WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Zanzibar jana walijitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura za
maoni ndani ya chama hicho, ili waweze kuteuliwa viongozi wa nafasi za ubunge , uwakilishi na udiwani
watakaoweza kupeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa dola unaotarajiwa kufanyika
Octoba 25 mwaka huu.
Zoezi hilo lililoanza majira ya
saa 2:30 asubuhi ya jana katika vituo mbali mbali vilivyokuwa katika matawi ya Chama hicho pamoja na shule kulimiminika wafuasi wa CCM wakiwa na ari za kuwachagua viongozi bora
watakaoweza kutatua changamoto zinazowakabili katika majimbo.
Akizungumza na UHURU Naibu katibu
mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai mara baada ya kupiga kura katika Tawi la
Magomeni Unguja, alisema ameridhishwa na muamko wa wanachama wa chama hicho
jinsi walivyojitokeza katika vituo mbali mbali kwa lengo la kuwachagua viongozi
wanaowaamini kuwa wana nia thabiti ya kuleta maendeleo na kusimamia Ilani ya uchaguzi
ya CCM kwa vitendo.
Alisema kuwa hali hiyo inaonyesha
taswira halisi ya umoja na mshikamano uliopo ndani ya chama hicho unaoendelea
kujenda demokrasia pana kwa kutoa fursa ya kira mwanachama kupata haki yake ya
kuchagua na kuchaguliwa bila ya kuwekewa vikwazo.Vuai alifafanua kuwa matarajio ya
chama hicho ni kuhakikisha kila kada mwenye sifa za kupiga kura ya maoni katika
eneo husika wanapata haki hiyo bila ya kuwekewa vikwazo ili kuweza kukamilisha
zoezi hilo kwa ufanisi na wakati uliopangwa.
“ Matumaini yetu ni kuhakikisha
zoezi hili linafanyika vizuri na kumalizika bila ya matatizo licha ya kuwa
mchakato wowote wa kidemokrasia hasa uchaguzi hauwezi kukosa kasoro kwa sababu
ni jambo ambalo lipo katika usimamizi wa binadamu lakini kama kutajitokeza changamoto lazima zitafutiwe ufumbuzi wa
kudumu.
CCM imetoa mafuzo mbali mbali kwa mawakala na wagombea wa nafasi mbali mbali pamoja na kuchapisha Makala mbali mbali zinazoelezea kanuni na taratibu za kura za maoni ndani ya chama chetu, hivyo bado tuna imani kuwa zoezi hili litafanyika kwa mujibu wa matarajio yetu kwa mujibu wa maandalizi yake.”, alisema Vuai na kuwapongeza wanachama wa Chama wa Zanzibar Unguja na Pemba kwa kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura za maoni.
Naibu katibu mkuu huyo Vuai
alitoa ufafanuzi juu ya malalamiko ya
baadhi ya wanachama kwa baadhi ya vituo kuchelewa kuanza kupiga kura hizo,
alisema kuwa kasoro hizo haziwezi kuzuia wanachama hao wasipige kura kwani
atafuatilia kwa makatibu wa wilaya na mikoa kuhakikisha wanaongeza muda kwa
vituo vilivyochelewa kuanza.
Vuai alisema kuwa baadhi ya
maeneo ikiwemo Jimbo la Mahonda Wilaya ya kaskaszini “B’” Unguja mchakato huo
umegubikwa na kasoro zilizosababisha kuhairishwa kupigwa kwa kura hizo mpaka
viongozi watakapoweza kutatua kasoro hizo.
Alizitaja kasoro hilo kuwa ni
kutokana na baadhi ya wagombea ndani ya jimbo hilo kuanza kuchafuana katika
vituo vya kupigia kura hali iliyosababisha kuhairishwa kwa zoezi hilo mpaka
kesho(leo).
Nao wananchi katika tawi la CCM Mpendae walilalamikia suala la kuchelewa kuanza kupiga kura hizo kutokana na kuchelewa kufikishwa vifaa jambo ambalo walisema linaweza kuharibu mchakato huo kwani baadhi ya wanachama wanaweza kususa kupiga kura.
Kwa upande wake Issa Hassan
Masoud mkaazi wa jimbo la Mpendae alisema kuwa wananchi wamekaa katika kituo
hicho kwa muda mrefu bila ya kupiga kura jambo ambalo linaweza kusababisha
athari ya kuonekana CCM haikujipanga na zoezi hilo na kutoa fursa ya vyama vya
upinzani kukichafua chama hicho.
Mkaazi kwa upande wake mkaazi wa
Jang’ombe Urusi, Saada Kassim Haji alisema kuwa katika kituo hicho zoezi hilo
limeendelea vizuri kwani vifaa na wasimamizi wa vituo wamefika mapema na kuanza
kupiga kura hizo bila ya usumbufu.
Kwa upande wake Katibu wa wilaya
ya Amani kichama Unguja, Abdalla
Mwinyi alisema zoezi hilo limeendelea
vizuri katika wilaya hiyo licha ya kujitokeza kwa changamoto ya kuchelewa
kuanza kwa baadhi ya vituo kutokana na sababu ambazo zipo nje ya uwezo wa
kiutendaji wa wilaya hiyo.
“ Wanachama wanaendelea kupiga
kura na tunapata faraja kuona wamejitokeza kwa wingi katika vituo mbali mbali
vilivyopo katika wilaya yetu, hivyo matarajio yetu ni kuhakikisha zoezi hili
linakamilika”, alisema Mwinyi.
Naye Katibu wa idara ya Itikadi
na uenezi NEC Zanzibar, Waride Bakar
Jabu alizungumza na gazeti hili baada ya kumaliza kupiga kura katika
kituo cha Tawi la Kiembe samaki, aliwataka wananchi kutumia fursa hiyo vizuri
kwa kuwachagua viongozi ambao wana nia ya dhati ya kutatua changamoto
zinazowakabili.
Waride ambaye pia ni Mgombea wa
nafasi ya Ubunge Jimbo la Kiembe samaki Unguja, alisema kuwa zoezi hilo ni
miongoni mwa hatua muhimu za kuwatafuta wagombea wa chama hicho wa ngazi mbali
mbali kama kanuzi zilizomo ndani ya katiba ya CCM zinavyoelekeza.
Kwa upande wake msimamizi mkuu wa
kituo cha Tawi la Kikwajuni Unguja, Pandu Ameir Kificho aliwashauri wafuasi wa
chama hicho kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa katika vituo hivyo ili
kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima.
Alisema katika kituo hicho
wanachama wamejitokeza kwa wingi na kuhakikisha zoezi hilo linaendelea vizuri
kwani mawakala na wasimamizi wengine wa uchaguzi wamekuwa na ushirikiano kwa
kila hatua ili kuhakikisha zoezi hili linakamilika kwa wakati.
“Lazima tuhakikishe zoezi hili
linakamilika kwa wakati na matokeo yanapatikana kwa muda uliopangwa kwani
endapo patafanyika uzembe wa aina yoyote unaweza kusababisha athari ya
kutokamilika kwa zoezi hilo kwa wakati”, alisema Kificho.
Kwa mujibu wa uchunguzi
uliofanywa na katika vituo mbali mbali umebaini kuwepo na demokrasia
katika zoezi hilo kutokana na kila mwanachama mwenye sifa kupewa haki ya kupiga
kura hizo bila ya kuwekewa vikwazo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni