RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiweka Jiwe la Msingi Skuli ya msingi Kwarara Wilaya ya Magharibi 'B' Unguja. |
BAADHI ya Wananchi wakiwemo wanafunzi walioudhuria hafla ya uwekaji wa Jiwe la msingi katika Skuli ya msingi Kwarara. |
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein
amesema katika kutekeleza sera ya elimu bila malipo, Serikali inaendelea
na juhudi za kuimarisha miundo mbinu ya kielimu ili kwenda sambamba na mahitaji
yaliopo.
Dk Shein amesema hayo leo katika
hafla ya uwekaji wa jiwe la Msingi wa
Skuli ya msingi Kwarara, Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.
Amesema kutokana na
ongezeko kubwa la wanafunzi hali inayotokana na kiwango kikubwa cha
wakaazi wa Zanzibar hivi sasa, Serikali inalazimika kuongeza idadi ya madarasa
ili kwenda sambamba na ongezeko la wanafunzi katika skuli za msingi na
sekondari.
Amesema ongezeko la idadi ya watu
kutoka 300,000 mwaka 1964 hadi kufikia Milioni moja na nusu hivi sasa imefanya
kuwepo mahitaji makubwa ya madarasa , huku baaadhi ya skuli zikiwa na wanafunzi
wanaofikia 234 katika darasa moja,
Amesema hivi karibuni Serikali imeagiza madawati 44,000 kutoka nchini
China na kubainisha kuwa nusu ya samani
hizo zimewasili nchini na kugawiwa katika skuli za msingi na sekondari.
Dk. Shein amesisitiza azma ya
serikali na kuwataka wazazi na walezi wa wanafunzi kutokuchangia huduma zote za
kielimu katika skuli za msingi na
sekondari, ikiwemo vitabu madaftari.
Amesema lengo la serikali ni
kuwaandaa vijana wake kielimu ili kufanikisha azma ya kuwa an wataaalamu katika fani mbali mbali ili kuliwezesha Taifa
kupata maendeleo ya haraka.
Alisema uchumi wa Zanzibar umeendelea
kuimarika kadri miaka inavyosonga hatua inayotokana an makusanyo mazuri ya
mapato na kubainisha kuwa hivi sasa Serikali inakusanya kati ya shilingi Bilioni 65 hadi 70 kwa mwezi, hivyo
kumudu gharama za uendeshaji wa miradi
mbali mbali ya maendeo, ikiwemo ya maji na barabara.
Amesema hali hiyo imechangia
kufanikisha azma ya serikali ya kusomesha wataalamu wake katika fani tofauti,
ikiwemo madaktari.
Akigusia historia ya elimu nchini,
Dk. Shein amesema Mapinduzi ya 1964 yamekuja kuwakomboa watoto wa wanyonge
kutokana an dhuluma ya kukoseshwa elimu.
Ameeleza wakati chama cha ASP
kikipigania uhuru, kilibainisha wazi katika Ilani zake, dhamira ya kuipa
kipaumbele elimu na kutolewa bila malipo.
Alisema elimu ina umuhimu mkubwa
katika maisha ya binadamu, kama Mwenyezi Mungu alivyobainisha katika kitabu
kitakatifu cha Quran.
Amesema ni lengo la Serikali katika
siku zijazo kujenga skuli za msingi za ghorofa, ili kukidhi mahitaji kutokana
na ufinyu wa ardhi uliopo.
Dk. Shein alichukuwa fursa hiyo
kuipongeza taasisi ya Good Neighbor kutoka Jamuhuri ya Korea Kusini kwa msaada mkubwa wa kufanikisha
ujenzi wa skuli hiyo.
Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali,
Riziki Pembe Juma amesema Wizara hiyo kwa kushirikiana Wizara ya Nchi (OR)
Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa, Tawala za Mikoa, idara maalum na Vikosi vya SMZ pamoja na Jamuhuri ya Korea italiendeleza jengo hilo katika
awamu inayofuata.
Waziri Pembe amesema Rais Dk. Shein
kuwa huduma za kielimu pamoja na vitabu na madaftari zitaendelea kutolewa bure
nchini kote ili kwenda sambamba na Sera ya Elimu.
Mapema,Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
elimu na maunzo ya Amali Madina Mjaka, amesema ujenzi wa skuli hiyo itawasogeza
wanafunzi karibu na makazi, kama
ilivyoainishwa kwenye ilani ya CCM.
Aidha, amesema itapunguza mlundikano
wa wanafunzi wa skuli za jirani, hususan Kijitoupele, ambapo kwa sasa darasa
moja hujumuisha hadi wanaafunzi 100 – 120.
Ameeleza kuwa awamu ya kwanza ya
ujenzi wa skuli hiyo umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 1.5, ambapo skuli
hiyo inatarajiwa kuchukuwa wanafunzi 3,780.
Aidha alisema katika kufanikisha
ujenzi wa skuli hiyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetowa msamaha wa vifaa
vya ujenzi pamoja na kuchangia samani.
Wakati huo huo, Dk Shein ameendelea na
ziara yake kwa uwekaji wa Jiwe la msingi wa Kituo cha Afya Magirisi, Wilaya ya
Magharibi ‘B’ Unguja.
Akizungumza na wananchi Dk. Shein
amesema ujenzi wa kituo hicho cha Afya ni jambo la faraja kwa wananachi wa Jimbo
la Kijitoupele, akiwashukuru viongozi wa jimbo hilo kwa uamuzi wao wa busara.
Amesema Ilani za Uchaguzi za Chama cha
ASP za mwaka 1961 na 1965 ziliweka bayana azma ya Serikali kutowa huduma za Afya bila malipo, jambo ambalo Serikali ya
Mapinduzi inaliendeleza.
Ameeleza kuwa Mapinduzi ya 1964
yameleta mabadiliko makubwa katika sekta ya Afya na elimu, mbali na kuwepo kwa changamoto ya
ongezeko la watu hapa nchini.
Akinasibishana kauli hilo, Dk. Shein alisema kituo hicho
kina uwezo wa kutoa huduma kwa wastani wa watu 15,000 pekee hivyo hakitoshelezi
mahitaji kwa kuzingatia wananchi 93,119
wanaotarajiwa kukitumia.
Ameishukuru taasisi ya Direct AID
kutoka Kuwait kwa kuunga mkono juhudi za viongozi wa jimbo hilo baada ya
kukubali kukamilisha hatua iliypobaki ya ujenzi.
Alisema kituo hicho kitakapokamilika
kitaweza kutoa elimu ya kinga ya maradhi mbali mbali na kubainisha wazi
upatikanaji wa uhakika wa dawa, kutokana na juhudi za Serikali za kuimarisha
bajeti ya Wizara ya Afya katika mwaka wa fedha unaoendelea.
Amesema katika mwaka wa fedha wa
2018/19 Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 12.7 kwa ajili ya kuimarisha huduma za Afya,
hususan katika suala zima la upatikanaji wa dawa, akibainisha huduma zote
muhimu ikiwemo uchunguzi wa magonjwa mbali mbali kupatikana bure.
Dk. Shein ameiagiza Wizara ya Afya
kujiandaa vyema, ili pale kituo hicho kitakapofunguliwa kiwe na waataalamu na
wafanyakazi wanaotosheleza ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Nae, Mkuu wa Wilaya ya Maghribi “B”
Kepteni Silima Haji Haji amesema ujenzi wa kituo hicho kwa kiasi kikubwa
kutavipungumzia mzigo vituo vyengine , ikiwemo kituo cha Afya Mwera katika
kutoa huduma za Afya.
Mapema, Waziri wa Nchi (OR)Tawala za
Mikoa, Serikali za Mitaa, Idara maalum na Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir
amesema Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara Afya itajenga uzio pamoja na
kukipatia wataalamu an wafanyakazi kituo hicho.
Ameipongeza taasisi ya Direct Aid kwa
kuendelea kutoa misaada ya kijamii kwa
wananchi wa Jimbo la Kijitoupele baada ya kufanikisha ujenzi wa kisima.
Nae, Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa
Magharibi “B” Ali Abdalla Said amesema ujenzi wa kituio hicho umegharimu zaidi
ya shilingi Milioni 90 ambapo miongoni mwa fedha hizo zinatoka Halmashauri
na mfuko wa Jimbo kupitia Mbunge na
Mwakilishi wa Jimbo la Kijitoupele.
Amesema ni matarajio ya kituo hicho
pale kitakapokamilika kuweza kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wapatao
93,119.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni