Jumatatu, 4 Februari 2019

NDG.MOHAMED RAJAB: ASEMA 2020 CCM ITAUFUTA UPINZANI ZANZIBAR.

MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Magharib Ndugu Mohamed Rajab (wa kwanza kulia) akizungumza kwa niaba ya kamati ya Siasa baada ya kumtembelea kiongozi mstaafu wa UWT wa Mkoa huo hapo Nyumbani kwake Kiembesamaki, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Magharibi Bi.Zainab Ali Maulid(wa pili kulia), Mwenyekiti Mstaafu wa UWT Mkoa wa Magharib Bi.Salma Salami Mselem(wa tatu kulia) pamoja na Katibu  wa Siasa na Uenezi CCM Mkoa wa Magharib Bi.Msekwa Mohamed Ali wakiwa katika ziara ya kuwatembelea Wazee wa CCM na Serikali ndani ya Mkoa huo.  
 WAZIRI mstaafu Wizara ya Ardhi, Maji,Nishati,Makaazi na Mazingira Ndugu Kamal Basha Pandu (kulia) akizungumza mara baada ya kutembelewa na Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Magharib kichama.
 BAADHI ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Magharib wakiwemo Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kupitia Mkoa huo walioshiriki katika ziara hiyo.



NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Magharibi Zanzibar, ndugu Mohamed Rajab Soud amesema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 42 ya CCM yametokana na juhudi na maarifa ya Wazee na Waasisi wa Chama hicho.

Kauli hiyo ameitoa katika ziara ya kuwatembelea wazee na waasisi mbali mbali waliohudumu katika CCM, Jumuiya na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa miaka mingi.

Ndugu Mohamed amesema CCM inatimiza miaka 42 ikiwa na azna na rasilimali watu ambao ni wazee wenye uwezo na maarifa mbali mbali ya kiungozi, kitaaluma na kiitikadi wanaoshauri masuala muhimu ya kuiletea maendeleo taasisi hiyo na jumuiya  zake.

Ameeleza kwamba Chama hicho bado kinathamini,kutambua na kuunga mkono juhudi za wazee waliofanya kazi kubwa ya kuviunganisha TANU na ASP hatimaye ikazaliwa CCM ambayo hivi sasa ni taasisi pekee ya kisiasa inayoongoza dola kwa ufanisi mkubwa.

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo amebainisha kwamba Mkoa wa Magharibi kichama unaadhimisha miaka 42 ya kuzaliwa kwa CCM kwa kuwatembelea wazee mbali mbali wa CCM, kufanya usafiri katika maeneo ya kijamii pamoja na kufanya kazi za kijamii.

Amesema CCM inajipanga vizuri kuhakikisha mwaka 2020 inashinda kwa kishindo na kuufuta upinzani katika Mkoa wa Magharib na maeneo mbali mbali nchini humo,kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani yake ya mwaka 2015/2020.

Naye Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Magharibi, Bi.Zainab Ali Maulid amesema umoja huo unaimarika kutokana na juhudi za viongozi wachapakazi waliowarithisha uzalendo,weledi,maarifa na mbinu mbadala viongozi wa sasa,ambao wanaendelea kuimarisha taasisi hiyo.

Amesema UWT inajivuania kuwa na waasisi imara walioacha alama za mafanikio katika enzi za uongozi wao ambazo mpaka sasa zimebaki kuwa ni ishara ya maendeleo endelevu kisiasa na kiitikadi.

Akizungumza mara baada ya kutembelewa na Kamati ya Siasa ya Mkoa huo Katibu Mstaafu wa UWT Mkoa wa Magharib, Bi.Salma Salami Mselem ameupongeza uongozi huo kwa maamuzi yao ya kumtembelea.

Bi.Salma amewasihi viongozi hao wa Chama Cha Mapinudizi waendelee kushikamana na kubuni njia mbadala za kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi ili kiendelee kuongoza dola.

Kwa upande wake Waziri mstaafuwa Maji, Nishati, Makaazi na Mazingira Zanzibar , Ndugu Kamal Basha Pandu ameeleza kuwa licha ya kuwa amestaafu nafasi za uongozi mbali mbali ndani ya Chama na Serikali bado anaendelea kuwamini kuwa CCM ni taasisi yenye sera nzuri zinazotatua kero za wananchi.

Ndugu Kamal, ambaye pia ni Naibu Spika Mstaafu wa Zanzibar ametoa nasaha kwa viongozi na watendaji wa CCM wafanye kazi kwa bidii ili wananchi waendelee kuamini sera, miongozo na siasa zinazotekelezwa na Chama hicho.

Ziara hiyo ni miongoni mwa shamrashara za kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi  kinachotimiza miaka 42 toka kuasisiwa kwake mara baara ya Vyama vya Ukombozi kwa ASP na TANU kuungana na hatimaye kuzaliwa kwa CCM Februari 5, mwaka 1977.







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni