kuhakikisha kinashinda kwa kishindo katika uchaguzi Mkuu wa Dola wa mwaka 2020.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni