Jumapili, 3 Desemba 2017

MHE.KHADIJA- WANA CCM CHAGUENI VIONGOZI IMARA

Na Is-haka Omar,Picha na Abeid Machano Kh -  Zanzibar.
             
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa , Khadija Hassan Aboud amewataka Wajumbe wa mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Mjini, kuwachagua viongozi wenye uwezo na uadilifu wa kulinda maslahi ya Chama bila ya kuteteleka.


Kauli hiyo aliitoa wakati akifungua Mkutano mkuu wa uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini,Unguja, amesema viongozi watakaochaguliwa ni lazima wawe na uwezo wa kupambana na vikwazo vya kisiasa vilivyopo ndani ya Mkoa huo.

Amewasisitiza wajumbe wa mkutano huo kutumia vizuri haki yao ya kidemokrasia kwa kuhakikisha viongozi watakaowachagua wanasimamia kikamilifu haki na maslahi ya wanachama wote bila ya ubaguzi na makundi ya kuhatarisha uhai wa Chama. 

“Viongozi watakaochaguliwa leo watapewa dhamana za kuongoza Mkoa huu kwa miaka mitano ijayo hivyo ni matarajio yangu kuwa watakuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya ubaguzi, rushwa na ufisadi ndani na nje ya Chama chetu”,alisema Khadija. 

Mjumbe huyo amewataka viongozi na wanachama kwa ujumla kuacha tofauti zao badala yake kushirikiana katika kukijenga Chama ili kiendelee kuwa imara katika Bara la Afrika.

Amesema ni wajibu wa kila mwanachama kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mwenyekiti wa CCM, Dk. John Pombe Magufuli katika kudhibiti vitendo vya rushwa, ufisadi na ubadhilifu wa mali za umma.

Khadija ameeleza kuwa viongozi hao wanapaswa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa kuhakikisha wananchi bila kujali itikadi zao za kisiasa wanapata maendeleo ya kudumu.

Amewakumbusha viongozi wa Chama na Jumuia zake waliochaguliwa kuanzia ngazi ya mashina, kuwa wanatakiwa kujipanga kwa kuongeza wanachama wapya watakaosaidia kufanikisha ushindi wa CCM katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi, amesema hakuna Chama chochote za kisiasa nchini kinachoweza kuzuia kasi ya taasisi hiyo katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Dk. Mabodi alisema CCM imekuwa ni kinara wa demokrasia kutokana na mfumo wake wa kuongoza Chama kwa kuzingatia matakwa ya Kikatiba.

“ CCM tupo imara na kwa sasa tunaendelea kusajili wachezaji wapya katika safu za uongozi watakaofanikisha na kukiletea ushindi chama chetu katika ligi Kuu ya kisiasa ya uchaguzi wa mwaka 2020.”, alisema Dk.Mabodi.

Alitoa wito kwa wanachama wa vyama vya upinzani visiwani Zanzibar kufanya maamuzi ya busara ya kujiunga na Chama cha Mapinduzi ili nao wanufaike na siasa zinazojali misingi ya haki na demokrasia kwa wananchi wote bila ya mipaka.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi katika Mkutano huo.
 Wajumbe wa  Mkutano huo wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo.
Mjumbe  wa mkutano huo akipiga kura ya kuwachagua viongozi wa CCM Mkoa huo watakaoongoza kwa miaka mitano ujayo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni