Jumatano, 13 Februari 2019

DK.SHEIN ATAKA WANA CCM KUFANYA KAZI KWA BIDII KUELEKEA 2020,DK.MABODI ASEMA MWENDO WA CCM HAKUNA WA KUUZUIA


 MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi huko CCM Mkoa wa Magharib Zanzibar.


NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akizungumza katika mkutano wa Dk.Shein na wanachama wa CCM.

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein amewata viongozi na wanachama wa CCM kufanya kazi za kuimarisha Chama Cha Mapinduzi ili kuwavutia baadhi ya wananchi ambao siyo wanachama wa CCM wajiunge na taasisi hiyo.

Rai hiyo ameitoa wakati alipozungumza na wanachama na viongozi hao, katika ukumbi wa CCM  Mkoa wa Mjini ulipo Amani  Unguja.

Amesema CCM ni taasisi kubwa Tanzania, Barani Afrika na Duniani kote hivyo ni lazima ifanye kazi zake kwa ufanisi zaidi ili kurahisisha mazingira ya kufanya shughuli za kisiasa katika michakato ya uchaguzi wa kidemokrasia nchini.

Katika maelezo yake Dk.Shein ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kutekeleza ahadi zilizotolewa katika uchaguzi Mkuu uliopita ikiwa ni sehemu ya kujipanga na uchaguzi ujao.

Dk.Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amesisitiza  umoja na mshikamano kwa wanachama,viongozi,watendaji, makada na wananchi kwa ujumla.

 Pamoja na hayo amewataka viongozi na wanachama hao kujipanga kikamilifu kwa kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kihistoria mwaka 2020,kwani kazi kubwa za kuwaletea maendeleo wananchi tayari zimeshatekelezwa kwa ufanisi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’, amesema CCM kwa sasa inatembea kifua mbele kutokana na Utekelezaji mzuri wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Aliongeza kuwa kwa sasa viongozi wa CCM wamejielekeza katika kushuka kwa wananchi wa ngazi zote kuratibu changamoto zao na kuzitatua kwa wakati tofauti na vyama vingine vinavyokesha kwa porojo na maneno ya upotoshaji.

Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo,amemuhakikisha Dk.Shein kuwa CCM kwa upande wa Zanzibar ipo vizuri na itaandika historia mpya ya ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo, ndugu Talib Ali Talib amesema ndani ya Mkoa wake amekuwa akishirikiana vizuri na viongozi wa Chama na Serikali ndio siri ya mafanikio katika mkoa huo.

Awali Katibu wa CCM Mkoa huo, ndugu Mohamed Nyawenga amesema katika kuimarisha Chama Cha Mapinduzi taasisi hiyo nimefanikiwa kuanzisha madarasa ya itikadi kwa vijana ili wajue historia halisi ya Chama na wawe na itikadi ya pamoja katika kulinda Taifa.

Aidha ameeleza kuwa miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa ni pamoja na kutekeleza kwa vitendo Sera ya kujitegemea kiuchumi ambapo kwa sasa wanakusanya mapato kwa wingi kupitia vitega uchumi yanayowawezesha kujilipa wenyewe mishahara na posho kwa viongozi wanaojitolea kwa ngazi za Tawi hadi Mkoa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni