RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali
Mohamed Shein ameendelea kutoa pongezi kwa timu ya Taifa ya Zanzibar, ‘Zanzibar
Heroes’ kwa kuirudishia Zanzibar heshima yake na sasa imekuwa inasemwa vizuri
kutokana na jinsi timu hiyo ilivyoonesha kiwango safi cha kusakata soka.
Dk. Shein aliyasema hayo leo huko katika viwanja vya Ikulu
mjini Zanzibar katika chakula maalum cha mchana alichowaandalia wachezaji wa
Timu ya Zanzibar Heroes pamoja na viongozi wake wote baada ya kufanya vyema katika
mashindano ya mwaka huu ya Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’
yaliofanyika nchini Kenya.
Aliongeza kuwa wachezaji hao wa ‘Zanzibar Heroes’
wamewawakilisha vizuri Wazanzibari wote kutokana na uwezo na nguvu ya mpira
waliouonesha na hadi kufikia fainali za mashindano hayo ya CECAFA.
Dk. Shein ameeleza
kuwa watu waliowengi hawakuifikiria timu hiyo ya Zanzibar kama itafika
ilipofika na pia baadhi ya watu hawakuwa wakiisema vizuri lakini hatimae
imedhihirisha kuwa Zanzibar ina historia nzuri ya soka na kuondosha usemi kuwa
‘Chenga twawala’.
Aidha, Dk. Shein amesema
kuwa kuwaandalia chakula hicho cha mchana hivi leo ni mwanzo tu wa
pongezi zake lakini kuna zawadi tatu kubwa amewaandalia ikianzia taarab maalum
ya kikundi cha Taifa cha Zanzibar pamoja na zawadi nyengine mbili kubwa ambazo
hazijawahi kutokea na kukataa kuzitaja hii leo na kuahidi kuzitaja hapo kesho.
Nae Kocha Mkuu wa Zanzibar Heroes Hemed Suleiman Moroko
ametoa pongezi kwa Rais Dk. Shein pamoja
na kwa viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kocha Abdulkhani
Msoma pamoja na Mwalimu Abdalla Mwinyi kutokana na nasaha zake za kutaka
wachezaji wawe na silka na hulka za Kizanzibari wakiwa katika mashindano hayo
ambazo ndizo zilizowasaidia.
Pamoja na hayo, Kocha mkuu huyo ametoa ombi maalum kwa Rais Dk. Shein kumualika Rais wa
Shirikisho la Soka Barani Afrika Ahmad Ahmad kuja Zanzibar ili kufanya
mazungumzo nae kwa ajili ya kuzungumza mustakbali wa Zanzibar katika soka
kimataifa.
Wakati huo huo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla
Juma Mabodi ameeleza kwamba kwa niaba ya CCM Zanzibar anaipongeza Timu hiyo kwa
kulinda heshima ya Zanzibar katika mashindano ya CECAFA.
Dk. Mabodi ameeleza kuwa kutokana na uwezo wa soka
ulioonyeshwa na vijana hao, unatoa taswira halisi ya kuwa Zanzibar inastahiki
kuingia katika orodha ya nchi za Afrika zinazotakiwa kushiriki bila vikwazo
katika soka la kimataifa.
" Chama cha Mapinduzi Zanzibar kinawapongeza kwa mara
nyingine tena wachezaji na viongozi wote walioshiriki katika mashindano hayo na
kuibuka mshindi wa pili kwani hatua hiyo ni kubwa sana kwa nchi yetu kwani
mmerejea historia ya Zanzibar ya mwaka 1995 ambapo timu yetu ilitwaa kombe la
chalenji", alisema Dk. Mabodi.
Pamoja na hayo Naibu Katibu Mkuu huyo amewasihi vijana mbali
mbali nchini kuachana na vikundi viovu badala yake watumie sekta ya michezo
hasa Soka kujiajiri wenyewe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni