Alhamisi, 14 Desemba 2017

JOKATE- VIJANA TUTHAMINI UTAMADUNI WETU KWA MAENDEEO MAPANA YA TANZANIA.

 
 KAIMU  Mkuu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM  Taifa, Jokate Mwegelo .

NA IS-HAKA OMAR, DODOMA.

UMOJA wa Vijana  wa CCM  (UVCCM)  umeunga mkono matamshi ya Mwenyekiti  wa CCM  Rais Dkt. John Magufuli ya kutaka vijana kusimamia, kuendeleza na kuheshimu maadili ya Taifa na kuacha kuvaa  mavazi yasio na heshima lakini pia kuhimiza utunzaji  mazingira na malezi kwa vijana.

Pia umoja huo umekiri ipo haja na umuhimu kwa  vijana wa kitanzania na Afrika  kufuata tamaduni zao. kuenzi mila,jadi, asili na  desturi   bila kupapatikia silka , mavazi au utamaduni wa kigeni .

Matamshi hayo yametamkwa jana na Kaimu Mkuu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi UVCCM  Taifa, Jokate Mwegelo alipotakiwa kutoa maoni yake kufuatia hotuba ya Mwenyekiti wa CCM  Rais Dk Magufuli aliyoitoa  kwenye mkutano Mkuu wa Wazazi Mkoani  hapa.

Jokate alisema kila Taifa duniani lina utamaduni wake, desturi na ustaarabu wake hivyo hakuna shuruti wala lazima ya Taifa moja kuiga utamaduni wa Taifa au mataifa  mengine kwani kutenda hayo ni kukubali ukoloni mamboleo.

Alisema Afrika na vijana wake hawalingani kabisa na vijana  kwenye mabara mengine duniani yenye kufuata utamaduni usiofanana aidha na Tanzania au Afrika hivyo uamuzi wa kufuata mkumbo una gharama na hasara kama za bendera kufuata upepo .

"Kama kuna mahali vijana wa Tanzania tulijikwaa  kiutamaduni na kimaadili ipo haja ya kujiuliza , kujipanga upya na kutanabahi. Kujikwaa si kuanguka .Tuna nafasi ya kujisahihisha na kuheshimu  tunayoelekezwa aidha na Wazazi au viongozi wetu "Alisema Jokate.

Alieleza k aina ya mavazi,  lugha , mazingatio ya kiutamaduni na kutofuata maadili kwa msukumo wa utandawazi ikiwemo kuiga mitindo ya maisha kwa  mtu mmoja mmoja na Taifa ni ishara ya kuanza kupotea asili yetu .

"Maendeleo ya dunia yana faida na hasara zake. Ipo haja kuzitazama faida na kuzifuata lakini pia kuzianisha hasara na kuzikwepa.Tufike mahali tusikubali kufuata mkumbo wa kuacha asili ya tamaduni zetu hatimaye  kuiga za kigeni "Alisema.

Pia Kaimu huyo Katibu wa Idara alisema licha ya kuwa ni  utumwa wa fikra na kudumaa kwa mawazo kwa kutojali vyenu na kuenzi vya wenzenu pia iko hatari ya kuacha mila na desturi zenu na kujikuta mkiiiga tamaduni za kigeni na kupuuziia asili zetu.

"Tuna Taifa letu linaloheshimika  ambalo ni huru na lenye kujitegemea . Hatuwajibiki kuiga mambo ya nje na kuubeza utamaduni wetu au kuziacha jadi za bibi na babu zetu. Ustaarabu wetu haulingani na wa mataifa mengine vile vile hatulazimiki kuwapia magoti watu wengine  "Alisema.

Jokate alisema moja kati ya malengo ya jumuiya ya Wazazi ni kusimamia malezi na maadili, afya, elimu na mazingira hivyo ipo haja kwa jumuiya hiyo kujikita zaidi kimikakati katika uhifadhi  wa mazingira ili kukabiliana na tishio la mabadiliko ya tabia nchi .

"Tunaipongeza jumuiya ya Wazazi kwa kutilia maanani ujenzi wa sekondari nyingi nchini katika dhima ya kukuza sekta ya elimu. Tuna tatizo zito  la mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu mkubwa  wa mazingira , misitu yetu imeharibiwa,baadhi ya mito na maziwa yanakauka na kupotea kwa uoto wa asii"Alieleza Joate 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni