RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akiweka Jiwe la Msingi Kituo cha Afya cha Magirisi Unguja. |
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein ameeleza kuridhishwa na
utekelezaji wa shughuli mbalimbali za chama na serikali zilizotekelezwa katika
Wilaya ya Magharibi ‘B’.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo katika
Majumuisho ya ziara yake ya Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi
yaliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya
Zanzibar Beach Resort Mazizini, mjini Zanzibar ambapo viongozi mbali mbali
walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Mama Mwanamwema Shein na viongozi
wengine.
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein
alipongeza juhudi zilizochukuliwa na uongozi wa Wilaya hiyo katika kuendeleza
na kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na mashirikiano
mazuri yaliopo kati ya uongozi wa Wilaya na uongozi wa Chama.
Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo
kueleza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inazozichukua katika
kuhakikisha inawapelekea huduma bora wananchi wake wote bila ya kujali rangi,
dini, kabila wala itikadi ya kisiasa.
Amepongeza kwa taarifa nzuri ya Wilaya
iliyotolewa katika majumuisho hayo ambayo imeonesha wazi kuwa kazi kubwa
imefanywa tena kwa mafanikio mazuri.
Dk. Shein ameeleza furaha yake
iliyompelekea kuridhika na ziara hiyo kwa kuona miradi muhimu ya maendeleo
ambayo ameiwekea mawe ya msingi kikiwemo kituo cha afya Magirisi pamoja na
Skuli ya Msingi ya Kwarara katika Wilaya hiyo.
Aidha,
Dk. Shein ametaka vituo vya afya vinavyohudumia watu ni
vyema vikaandaliwa vizuri katika kutoa huduma na kuitaka Wizara ya Afya
kujipanga vyema kabla ya kuanza kutoa huduma katika kituo hicho pale
kitakapokuwa tayari.
Amesema kuwepo kwa amani na utulivu
hapa Zanzibar kumeweza kuwavutia wageni kutoka nchi mbali mbali duniani kuja
kuitembelea Zanzibar na kusisitiza haja ya kulindwa na kuenziwa ili Zanzibar
izidi kupata mafanikio ikiwemo kuongezeka kwa watalii.
Amesema Zanzibar iweze kufika
katika uchumi wa Kati nguvu kubwa zinahitajika katika kuimarisha sekta ya elimu
na kusisitiza kuwa iwapo Zanzibar ikitaka kuimarisha sekta ya elimu ni lazima
elimu ya msingi iimarishwe.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuupongeza
uongozi wa Wilaya, uongozi wa Wizara ya Elimu kwa mashirikiano makubwa yaliopo
ambayo yamepelekea kujengwa kwa Skuli mpya ya Msingi ya Kwarara.
Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala
za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir alieleza kuwa
mbali ya Wakuu wa Wilaya kusubiri ziara za viongozi pia, wanajukumu la
kuzishughulikia changamoto za wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘B‘ Kapteni
Silima Haji Haji akitoa taarifa ya Wilaya hiyo amesema katika kufanikisha
zoezi la ukusanyaji wa mapato Baraza la Manispaa lilipanga mikakati mbali mbali
na njia za utekelezaji wake ili liweze kufikia malengo ya ukusanyaji mapato ya
TZS Bilioni 2 kwa mwaka 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia 35 ya makisio ya
mwaka 2017/2018 ambayo yalikuwa TZS bilioni 1.3.
Aliongeza kuwa njia za ukusanyaji wa
mapato zimeimarishwa ikiwemo kuanzisha mfumo wa kukusanyia mapato wa
kielektroniki ambapo jumla ya ‘Point of Sale’ (POS) 19 zimenunuliwa.
Kwa upande wa sekta ya elimu amesema kuwa
mafanikio makubwa yanaendelea kupatikana yakiwemo ya uandikishaji wa wanafunzi
wapya ambapo kwa upande wa elimu ya awali uandikishaji umepanda kutoka
wanafunzi 3,009 mwaka 2018 hadi wanafunzi 3,225 mwaka 2019 huku akieleza
mikakati iliyowekwa ya elimu ya Sekondarinkatika Wilaya hiyo.
Aidha, ameeleza juhudi zinazochukuliwa
katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji
wa wanawake na watoto zinavyoendelea ambapo muitiko wa kuripoti matukio
hayo unaonekana kuongezeka ingawa changamoto iliyokuwepo ni pamoja na baadhi ya
wananchi kukataa kutoa ushahidi pindi wanapohitajika kufanya hivyo.
Amesema Serikali kupitia Mamlaka ya
Maji imeweza kwa kiwango kikubwa kuimarisha miundombinu ya maji ndani ya Wilaya
hiyo hivi sasa Shehia zimeunganishwa na zinapata maji safi na salama kutokana
katika visima 22 vya Serikali kutegemea utaratibu uliopangwa.
Katika juhudi za kuwapatia huduma ya maji
safi na salama katika Wilaya hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya amesema Serikali
kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo inatarajia kuanza kwa mradi wa maji
utakaogharimu Dola za Marekani Milioni 92.8 ambao utapunguza tatizo la maji
safi na salama kwa wananchi wa Wilaya hiyo.
Ameongeza kuwa Mradi huo utahusisha
uchimbaji wa visima, ujenzi wa matenki na ulazaji wa mabomba katika maeneo
mbali mbali likiwemo eneo la Kwarara Kidutani.
Akitoa neno la shukurani Mkuu wa Mkoa wa
Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa mashirikiano
na kueleza kuwa watayafanyia kazi yale waliyoelekezwa na Rais Dk. Shein katika
majumuisho hayo.
Amesema kuwa Rais Dk. Shein ametoa elimu
klubwa katika ziara yake kwenye Wilaya zote tatu na kueleza kufarajika kwa
namna Dk. Shein kumaliza ziara yake katika Mkoa huo akiwa na furaha tele
kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na kuahidi kuwa changamoto zilizoelezwa
jitihada zitafanyika ili kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi.
Rais Dk. Shein anatarajia kuendelea na
ziara yake katika Mkoa wa Kaskazini itakayoanzia
katika Wilaya ya Kaskazini A Unguja siku ya Jumaapili ya tarehe 17 Februari
mwaka huu 2019.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni