Jumatatu, 4 Februari 2019

NDG.TUNU: ASEMA MIAKA 42 YA CCM WANAWAKE WAMEKWEA KILELE CHA MLIMA WA MAFANIKIO.


 NAIBU Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Ndugu Tunu Juma Kondo akiwa Coconut FM akizungumzia miaka 42 tangu kuzaliwa kwa CCM.


NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake (UWT) Zanzibar Bi.Tunu Juma Kondo amesema katika kipindi cha miaka 42 ya Chama Cha Mapinduzi Wanawake wamekwea kilele cha mlima wa mafanikio kwa kunufaika na fursa za elimu,uongozi na kusogezewa karibu huduma za msingi za kijamii.

Kauli hiyo ameitoa leo katika mahojiano maalum ya miaka 42 ya CCM katika Kituo cha Redio ya Coconut FM kisiwani Unguja, amesema kundi la wanawake limekuwa mfano wa kuigwa katika jamii kutokana na mafanikio wanayoyapata katika awamu mbali mbali za uongozi wa Dola.

Amesema wanawake wanatakiwa kuchangamkia fursa za elimu,uongozi na ujasiriamali ili wafikie kiwango cha kujitegemea wenyewe bila kusubiri utegemezi kutoka kwa kundi la wanaume.

Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo wa UWT, amesema kundi la wanawake limetoa mchango wake katika harakati za kuasisiwa kwa CCM mnamo mwaka 1977,ambapo wanawake mbali mbali walijitokeza kuunga mkono juhudi za taasisi hiyo.

Akizungumzia baadhi ya maendeleo yaliyopatikana katika miaka 42 ya CCM,Ndugu Tunu ametaja utekelezaji wa Ilani za Uchaguzi za CCM katika vipindi tofauti vya uongozi wa dola chini ya uongozi wa ASP hadi CCM.

Amebainisha kwamba wanawake wanawake wengi wamepata nafasi za uongozi, utendaji katika taasisi mbali mbali za binafsi,Serikalini na katika Chama,sambamba na ongezeko la wanawake wengi wasomi tofauti na ilivyokuwa wakati wa enzi za ukoloni na usultani.

Akifafanua historia fupi ya CCM Naibu Katibu huyo,ameeleza kuwa baada ya kupatika kwa uhuru wa Tanganyika tarehe 9 disemba ,1961 na ule wa Zanzibar kupitia Mapindizi ya Zanzibar ya Januari 12,1964 ,kulifanya TANU na ASP viwe vimekamilisha jukumu la ukombozi wa nchi hizi kutoka katika makucha ya kisultan na ukoloni.

Anaeleza kwamba wakati huo mataifa machanga yaliishi katika hali ya ungonge lakini viongozi wake walitawaliwa na fikra za ukombozi wakipanga mikakati yao kwa siri,ili kujinasua katika utawala wa wageni, jambo lililochangia Zanzibar na Tanganyika kuungana mnamo April 26,1964.

Anasema baada ya muungano huo ikazaliwa Tanzania iliyokuwa na Vyama viwili vya ASP na TANU katika mazingira ya Chama kimoja cha siasa huku vikitambua kuwa kuna umuhimu wa kuwa na chombo madhubuti cha uongozi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Amesema baada ya viongozi wakuu wa vyama hivyo kwa wakati huo kujitathimini na kutafakari kwa kina wakaamua kuviunganisha ASP na TANU na ikazaliwa rasmi CCM.

Pamoja na hayo ameongeza kwa kueleza kuwa UWT inalaani vikali vitendo vya udhalilishaji wa Kijinsia kwa wanawake na watoto vinavyofanyika kwa baadhi ya maeneo nchini.

Amevishauri vyombo vya kisheria vinavyohusika na udhibiti wa vitendo hivyo hasa vinavyohusika na utoaji wa hukumu kwa wahalifu wa kesi za udhalilishaji kutenda haki katika utoaji wa hukumu hizo ili kutoa fundisho kwa watu wenye tabia hizo.

Naye Afisa Habari wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Ndugu Is-haka Omar Rweyemamu, amesema taasisi hiyo ya kisiasa inajivunia kuwa karibu na Vyombo vya Habari nchini,ambao ni wadau wakubwa wa kufikisha taarifa na matukio ya CCM na Jumuiya zake kwa jamii.

Ametoa wito kwa viongozi wa Chama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendeleza utamaduni wa kushirikiana vya Vyombo vya habari ili wananchi wajue namna Serikali inavyotekeleza Ilani ya CCM kupitia miradi mbali mbali ya maendeleo.











Hakuna maoni:

Chapisha Maoni