BAADHI ya Wajumbe wa Kamati Tekelezaji wa UWT Wilaya ya Dimani wakiwa katika hafla ya kupokea wanachama wapya ndani ya Wilaya hiyo.
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar
kimesambaratisha ngome ya Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) kwa kuwang’oa
vigogo Saba na Wanachama mbali mbali wa Chama hicho.
Vigogo hao waliong’oka kutoka
Chama Cha ukombozi wa umma(CHAUMMA) ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja
wa Akina Mama Taifa wa Chama hicho Ndugu Salma Mohamed Juma, Mwenyekiti wa
Vijana wa Wilaya ya Mjini wa Chama hicho Ndugu Salamuu Abdalla Juma.
Wengine ni Katibu wa Vijana
Wilaya ya Mjini ndugu Mwanabaraka Ali
Mohamed, Mjumbe wa chama hicho Wilaya ya Mjini Shadya Juma Khamis, Mjumbe wa
Chama hicho Mkoa wa Magharibi Mariam
Peter John pamoja na Mjumbe wa ngazi ya wilaya ya Mjini Raya Ali Masoud.
Viongozi hao wa CHAUMA leo
wamejiunga rasmi na CCM na kupewa kadi za Chama Cha Mapinduzi na Umoja wa
Wanawake wa Tanzania(UWT) hafla iliyofanyika katika Afisiu ya UWT Wilaya ya
Dimani Unguja.
Akizungumza mara baada ya
kujiunga na CCM, aliyekuwa Mwenyekiti wa Wanawake CHAUMA Taifa, ndugu Salma
Mohamed Juma, amekiri kwamba sababu ya kurejea CCM ni kutokana na Utekelezaji
mzuri wa Ilani ya CCM unaosimamiwa na Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein
pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli.
Ndugu Salma ameweka wazi kwamba
mwananchi yeyote ambaye ni mzalendo,mpenda maendeleo ,anayechukia rushwa na
ufisadi kwa vitendo hawezi kuendelea kubaki katika Vyama vya upinzani na ndio
msaana wao wakaamua kujitoa na kujiunga na CCM.
Kupitia hafla hiyo Kigogo huyo,
ametoboa siri ya vyama vya upinzani hasa vilivyounda UKAWA alidai kwamba Chama
hivyo vinaongozwa na viongozi mafisadi, wala rushwa,wabinafsi na mawakala wa
Mataifa ya kigeni yenye mikakati ya kuhujumu uchumi na maendeleo ya Zanzibar na
Tanzania kwa ujumla.
“Leo najihisi kama nimetoka jela
kwani huko tulipokuwa kulikuwa hakuna Demokrasia, Uhuru wa kutoa na kupokea
maoni wala kumthamini Mwanamke kama mtu anayesitahiki haki na fursa kama
walivyo watu wengine,,,baada ya kunyanyaswa kisiasa kwa muda mrefu ndani ya
CHAUMA tumeamua kurudi katika Chama chetu cha asili kinachojali utu na haki za
watu wote ambacho ni CCM.
Nimekuwa kiongozi wa ngazi za juu
ndani ya CHAUMA nimekutana na vikwazo vingi mpaka nikafikia hatua ya kuacha
cheo changu na kuwa mwanachama wa kawaida ndani ya CCM mjue kuwa huko katika
upinzani sio sehemu salama ya watu wenye akili timamu kuishi nami nawakaribisha
akina mama wenzangu wajiunge na CCM taasisi huru ya kisiasa inayojali maisha ya
watu wote.”,alisema Salma.
Naye aliyekuwa kiongozi wa Vijana
wa Chama hicho Wilaya ya Mjini ndugu SalamuuAbdallah Juma, alitoa wito kwa
vijana waliopo katika vyama vya upinzani kufanya maamuzi sahihi ya kujiunga na
CCM kabla ya mwaka 2020 ili wapate uwanja mpana wa kunufaika na fursa mbali
mbali za kimaendeleo.
Alisema Vyama vya upinzani vinawaandaa
vijana kuwa mabalozi wa vurugu,uchochezi,fitna na siasa za jino kwa jino na sio
kuwarithisha elimu na nafasi za uongozi kama kilivyo Chama Cha Mapinduzi.
“ Mimi ni kijana nimeamua kwa
ridhaa yangu kujiunga na CCM ili kusaidiana na vijana wenzangu wa Chama
hiki kuendeleza mambo mema ya kuzijenga
kiuchumi na kijamii nchi zetu,sambamba na kulinda kwa vitendo dhana ya Umoja na
Utulivu kwani ndio chimbuko la maendeleo ya taifa lolote.
Akipokea wanachama hao wapya wa
CCM, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdalla Juma Saadalla ‘Mabodi’ ,
ameeleza kwamba Chama Cha Mapinduzi ndio kimbilio la wananchi wa makundi yote
katika jamii.
Ameeleza wananchi wanaotoka
katika vyama vya upinzani na kujiunga na CCM sio kwa bahati mbaya wala
kushawishiwa bali wanajiunga na taasisi hiyo kutokana na mifumo imara ya
kisiasa inayoongoza sera za maendeleo ambazo ni kivutio kwa wananchi wa rika
zote.
Alisisitiza kuwa Wapinzani
wataendelea ‘kupata tabu sana’ kwani wapo wafuasi wa vyama hivyo makundi kwa
makundi wakiwemo vigogo wa ngazi za juu wapo tayari kujiunga na CCM visiwani
Zanzibar ambapo kwa sasa wanaandaliwa utaratibu wa kikatiba ili waweze kurudi
CCM.
Aliweka wazi kwamba CCM
inaendeleza msimamo wake wa kipigo kama kile cha kimbunga cha ‘Sunami’ ndani ya
vyama vya upinzani kwa kuhakikisha kabla ya mwaka 2020 vyama hivyo vinabaki
bila wanachama na hatima yake vinakosa sifa ya kuwa wawakilishi wa wananchi.
Ameeleza kwamba wanawake wa
kiafrika kwa upande wa Zanzibar walidhalilishwa,kudhulmiwa na kuteswa kwa muda
mrefu kabla ya Mapinduzi suala lililoondolewa na Chama cha ASP iliyoungana na
TANU kasha kuzaliwa kwa CCM inayowathamini wanawake na kuwapa haki na fursa
zote za kiuchumi,kijamii na kisiasa.
Dk.Mabodi alieleza kwamba
Wanawake wana historia kubwa na ya kipekee ndani ya CCM kwani kundi hilo ndio
lililoshiriki kwa kiasi kikubwa kufanikisha Mapinduzi ya Januari 12,mwaka 1964
yaliyowapatia haki,utu na fursa za kimaendeleo jamii ya wakwezi, wakulima na
wafanyakazi.
Aliongeza kwamba mbali na hilo
Wanawake ndio walioshiriki kuchangia fedha za kujenga jingo la Afisi Kuu ya CCM
Zanzibar kisiwandui kwa michango ya fedha kupitia jumuiya ndogo ndogo za Akina
mama kwa wakati huo.
Akitaja tathimini ya uchapakazi kwa wanawake
wa UWT alisema wamekuwa wakipigania asilimia 50 kwa kila Nyanja na kwa sasa
tayari kinadharia wamefikia asilimia 30 na kwa vitendo wamefikia asilimia 60
hatua ambayo ni ya kupongezwa na kila mpenda maendeleo na umoja na mshikamano.
Katika maelezo yake Dk.Mabodi
amesisitiza umuhimu wa Vijana kuthamini Tunu za Taifa ambazo ni Muungano,
Mapinduzi, Utu pamoja na Lugha ya Taifa kwani mambo hayo ndiyo yanayochochea
umoja na mshikamano kwa wananchi.
Alisema wananchi wanatakiwa
kutathimini na kuweka katika uzani mambo yanayotekelezwa na CCM na walinganishe
na yale yanayofanywa na Vyama vingine vyenye ruzuku Kisha 2020 watoe hukumu
sitahiki kwa kila taasisi ya kisiasa nchini.
Aidha amewakumbusha akina Mama
hao kuchangamkia fursa za kuanzisha vikundi vya ujasiriama ili wanufaike na
mikopo nafuu kutoka Serikalini ambayo kwa sasa zimetengwa kiasi cha shilingi
bilioni 3.6 kwa ajili ya vikundi.
Sambamba na hayo amewasihi
wanawake wa UWT katika Wilaya ya Dimani kuachana na tabia za fitna na kumakundi
ya kuwania nafasi za uongozi kwani mambo hayo yasipochukuliwa hatua za
kinidhamu yanaweza kuharibu sifa ya maendeleo ndani ya Wilaya hiyo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa UWT
Taifa Thuwayba Kisasi, aliwashukru akina mama wote waliojiunga na CCM pamoja na
umoja huo, na kuwaeleza kuwa taasisi hiyo haina ubaguzi wala siasa za chuki na
visasi hivyo akawasihi akina mama na vijana warudi nyumbani kumenoga.
Awali Naibu Katibu Mkuu wa UWT
Zanzibar ndugu Tunu Juma Kondo, aliseleza kwamba kipaumbele mahsusi cha taasisi
hiyo ni kuongeza wanachama kwa wingi ndani ya CCM na UWT ili 2020 CCM iendelee
kushinda na kubaki madarakani.
Akizungumza Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Magharibi Ndugu Zainab Ali Maulid amesema Akina Mama ndani ya Mkoa huo wamekuwa na muamko mkubwa wa kushiriki katika shughuli mbali mbali za kimaendeleo zinazowapatia fursa za kujifunza masuala mbali mbali ya kujiwezesha wenyewe.
Alisema hafla hiyo ni miongoni
mwa mwendelezo wa ziara yake ya kujitambulisha kwa wanachama na viongozi wa CCM
na Jumuiya zake toka ateuliwe kushika nafasi hiyo, pia amewashukru wanachama
wote walioshiriki katika mapokezi yake.
Katika taarifa yao UWT Wilaya ya
Dimani, wameeleza kwamba taasisi hiyo imeanzisha miradi ya ufugaji wa kuku wa
nyama na mayai ili kuondokana na mifumo ya utegemezi wa ajira kutoka serikalini
ambapo miradi hiyo imetolewa na Wawakilishi wa Viti Maalum ndani ya Wilaya
hiyo.
Pamoja na hayo ameeleza kwamba
katika kuadhimisha miaka 42 ya kuzaliwa kwa CCM wamefanya ziara ya kuwafariji
Watoto yatima wa Kituo cha African Muslim Agency kwa lengo la kusikiliza
changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Kupitia taarifa hiyo walieleza
kuwa ndani ya Wilaya hiyo Wabunge, Wawakilishi, Madiwani, CCM,UWT,Jumuiya ya
Wazazi na UVCCM wanashirikiana katika masuala mbali mbali ya kuimarisha Chama
Cha Mapinduzi.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni