Jumatatu, 25 Februari 2019

DK.SHEIN ATOA AGIZO KWA WIZARA YA AFYA, AZINDUA BARABARA YA KUYUNI -NGOMENI (3.2KM) NA KITUO CHA AFYA NGOMENI PEMBA.


RAIS wa Zanzibar Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiweka Jiwe la Msingi na kukizindua  Kituo cha Afya cha Ngomeni katika Wilaya ya Chake Chake Pemba.

BAADHI ya Wananchi wakiwa katika uzinduzi wa kituo cha Afya Ngomeni huko Wilaya ya Chake Chake Pemba.

BAADHI ya Viongozi mbali mbali wa Serikali na CCM wakiwa katika hafla hiyo ya uzinduzi wa Barabara na KItuo cha Afya cha Ngomeni Wilaya ya Chake Chake Pemba.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Ngomeni mara baada ya kuzindua Barabara na Kkituo cha Afya katika Kijiji hicho.

WAZIRI wa Nchi(OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Haji Omar Kheir akizungumza katika hafla hiyo juu ya dhana ya Ugatuzi ambapo Serikali Kuu imeshusha baadhi ya madara kwa Serikali za Mitaa ili wananchi waamue wenyewe vipaumbele vyao katika masuala ya Huduma za Kijamii.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi(kushoto) akifuatilia matukio mbali mbali katika hafla hiyo ya uzinduzi wa kituo cha afya.

Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Usafirishaji Dk Sira Ubwa Mamboya akitoa maelezo juu ya mikakati ya SMZ itakavyoendelea  kujenga barabara za Kisasa katika maeneo mbali mbali ya Pemba.

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti  wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein ameiagiza Wizara ya Afya Zanzibar kutoa huduma bora za Afya sambamba na kuwashauri wananchi juu ya masuala mbali mbali ya Afya huko katika Kituo cha Afya kilichopo  Kijiji cha Ngomeni, Wilaya ya Chake Chake Pemba.


Dk.Shein ametoa agizo hilo mara baada ya kuweka jiwe la msingi na kukizindua rasmi Kituo cha Afya katika Kijiji hicho, amesema kuwa kituo hicho lazima kitoe huduma bora na kuwaondoshea wananchi changamoto za ukosefu wa huduma bora za afya ambazo awali wananchi wa Kijiji hicho walizifuata maeneo ya mbali.


Amesema lazima Wizara husika ihakikishe inapeleka Watendaji na Vifaa tiba vya kutosha ili kumaliza changamoto za ukosefu wa huduma hizo muhimu za Afya kwa wananchi hao.


Amesema kuwa baada ya miezi miwili ataenda kukagua Kituo hicho kwa lengo la kujiridhisha juu ya maagizo yake yamefanyiwa kazi kwa kiasi gani.


Ameeleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitomvumilia Watendaji na Viongozi wanaokwamisha maendeleo ya nchi kwa makusudi kwani serikali inatumia gharama kubwa kuwasogezea wananchi huduma za msingi lakini wapo baadhi ya watendaji wanaokwamisha juhudi hizo kwa makusudi.


Katika maelezo yake Dk. Shein, ameeleza kuwa uamuzi wa Serikali kujenga  Barabara ya Kuyuni hadi Ngomeni pamoja na Ujenzi wa Kituo cha Afya   Ngomeni,  umekuja kufuatia eneo hilo kuzalisha kiwango kikubwa cha zao la karafuu.


Dk. Shein amesema ufunguzi wa  barabara ya Kuyuni hadi Ngomeni yenye urefu wa kilomoita 3.2, iliojengwa kwa kiwango cha Lami  pamoja na kituo cha Afya , ujenzi uliofanikishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni miongoni mwa fursa za maendeleo katika Kijiji hicho na vijiji jirani.


Amesema juhudi za ujenzi wa barabara na kituo hicho cha Afya, utaendana na ujenzi wa barabara ya Mgelema hadi Wambaa, kazi itakayotekelezwa kabla ya mwisho wa mwaka huu.


Amewaeleza wananchi hao, kuwa maendeleeo makubwa yaliopatikana katika eneo hilo yanatokana na uzalishaji mkubwa wa karafuu, hivyo akawapongeza wananchi wa maeneo hayo kwa kuuza karafuu zao ZSTC.
Dk. Shein amewataka  wananchi kukaa pamoja na Wawakilishi wao ili waweze kusaidia upatikanaji wa gari la wagonjwa (ambulance) ili kusaidia usafirishaji wa wagonjwa wanaohitaji huduma za ziada  katia Hospitali kuu.


Katika hatua nyengine, Dk. Shein amemuagiza  Katibu Mkuu Wizara Afya kujipanga na watendaji wake na kuainisha gharama za ujenzi wa kituo cha Afya Ngomeni, baada ya kushindwa kubainisha katika taarifa yake.


Dk.Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amesema mafanikio yanayopatikana katika Nyanja mbali mbali Visiwani Pemba yatatokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.


Amesema kabla ya kupelekwa huduma za msingi katika Kijiji cha Ngomeni wananchi wa maeneo hayo waliishi kwa changamoto mbali mbali kutokana na kukosa Barabara, Umeme, Maji Safi na Salama, Kituo cha Afya mambo ambayo kwa sasa tayari yametekelezwa kwa ufanisi mkubwa.


Katika hatua nyingine Dk.Shein mara baada ya uzinduzi huo amepokea Taarifa za Serikali na Chama Cha Mapinduzi kupitia Majumuisho ya ziara yake katika Wilaya hiyo yaliyofanyika katika ukumbi wa ZSTC Makonyo Pemba, ikiwa ni hitimisho la ziara hiyo kwa Unguja na Pemba.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni