MWENYEKITI wa Chama
cha Mapinduzi (CCM) Taifa Dkt. John Pombe Magufuli amewataka viongozi wapya
watakaochaguliwa kupitia Mkutano Mkuu wa Umoja huo kutobweteka na badala yake
waanzishe miradi mikubwa ya kiuchumi itakayotoa fursa za ajira kwa vijana na
wananchi kwa ujumla.
Agizo hilo amelitoa leo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Tisa
wa UVCCM Taifa uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango mjini Dodoma, Dkt.
Magufuli amebainisha kwamba umoja huo umejaliwa kuwa na bahati ya kumiliki
rasilimali nyingi lakini cha kusikitisha zinawanufaisha wa wachache huku kundi
kubwa la vijana naishi bila ajira.
Amesema sasa ni wakati
wa UVCCM kufungua ukurasa mpya wa kuwachagua viongozi waadilifu na wachapa kazi
watakaoweza kusimamia uhai na ustawi wa umoja huo ili uweze kuwatumikia vijana
wote bila ya ubaguzi.
Dkt. Magufuli ambaye ni
Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania amesema umoja huo utakuwa na
nguvu endapo utapata viongozi wenye uthubutu wa kupinga vitendo vya
rushwa,ufisadi pamoja na makundi yasiyofaa ndani ya umoja huo.
“ Anzisheni miradi sisi mkitujia mnataka msaada tupo tayari
kuwasaidia na sijawahi kuwaona mkitaka msaada, lakini najua wenda baadhi yenu mliogopa
kuomba msaada kutokana na matendo yenu ya kuhujumu mali za UVCCM.
Lazima tuambizane ukweli kuwa rasilimali nyingi za UVCCM
zinaishia mikononi mwa wajanja huku vijana wengi ambao ndio kundi kubwa
hawanufaiki.”, alieleza Dkt. Magufuli.
Aliwambia vijana hao kuwa ndio tegemeo la CCM katika kujenga
taifa huru kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Aliweka wazi kuwa serikali ya awamu ya Tano anayoiongoza
inawathamini vijana kuliko wao wanavyofikiria ndio maana amekuwa akiwateuwa
katika nafasi mbali mbali za uongozi.
“Huu ni wakati wenu vijana wa kilipeleka mbele taifa letu
kiuchumi kwani wengi wenu mna ujuzi na maarifa tofauti, fanyeni kazi kwa bidii
ili nchi yetu iwe imara kiuchumi.
Lakini pamoja na yote hayo Mimi na Rais mwenzangu Dk.Shein
hatuwezi kukubali kuiacha nchi katika mikononi mwa viongozi mafisadi na wala
rushwa, hata waasisi wetu wa ASP na TANU huko waliko hawatoridhika.”, amesema
Dkt. Magufuli.
Amefafanua kwamba UVCCM inahitaji viongozi wenye uzalendo
uliokidhi sifa za uwajibikaji, waadilifu na wenye uthubutu wa kujenga hoja
zenye fikra za kuwanufaisha vijana wa makundi yote.
Amewatanabaisha kwamba endapo watachagua viongozi wala rushwa
na walioingia madarakani kwa hongo basi wakubali kuumia kwa miaka mitano ijayo.
Hata hivyo alieleza kwamba CCM inatambua mchango mkubwa wa
vijana wake katika kulinda na kupigania maslahi ya chama kisiasa na kijamii,
hivyo hatowaangusha bali ataendelea kushirikiana nao kwa kila japo.
Mapema akisoma taarifa ya utekelezaji ya UVCCM ya kipindi cha
miaka mitano iliyopita Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Shaka Hamdu Shaka,
alisema umoja huo umekuwa mstari wa mbele katika kujenga itikadi, imani na
kudumisha uzalendo kwa vitendo.
Amesema umoja huo unajiuvunia kuwa na Marais wenye imani na
mapenzi ya kweli kwa wananchi wanaowangoza ambao wapo tayari kuwapigania ucku
na mchana ili waweze kunufaika na rasilimali zilizopo nchini.
Shaka ameeleza kwamba kwa kipindi cha miaka mitano Umoja huo
umejiimarisha katika Nyanja mbali mbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa na
kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa kitovu cha amani na utulivu wa kudumu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni