RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein. |
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa migogoro ya ardhi iliyopo katika Wilaya ya
Magharibi A, inachingiwa na baadhi ya viongozi wa Wilaya hiyo ambao
wanajihushisha na migogoro hiyo.
Dk. Shein aliyasema
hayo katika Majumuisho ya ziara yake ya Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa
Mjini Magharibi katika ukumbi wa Kituo cha Utengamano Welezo mjini Zanzibar
ambapo Mama Mwanamwema Shein na viongozi wengine wa chama na Serikali walihudhuria.
Katika hotuba yake ya
Majumusho, Rais Dk. Shein ameutaka uongozi wa Wilaya hiyo kutojihusisha na
migogoro hiyo na badala yake wawasaidie wananchi kuondokana na migogoro hiyo ya
ardhi.
Ameongeza kuwa tayari
Zanzbar kuna Sheria sita za Ardhi hivyo hakuna sababu za kuwepo migogoro hiyo
ambayo haileti tija wala manufaa.
Dk. Shein ameeleza kuwa hali hiyo imekuwa ikichangia migogoro na kusema kuwa yeye anapochagua
viongozi hachagui kwa lengo la kusemwa vibaya Serikali na badala yake huchagua kwa
lengo la kuwasaidia wananchi ambapo wapo baadhi viongozi wanafanya kinyume na
lengo hilo.
Aidha, amesema kuwa
katika ziara yake hiyo ya Wilaya ya Magharibi A, kuna mambo amaeyaona ambayo
yapo kinyume na utaratibu hivyo,
aliitaka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ pamoja
na uongozi wa Mkoa na Wilaya hiyo kuyatafutia ufumbuzi.
Rais Dk. Shein
amesema kuwa katika ziara yake hiyo akiwa eneo la Chuini alikuta gari za mawe,
wauza miti pamoja na soko ambavyo vyote hivyo vipo kinyume na utaratibu huku
viongozi wa Wilaya wakiiona hali hiyo na kuifumbia macho hivyo, aliwataka kuifuatilia
hali na kuitafuta ufumbuzi wa haraka.
Dk. Shen amesikitishwa kuona agizo alilolitoa siku za nyuma la kuondoshwa kwa gari za mawe katika eneo
la Mwanakwerekwe likiwa bado halijafanyiwa kazi na bado gari hizo zimeendelea
kuwekwa katika eneo hilo na kuleta usumbufu kwa wapita njia.
Ameelezea kuwepo kwa
gari za Mawe katika eneo la Welezo pamoja na kujaa kwa wauza miti katika eneo
hilo pamoja na lile la Mwera kwenye kituo cha mafuta kuwa kituo cha gari za
mawe si jambo la busara na viongozi wanatakiwa kuchukua hatua stahiki.
Dk. Shein alishangazwa
kuwa hivi sasa katika eneo hilo gari za mchanga zinaengeshwa barabarani kinyume
na utaratibu pamoja na kueleza hatua za uchimbaji wa rasilimali hiyo
zilivyofanywa hali ambayo imechangia mchanga Zanzibar kuadimika.
Alieleza kuwa wapo
baadhi ya watu wameuficha mchanga likiwemo eneo la Chechele hali ambayo
imezidisha kuwepo uhaba wa mchanga hali inayopelekea hadi baadhi ya ujenzi wa
miradi ya Serikali kusuasua ukiwemo ujenzi wa jengo la Mamlaka ya Uthibiti wa
Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) kutokana na uhaba wa rasilimali hiyo
hapa nchini hivi sasa.
Amesema kuwa mchanga
na mawe ni mali ya serikali akiwa na maana kwamba ni mali ya watu wote hivyo,
alishangazwa na wale waliozihodhi mali hizo katika maeneo yao huku wakiwaacha
wananchi wakipata tabu kusaka rasilimali hiyo.
Hivyo, aliutaka
uongozi huo wa Wilaya kuwasimamia wenye gari za mawe na mchanga kwa lengo la
kuyaondosha katika maeneo ambayo hayajaruhusiwi
na kuutaka uongozi wa Wilaya hiyo
kuongeza mapato kutokana na kuwepo kwa vianzio vingi vya mapato.
Rais Dk. Shein
alieleza haja kwa uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Makaazi pamoja
na uongozi wa Mkoa na Wilaya hiyo kushirikiana katika kuangalia miundombinu ya
maji ili maji machache yaliopo wananchi waweze kuyapata na kuyatumia ipasavyo.
Katika maelezo yake
Rais Dk. Shein alisisitiza haja kwa uongozi wa Wilaya hiyo kuongeza kasi katika kusimamia masuala mazima
ya udhalilishaji huku akipongeza hatua zilizochukuliwa na Wilaya hiyo katika
kupambana na janga hilo hatari.
Ameeleza furaha yake
kutokana na makusanyo ya fedha na kuwapongeza kwa kukusanya mapato ya wastani
Bilioni 1.5 ambalo ni ongezeko la asilimia 14 ya makadiria yao nan kuvuka lengo
walilojiwekea pamoja na kufanya vizuri katika masuala ya kesi za udhalilishaji,
ajira kwa vijana kwa kukusanya nguvu ili waweze kujiajiri.
Aliwapongeza kwa
kufanya vizuri katika masuala ya ulinzi na usalama kwa kupambana na wezi,
vitendo vya wizi wa kutumia nguvu ambapo wengine hutumia silaha katika
kutekeleza hujuma hizo.
Pia, alitoa pongezi
zake kwa kukusanya nguvu kwa vikundi vya vijana katika Wilaya hiyo kwa azma ya
kutaka kujiajiri wenyewe pamoja na mafanikio mengine.
Kwa upande wa
changamoto ya uhaba wa maji, Rais Dk. Shein alieleza hatua zinazochukuliwa na
Serikali katika kupunguza changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kuutumia mkopo wa
Dola za Marekani 92 kutoka Exim Benki ya India ambapo tayari maandalizi ya
kukusanya tenda yameshaanza.
Aidha, katika kutatua
changamoto ya maji, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Shehia 26 zikiwemo za Mji
Mkongwe na maeneo mengine ya Mji wa Zanzbar zitafaidika na Mradi wa maji wa
ujenzi wa matangi ya maji ya Saateni na Mnara wa Mbao mradi utakaogharimu TZS
Bilioni 37.1 ambao unatarajiwa kumalizika mwezi Disemba mwaka huu 2019 ambao
tayari umeshafikia asilimia 55 ya utekelezaji.
Nae Waziri wa Nchi
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir alieleza
hatua zinazochukuliwa na Ofisi hiyo
katika kutatua changamoto kadhaa zilipo ambazo zilikuwa ni vikwazo kwa
wananchi.
Akisoma taarifa ya
utekelezaji wa Wilaya ya Magharibi A,
Mkuu wa Wilaya hiyo Kepteni Khatib
Khamis Mwadini amesema kuwa Wilaya hiyo inatekeleza Mkakati wa Kukuza Uchumi na
Kupunguza Umasikini (MKUZA III), Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020, Malengo
ya Maendeleo Endelevu (SDG) na Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020.
Ameeleza miongoni wa
changamoto alisema ni pamoja na uhaba ajira ambapo alieleza hatua
walizozichukua katika kuhakikisha ikiwa ni pamoja na kuunda vikundi ambavyo
vimepewa taaluma.
Amesema kuwa Wilaya
hiyo inakabiliwaa na wimbi 114 ziliripotiwa zikiwemo kesi za wazazi
kutowahudumia watoto wao, ubakaji na nyenginezo ambapo imejipangia mkakati wa
kutoa mafunzo ya kujilinda na udhalilishaji zikiwemo kuunda Kamati pamoja na kuitumia
sanaa na mikutano kadhaa kati yao na wananchi.
Mkuu wa Wilaya hiyo alieleza
kuwa huduma ya maji safi na salama bado haiko vyema na inapelekea wananchi wa
maeneo hayo kuhangaika katikam kutafuta huduma hiyo ya maji hali ambayo
inapelekea kudhorotesha utendaji wao wa kazi.
Alieleza kuwa migogoro
ya ardhi imekuwa ikijitokeza katika Wilaya hiyo na kueleza mikakati iliyowekwa
ikiwa ni pamoja na kuwafuatilia watu wanaojenga bila ya kuwa na Vibali vya
ujenzi.
Nae Mwenyekiti wa
Wilaya ya Mfenesini akisoma ripoti ya Wilaya hyo kwa ufupi amepongeza kwa
niaba ya viongozi na wanaCCM wa Wilaya hiyo huku akiahidi kuwa ushindi katika
Majimbo yote sita ya Wilaya hiyo ni lazima kwa CCM.
Akitoa neno la
shukurani, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mahmoud amesifu hekima na
busara za Dk. Shein katika uongozi wake hatua ambayo inasaidia katika kuleta
maendeleo endelevu.
RC Ayoub amemuahidi Rais kuwa
yale yote aliyowaelekeza watayafanyia kazi hasa migogoro ya ardhi, maegesho ya
gari za mawe na mchanga katika maeneo yasiyoruhusika pamoja na kuongeza bidii
na mkazo katika suala la udhalilishaji na ukusanyaji wa mapato pamoja na
mengineyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni