Jumanne, 19 Februari 2019

DK.SHEIN AWAONYA WANANCHI WANAOFANYA MAGENDO.

 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (hawapo pichani)akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Uzi Ng'ambwa mara baada ya kuweka Jiwe la msingi katika shule ya msingi na maadalizi ya Kijiji hicho.
 BAADHI ya Wananchi wa Uzi Ng'ambwa wakisikiliza Hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekitri wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein.



RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein  amewaonya baadhi ya wananchi wanaojihusisha na vitendo vya magendo ambavyo ni kinyume na sheria za nchi bidhaa zao zikikamatwa zitataifishwa na kuwa mali ya Serikali. 

Amesema kwa mujibu wa Sheria mpya ya kuthibiti Magendo Zanzibar inaelekeza Mali iliyosafirishwa kwa njia ya magendo pamoja na Chombo kilichohusika kusafirishia kutaifishwa na kuwa mali ya Serikali.

Dk. Shein tahadhari hiyo ameitoa wakati akiwahutubia Wananchi wa Uzi Ng’ambwa ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua shughuli za Serikali na Chama mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema tabia ya kusafirisha bidhaa kwa njia ya magendo ni mbaya kwani huikosesha Serikali mapato  ambayo hutumika katika kuendeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Amekitaka  Kikosi cha kuzuia magendo Zanzibar KMKM kufanya kazi zake kikamilifu ili kuhakikisha biashara hiyo inakoma katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

“Ndugu zangu nakuombeni sana jiepusheni sana na Magendo, Kikosi chetu cha KMKM tumekiwezesha kwa vifaa, hivyo anayejaribu kufanya magendo atakamatwa tu na kufilisiwa” alitanabahisha  

Akizungumzia kuhusu huduma ya maji safi na salama katika Kisiwa hicho Dk Shein amesema Serikali imejipanga vyema kuhakikisha huduma hiyo inapatikana muda wote.

Amesema kwa sasa Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati inaendelea na mipangilio yake kuhakikisha kunajengwa Tangi la Maji ambalo litatumika kusambaza huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa Uzi.

Kuhusu huduma ya usafiri wa kufikia kisiwani hapo Dk Shein amesema Serikali ina mpango wa kujenga Daraja litakalowezesha Wananchi kufika katika kisiwa hicho kwa wepesi.

Daraja hilo litaanzia katika Kijiji cha Ungujaukuu Kaipwani hadi Uzi na kujengwa juu ya usawa wa bahari ili kusaidia wananchi kufika kisiwani huko muda wote.

Katika kutekeleza azima hiyo Serikali itaomba Mkopo katika Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB kwa ajili ya kuendeleza maendeleo ya Kisiwa cha Uzi.

“Nakuombeni vuteni subra, Serikali ipo kwa ajili ya kukuleteeni maendeleo tumeshajenga miradi mingi ya gharama, hivyo Daraja haliwezi kutushinda tutalijenga panapo majaaliwa” alibainisha Dk. Shein.

Akizungumzia Sekta ya Elimu Dk.Shein, amewambia wananchi hao kuwa elimu ni bure hakuna mwananchi yeyote atakayelipishwa gharama za elimu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kati Mashavu Said Sukwa ameelezea mafanikio ya Wilaya yake ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo mbali mbali vya Wilaya hiyo.

Aidha ameishukuru Serikali kwa hatua yake ya kufanya ugatuzi jambo ambalo limesaidia kuzikabili changamoto za Wilaya.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Juma Abdallah Sadala ameipongeza Wilaya hiyo kwa mashirikiano mazuri katika ya Viongozi wa Serikali na Chama hali inayopelekea kasi ya maendeleo Wilayani humo.

Amewapongeza Wananchi na Wanachama wa Wilaya ya Kati kwa kubuni miradi ya maendeleo ambayo husimamiwa vyema na Serikali.

 Hivyo amewaomba Wanachama kuendelea kushirikiana vyema na viongozi wao ili kutekeleza vyema Ilani ya CCM ya mwaka 2015-20.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni