RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizindua Kituo cha Kuanikia Dagaa cha Bububu Kihinani. |
MKUU wa Mkoa Mjini Magharibi Mhe.Ayoub Mohamed Mahmoud akitoa ufafanuzi namna Serikali inavyowasaidia wananchi wanaojiajiri wenyewe katika eneo hilo. |
Dagaa linalokaushwa na kuuzwa na wajasiriamali katika eneo la Bububu Kihinani. |
MKURUGENZI wa Baraza la Manispaa Magharibi 'A' ndugu Amour Ali Mussa akisoma taarifa ya maendeleo ya eneo hilo la kukausha Dagaa. |
BAADHI ya Wananchi waliojiajiri katika eneo hilo uko Bububu Kihinani wakisikiliza hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliyefika katika eneo hilo. |
WANANCHI
waliojiajiri katika ujasiriamali wa kukausha na kuuza dagaa katika eneo la
Bububu Kihinani, wametakiwa kufanya kazi zako kwa kufuata taratibu za Kisheria.
Wito
huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali
Mohamed Shein mara baada ya kuzindua kituo cha kukaushia Dagaa, huko Bububu Kihinani Unguja.
Amewasihi
wananchi hao kuwa Serikali inawajali na kuwathamini hivyo waendelee kufuata
sheria za nchi ili waweze kunufaika na fursa mbali mbali kutoka Serikalini.
Amewataka wajasiriamali
hao kuendelea na shughuli zao na kuuza bidhaa zilizo bora ndani na nje ya nchi
bila ya woga.
Ameeleza kuwa Zanzibar imebarikiwa kuwa na bahari yenye
rasilimali kadhaa, hivyo ni vyema ikatumika katika kuwakomboa wananachi kuoka
katika lindi la umasikini.
Amewataka kuuza dagaa bora litakalokubalika katika soko
la Dunia na sio Afrika mashariki na nchi jirani pekee.
Ameiagiza Wizara ya kilimo, Mifugo na Uvuvi, kubuni njia
bora zaidi ili kuwawezesha wajasiriamali na wafanyabiashara wa dagaa waweze
kutumia mbinu bora za ukaushaji.
Aidha, Dk. Shein amewasihi wajasiriamali hao kuwa makini
katika matumizi ya mashine hiyo wakati wa ukaushaji ili kuepuka athari
zinazoweza kujitokeza na kuharibu ubora wa bidhaa zao.
Amesema serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha sekta
ya uvuvi kwa kununua meli mbili mpya, sambamba na kuliimarisha shirika la ZAFICO , azma inayokwenda sambamba
na ujenzi wa viwanda vya Mwani, kwa mashirkiano na washirika wa maendeleo.
Dk Shein, amewapongeza wananchi hao kwa utulivu na
usikivu wao wa kukubali kuhama katika eneo la Maruhubi walipokuwa wakiendesha
shughuli hizo na kuhamia Kihinani.
Mapema, Waziri wa Nchi (OR) Tawala na Mikoa, Serikali za
Mitaa na Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir amesema Serikali inatatua hatua kwa hatua
changamoto mbali mbali zinazowakabili wajasiriamali hao.
Amesema Serikali
haina lengo la kuwaonea wananchi wake, akibainisha kuwa utekelezaji huo
unakwenda sambamba na Ilani ya CCM katika kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Ameeleza kuwa serikali imelenga kuliendeleza eneo hilo
kwa kufanikisha utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa Bandari ya kisasa,
hatua itakayochangia ustawi mkubwa uchumi wa Taifa.
Nae, Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Magharibi 'A' Amour
Ali Mussa amesema Baraza hilo limetumia zaidi ya Shilingi Milioni 17.1 kwa
ajili ya kulipa fidia wananchi waliokuwa
wakilitumia eneo hilo la Kihinani.
Ametaja changamoto ya ufinyu wa nafasi kwa ajili ya
wafanyabiashara, ambapo eneo la eka 1.3 limeazimwa kutoka Chuo cha Mwalimu
Nyerere na hivi sasa linahitajika kwa matumizi ya chuo hicho.
Amesema jumla ya wananchi 1,396 wananufaika kwa kuendesha
shughuli za ujasiriamali katika sehemu hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni