Jumapili, 10 Desemba 2017

WALIOTOKA UPINZANI WASEMA DKT.MAGUFULI AMEVUNJA REKODI


 Kutoka kushoto ni: Aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) Bw. Patrobas Katambi, Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Mwanachama wa CHADEMA Bw. Lawrence Masha, Aliyekuwa mwanachama mwandamizi wa ACT Wazalendo Bi. Edna sunga, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM Humphrey Polepole, Aliyekuwa Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Samson Mwigamba na Katibu Mkuu Wizara ya Maji Profesa Kitila Mkumbo aliyekuwa kuwa mwanachama mwandamizi wa chama cha ACT Wazalendo.

 BAADHI ya wajumbe na Washiriki wa Mkutano Mkuu wa Tisa wa UVCCM Taifa Uliofanyika Leo Mjjni Dodoma katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Dodoma.

NA IS-HAKA OMAR, DODOMA.

VIONGOZI  mbali mbali waliotoka katika vyama vya upinzani na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (UVCCM), wamesema kuwa Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amevunja rekodi katika kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi nchini.

Pia, wameweka wazi kuwa Dkt.Magufuli amekuwa ni Rais  wa mfano wa kuigwa na viongozi wengine Duniani hasa ndani ya bara la Afrika katika kupambana na vitendo vya rushwa, ufisadi na kupigania haki na maisha ya wananchi wa kipato cha chini.

Kauli hiyo imetolewa kwa wakati tofauti na viongozi hao ambao kwa sasa ni wanachama wa CCM, wakati wakizungumza katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Tisa wa UVCCM Taifa uliofanyika leo Mjini Dodoma.

Akizungumza David Kafulika aliyewahi kuwa mbunge wa CHADEMA jimbo la Kigoma kusini na kwa sasa amejiunga na CCM, amewambia watanzania kwamba kiwango cha vitendo vya rushwa nchini kimeshuka kutokana na juhudi za Dkt. Magufuli katika kupambana na vitendo hivyo na kusimamisha haki na usawa kwa watu wote.

“ CCM ya sasa imerejesha matumaini ya Watanzania wengi, na imekuwa ni kitovu cha kusimamia misingi ya haki na usawa kwa wote.”, ameeleza Kafulila na kuongeza kuwa wapinzani kwa sasa hawana hoja wala muelekeo wa kuongoza kuisaidia nchi.

Amewashauri UVCCM kuendeleza kwa vitendo ndoto za Dkt. Magufuli za kuijenga Tanzania mpya,  itakayokuwa kisima cha amani na ukuaji wa kasi wa uchumi wa nchi.

Naye Mbunge wa zamani wa CUF jimbo la Kinondoni Maulid Mtulia ambaye kwa sasa amejiunga na CCM , amesema  kuwa amejivua nafasi zote za uongozi ndani ya CUF, kwa ajili ya kuunga mkono sera za Chama Cha Mapinduzi ambazo ni mkombozi kwa maendeleo endelevu ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Amemuomba Dkt. Magufuli awapuuze wapinzani wanaokesha wakisambaza kauli za upotoshaji kuwa amewanunua viongozi wa upinzani ili wajiunge na CCM jambo ambalo alidai sio kweli bali ni hoja za kufilisika kisiasa.

   “ Wengi wanajiuliza kwa nini tumetoka upinzani na tukajiunga na CCM, jawabu la hoja hiyo ni kwamba tumeona upinzani hauna sera wala dhamira ya dhati ya kuwasaidia wananchi  zaidi ya propaganda za kuingiza nchi katika migogoro na machafuko yasiyokuwa ya lazima.”,ameeleza Mtulia.

Kwa upande wake Albert Msando aliyewahi kuwa mwanasheria mkuu wa ACT na mshauri wa sheria wa chama hicho, amesema vijana wa Chama cha Mapinduzi wanatakiwa kuwa kioo kutazamia mambo mema yatakayoiletea nchi mafakinio ya Nyanja mbali mbali za kiuchumi ,kisiasa na kijamii.

Ameongeza kuwa juhudi,maarifa na fikra zenye muelekeo wa kimaendeleo kwa UVCCM ndio sababu pekee ya kuwatofautisha vijana wa Chama cha Mapinduzi na Vyama vya upinzani.

Akitoa ushuhuda wake aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) Patrobas Katambi na kwa sasa amejiunga na CCM, amesema Dkt. Magufuli ni miongoni mwa viongozi bora walioshushwa na mwenyezi Mungu ili wasimamie haki za wananchi bila ubaguzi.

“ Viongozi wa upinzani wanashindwa kuongoza familia zao je kweli wakipewa nchi wataweza kuiongoza hata kwa wiki moja, lazima tupime na kuangalia uwezo wa vyama vyetu vya kisiasa nchini.”, amefafanua Katambi.

Wanachama hao kwa pamoja wameahidi kuunga mkono sera, itikadi, miongozo na Katiba ya CCM pamoja na maelekezo mbali mbali yanayotolewa na viongozi na makada wakuu wa CCM.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni