Jumanne, 12 Februari 2019

DK.SHEIN AZINDUA MIRADI MIKUBWA YA MAJI SAFI NA SALAMA, CCM YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA ILANI.



 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiweka Jiwe la Msingi katika Tangi la Maji Safi na Salama la ujazo wa Lita Milioni Mbili linalojengwa Saateni mjini Zanzibar katika ziara yake iliyoanza leo Tarehe 12/02/2019. 
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema inatekeleza kwa haraka miradi ya Maji Safi na Salama katika Mkoa wa Mjini Magharibi ili kumaliza changamoto ya upungufu wa huduma hiyo.

Amesema  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kutafuta njia mbadala za kuhakikisha wananchi wanapata kwa wakati huduma za maji safi na salama katika maeneo wanayoishi.

Mikakati hiyo ameitoa leo huko Saateni katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi Tangi la Maji Saateni ambapo mapema aliweka jiwe la msingi Tangi la Maji Mnara wa Mbao, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya kutembelea Mikoa yote ya Zanzibar atakayoihimisha Februari 25 mwaka huu.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein amesema kila awamu ya uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilijitahidi katika kutatua tatizo la maji na kila kiongozi alifanya wajibu wake juu ya kuwapatia wananchi huduma hiyo na hakuna aliyedharau.

Amefafanua kuwa uongozi wa Serikali ya awamu ya Saba umetoa kipaumbele katika kuimarisha miundombibu ya upatikanaji wa maji safi na salama nchini .

Aliongeza kuwa jitihada za kukamilisha dhamira hiyo kuanza na suala la utafutaji wa fedha na vifaa mbali mbali vya maji ili kufikia azma hiyo.

Alieleza kuwa mradi huo wa maji ukikamila hali ya maji itakuwa imeimarika zaidi ikizingatiwa ni moja ya hatua kubwa za Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Ameeleza kuwa  juhudi za makusudi kwa kushirikiana na washirika wa Maendeleo ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB ambapo iliikopesha Zanzibar Dola milioni 21, Serikali ya Ras al khaimah imechimba visima 23, India imetoa kwa mkopo wa Dola milioni 92 pamoja na msaada kutoka Serikali ya Japan wa Dola milioni 100 kwa ajili ya kuimarisha huduma hiyo ya maji.

Kupitia hotuba yake Dk.Shein amesisitiza umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira kwani miongoni mwa sababu za uhaba wa maji katika Mkoa wa Mjini kunatokana na uharibifu wa mazingira uliofanywa katika vianzio vya maji zikiwemo chemchem.

Kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Salama Aboud Talib amesema juhudi zinazochukuliwa katika kuhakikisha mradi huo unakamilika huku akitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kusimamia utekelezaji wa miradi muhimu yenye tija kwa wananchi.

Awali Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo, Tahir Khamis Abdallah amesema Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Mkoa wa Mjini Magharibi (ZUWSP) unatekelezwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na utekelezaji wake ulianza mwaka 2013 na unatarajiwa kumalizika mwezi wa Disemba 2019.

Aliongeza kwa kufafanua kuwa uchimbaji wa visima vipya 6, ukarabati wa visima vikongwe 23, ujenzi wa Matangi 2 yenye ujazo wa lita Milioni mbili 2,000,000 Saateni na Milioni Moja 1,000,000 Mnara wa Mbao, ulazaji wa mabomba makubwa yenye urefu wa kilomita 20 kutoka Bumbwisudi hadi Welezo matangini pamoja na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 60 kutoam Welezo hadi kwa watumiaji.

Naibu huyo Katibu Mkuu alieleza kuwa katika mradi huo hadi kukamilika kwake kugharimu jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 23 sawa na TZS Bilioni 37.1 ambapo SMZ imetoa TZS Bilioni 3.8 na TZS Bilioni 33 zitatolewa kwa Mkopo kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).

Akizungumza Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao ameeleza kuwa Chama Cha Mapinduzi kinaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa Ilani ya CCM inayosimamiwa vizuri na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein.

Alisema mbali na miradi ya maji pia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa kinara wa kutatua kero sugu zilizokuwa zinawakabili wananchi kwa muda mrefu katika nyaza za huduma muhimu za kijamii katika Afya, Elimu, Miundombinu, ajira,ulinzi na usalama wa nchi sambamba na kulinda Amani na Utulivu wan chi.

Wakizungumza kwa wakati tofauti baadhi ya wananchi walioudhuria katika hafla hiyo wameeleza kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na kuimarika kwa miundombinu ya barabara inayowawezesha wananchi wa makundi yote hasa wa vijijini kusafiri kwa urahisi kutoka sehemu moja kwenda nyingine.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni