WANANCHI wa Kijiji cha Ngomeni Wilaya ya Chake Chake Pemba wamempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein kwa juhudi zake za kuimarisha huduma za msingi zilizofungua fursa za kiuchumi katika Kijiji hicho na vijiji jirani.
Wakizungumza kwa wakati tofauti mara baada ya kumaliza hafla ya ufunguzi wa Kituo cha Afya cha Ngomeni wameeleza kuwa wamefurahishwa na kasi ya Dk.Shein katika kutatua matatizo ya wananchi kwa wakati mwafaka.
Wameeleza kuwa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na SMZ katika Kijiji hicho wataituza na kuithamini ili iwahudumie wananchi mbali mbali wa Kijiji hicho.
Akizungumza mkaazi wa Kijiji hicho Bi.Mariam Juma Fakih, ameeleza kuwa Akina Mama wajawazito walikuwa wakijifungulia njiani na wengine kupoteza Maisha kutokana na ukosefu wa huduma za Afya katika maeneo ya karibu ambapo kwa sasa ameeleza kuwa changamoto hiyo tayari imetatuliwa na SMZ kwa kujenga klituo cha Afya cha Kisasa.
Naye Suleiman Haji Bakari Mkaazi wa Kijiji hicho, amesema wananchi wa maeneo hayo wanaishukuru serikali kwa kuimarisha huduma ya barabara kwani inawasaidia wakulima wa mazao mbali mbali hasa zao la Karafuu.
Pamoja na hayo Suleiman amemuomba Dk.Shein kuwasaidia wananchi hao kupata mnara wa mtandao wa simu kutokana na wananchi kukosa mawasiliano ya simu kwa sababu eneo hilo lipo bondeni jambo linalokwamisha baadhi ya harakati za kiuchumi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni