MWENYEKITI wa CCM Taifa, Dkt. John Pombe Magufuli akifungua Mkutano wa Tisa wa Umoja wa Wazazi CCM Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa JK -Dodoma. |
NA IS-HAKA OMAR, DODOMA.
MWEYEKITI wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Dkt. John Pombe
Magufuli ameuagiza Umoja wa Wazazi Tanzania kusimamia kikamilifu maadili na
malezi ya kijamii nchini.
Agizo hilo amelitoa wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Tisa wa
Umoja huo uliofanyia leo Mjini Dodoma, amesema viongozi watakaochaguliwa
kupitia mkutano huo ambao ni maalum kwa ajili ya uchaguzi wakemee vitendo vya
mmonyoko wa maadili na kurejesha mfumo wa malezi bora katika jamii.
Amesema kuwa ni aibu kuona maadili ya kijamii yaporomoka
wakati CCM ina chombo chake ambacho ni Umoja wa Wazazi ambao kwa mujibu wa
Katiba ya Chama umoja huo una wajibu wa kusimamia suala la maadili ya kijamii
ili kujenga nchini yenye watu waojiheshimu na kuheshimiwa na mataifa mengine.
Kupitia hotuba yake hiyo Dkt. Magufuli amehoji wajibu wa
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) yenye mamlaka ya kufungia chombo
chochote cha habari kinachoonyesha, kutangaza na kutoa taarifa zinazokwenda
kinyume na maadili ya Kitanzania na kuwataka kuchukua hatua mara moja.
Pia ameitaka Wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo
kujitathimini kisha kuchukua hatua kwa kuhakikisha wanadhibiti vitendo vyote
vinavyohatarisha maadili ya kijamii nchini.
“ Umoja wa wazazi simamieni maadili ya nchi yetu na hilo ni
moja ya jukumu lenu, kama mnashindwa kuchukua hatua basi pigeni japo kelele na
kukemea wapo watu watakusikieni na kubadilika kitabia lakini sio kukaa kimya huku nchi
inaangamia.
Hivi sasa mzazi unashindwa hata kuangalia TV ukiwa na watoto
wako kutokana na picha chafu za baadhi ya watu wanaokuwa wakicheza wakiwa
wamevaa nusu uchi.”, amesema Dkt. Magufuli na kuhoji TCRA na Wizara ya habari
kwa nini hawachukui hatua hata ya kuvifungia vyombo vya habari vinavyochangia
kuporomoka kwa maadili.
Dkt. Magufuli ambaye pia ni Rais wa jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, amewasisitiza Wajumbe wa Mkutano Mkuu huo kuhakikisha wanachagua
viongozi bora watakaomaliza haraka changamoto zinazokabili umoja huo.
“ Usimchague mtu kwa ajili ya mtu mwingine wala fedha zake
bali chagueni viongozi imara wenye uthubutu na ujasiri wa hata kuikosoa na kuielekeza
serikali mambo mema yenye manufaa kwa wananchi wote”, amesisitiza Dkt.
Magufuli.
Amesema yeye ni Mwenyekiti wa Chama hicho hana kiongozi
yeyote wala kundi analolipigia debe lichaguliwe hivyo kiongozi yeyote atakayechaguliwa kwa njia ya
halali ndiye atakayefanya naye kazi.
“Asije mtu huko akawadanganya kuwa eti Mwenyekiti ama
kiongozi yeyote wa ngazi za juu katoa maelekezo achaguliwe mtu Fulani.”,
ameeleza Dkt. Magufuli.
Akiendelea kufafanua Rais Magufuli amewambia Wajumbe hao kuwa uchaguzi huo ni
muhimu sana kwa maisha na ustawi wa maisha marefu ya CCM na umoja huo na
kuwasisitiza kufanya maamuzi sahihi ya viongozi watakaopambana na kushinda
vikwazo vilivyomo katika mfumo wa vyama vingi vya kisiasa nchini.
Amesema wanatakiwa kuwachagua viongozi wenye uwezo na msimamo
wa kukemea hadharani vitendo vya rushwa na ufisadi ndani ya Umoja wa Wazazi,
Serikali na Chama cha Mapinduzi kwa ujumla.
Ameeleza kwamba
anathamini umuhimu wa jumuiya hiyo ambayo ndio nguzo na chimbuko la ukomavu wa
kisiasa wa CCM kwani imeanzishwa toka mwaka 1955 na waasisi wa Chama hicho kwa lengo
la kusimamia mwenendo wa maadili ya chama hicho.
Aidha ameahidi kuwa ataendelea kushikamana na jumuiya hiyo
kwa lengo la kuhakikisha inakuwa na nguvu zaidi kupitia rasilimali zake za
kiuchumi na zinawanufaisha watu wote.
Kupitia mkutano huo ametangaza neema kwamba atazipa haki sawa
jumuiya zote za chama hicho hasa katika nafasi za uteuzi wa Wabunge wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ili waweze kuwa na uwiano sawa katika chombo cha kufanya
maamuzi na kutunga sheria.
Mapema akizungumza Mwenyekiti wa Umoja huo kabla ya kujiuzulu
kupisha uchaguzi huo, Abdalla Bulembo amesema licha ya umoja huo kukabiliwa na
changamoto nyingi lakini amemaliza uongozi wake umoja huo ukiwa na akiba ya
fedha shilingi bilioni 2.1 .
Pia, ameeleza kwamba katika upande wa sekta ya elimu umoja
huo unamiliki shule 54 kikiweo Chuo
kimoja kinachotoa mafunzo ya kuwajengea ujuzi wa kujitegemea vijana ambacho
kinatoa taaluma kwa ngazi ya cheti na stashahada.
Mwenyekiti huyo alisema katika ziara mbali mbali zilizofanya
na Umoja huo Tanzania nzima wamefanikiwa kuvuna wanachama 800,795 ambao ndio
mtaji wa kisiasa wa umoja huo, sambamba na kupunguza madeni kwa asilimia 65 waliyokuwa
wakidawa na mashirika mbali mbali ya umma na binafsi.
Sambamba na hayo Mwenyekiti huyo Bulembo anayemaliza muda
wake wa kuongoza Umoja huo, amempongeza Dkt. Magufuli kwa juhudi zake za
kuwaunganisha Wanzania na kuwa mzalendo wa kweli katika kupigania haki za
wanyonge.
Mkutano huo umeudhuriwa na wawakilishi wa Vyama mbali mbali
vya upinzani ambavyo ni marafiki wa Chama cha Mapinduzi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni