Jumatano, 6 Februari 2019

DK.MABODI: ASHIRIKI UJENZI WA TAIFA KUADHIMISHA MIAKA 42 YA CCM.


NAIBU Kaibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi(kushoto),Mwakilishi wa Jimbo la Tunguu Mhe.Simai Mohamed (kulia) wakishiriki kumwaga zege katika Tawi la CCM Ng’ambwa Mkoa wa Kusini kichama Unguja.

 NAIBU Kaibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akiwa na kofia mkononi kwa ajili ya kuchangisha harambee kwa ajili ya  ujenzi wa skuli ya Uchukuni .
 NAIBU Kaibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akiwa na viongozi mbali mbali wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wakila chakula kilichoandaliwa na Wananchi wa kijiji cha Uchukuni.
 
NAIBU Kaibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akiimba wimbo wa hamasa katika Tawi la CCM Mungoni.



NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi amesema viongozi wa CCM nchini wanasherekea miaka 42 ya kuzaliwa kwa Chama hicho kwa kushuka kwa wananchi,huku wakitekeleza kwa vitendo falsafa ya Tanzania Mpya na CCM Mpya.

Kauli hiyo ameitoa katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani na kufanya shughuli za kijamii ikiwa ni maadhimisho ya kutimiza miaka 42 ya kuzaliwa kwa  CCM ambapo ziara hiyo imefanyika katika Mkoa wa Kusini Kichama Unguja.

Amesema CCM ndani miaka 42 imepambana na mawimbi na mikwamo ya kisiasa mbali mbali na ikafanikiwa kushinda bila kuyumba wala kugawanyika hali inayodhihirisha kuwa taasisi hiyo bado ipo imara pia ni chaguo la wananchi.

Ameeleza kuwa kuimarika kwa misingi ya Demokrasiam,haki za binadamu na utawaka bora wa kisheria pamoja na ustawi wa maendeleo katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii havikupatikana kirahisi bali vimetokana na Sera,miongozo na mipango endelevu ya kiutendaji inayosimamiwa na CCM.

Amesema makada,wanachama na viongozi wa CCM wanajivunia kuwa na taasisi inayojali utu na maendeleo ya wananchi wote bila ubaguzi wa kisiasa,kidini na kikabila.

Amesema CCM imepiga hatua kubwa katika usimamizi wa Ilani yake kwa kuimarisha sekta za Elimu,Afya, Kilimo,Miundombuni ya usafiri wa anga na baharini pamoja na amani na utulivu wa nchi.

Ameeleza kwamba pamoja na mafanikio hayo bado wanachama wa CCM wana jukumu la kulinda urithi wa Mapinduzi ya mwaka 1964,Uhuru, Muungano na taasisi ya CCM ili azna hizo zirithiwe zikiwa katika mikono salama kwa viazi vijavyo.

Dk.Mabodi akiwa katika ukarabati wa Tawi la CCM Ng’ambwa amesema Tawi hilo ni la kihistoria kwani harakati za ukombozi zilifanyika katika eneo hilo hivyo wanachama wa chama hicho wanatakiwa kulinda historia ya Tawi hilo.

Akiwa katika Tawi hilo ameagiza fedha za mfuko wa Jimbo la Tunguu  ambazo ni zaidi ya milioni 90  zitumiwe kumaliza changamoto za wananchi na vilelezo vya matumizi ya fedha hizo viwasilishwe kwa wakati katika Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.

Amesema fedha za jimbo ni mali ya wananchi na kiongozi yeyote atakayekwamisha matumizi ya fedha hizo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa miongozo mbali mbali ya kanuzi ya CCM.

Akiwa katika ziara yake hiyo amesema CCM imejipanga kuhakikisha inaandika historia mpya ya ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa dola mwaka 2020.

Amesema siasa za kuuza maneno na kutoa ahadi zisizotekelezwa zimepitwa na wakati kwani wananchi wanahitaji kuona maendeleo ambayo ndio msingi wa ustawi wa kijamii.

Ameeleza kwamba kuna baadhi ya Vyama vya siasa nchini havina Sera wala dira ya kisiasa bali kazi zake ni kubeza mambo mema yanayotekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hali ya kuwa hata baadhi ya viongozi wa vyama hivyo bado wanalipwa mafao na serikali iliyopo madarakani.

Akizungumza katika ziara hiyo Mwakilishi wa Jimbo la Tunguu Ndugu Simai Mohamed Said ameeleza kwamba toka aingie madarakani amekuwa karibu na wananchi kwa kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili.

Amesema amekuwa mstari wa mbele kuimarisha Sekta za elimu, afya miundombinu ya barabara, vikundi vya ushirika na kusaidia mitaji kwa vikundi vya vijana mbali mbali, huku akitafuta ufumbuzi wa kudumu wa kutatua changamoto ya upungufu wa maji safi na salama kwa baadhi ya maeneo.

Naye Mwakilishi wa tiketi ya CCM Jimbo la Paje Unguja, Mhe.Jaku Hashim Ayoub amesema ametekeleza kwa ufanisi Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020, na bado anaendelea kutatua changamoto mbali mbali zinazojitokea katika jimbo hilo.

Katika ziara hiyo amefuatana na Kamati za Siasa za CCM Wilaya ya Kusini, CCM Wilaya ya Kati , CCM Mkoa wa Kusini, Viongozi wa Halmashauri za Wilaya ya Kati na Kusini Unguja, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ndugu Abdallah Haji Haidari pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Zanzibar Othman Ally Maulid.

Ziara hiyo ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM sambamba na kufanya shughuli za kijamii, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kutimiza miaka 42 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Naibu Katibu Mkuu huyo Dk.Mabodi, ametembelea maeneo mbali mbali yakiwemo kijiji cha Uchukuni katika ujenzi wa skuli ya msingi na maandalizi,Kisiwa cha Uzi kujenga Tawi la CCM Ng’ambwa,kukagua eneo la daraja lililopendekezwa kujengwa na marehemu Mzee Abeid Karume huko Uzi, Tawi la CCM Mungoni pamoja na kuweka jiwe la msingi maskani ya CCM Mawe Mawili huko Mtule Paje.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni