RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiwa na Mawaziri mbali mbali wa SMZ akikagua eneo linalochimbwa Mchanga la Donge Chechele. |
Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ziara yake ya Wilaya ya Kaskazini B Unguja wakati alipotembelea maeneo yanayochimbwa mchanga huko Pangatupu, Chechele na Kiombamvua na kujionea jinsi maeneo hayo yalivyoathirika kutokana na rasilimali hiyo kuanza kumalizika kabisa.
Katika ziara hiyo ambapo Makamo
wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd na Mama Mwanamwema Shein walishiriki
kikamilifu, Rais Dk. Shein aliwataka wananchi wajue uhaba uliopo wa rasilimali
hiyo ya mchanga.
Akiwa katika eneo la Pangatupu na
Chechele, Rais Dk. Shein alieleza kuwa rasilimali ya mchanga hapa Zanzibar
imeanza kutoweka na haipo hivyo kuna haja ya kuweka mikakati maalum ya kunusuru
huo mchache uliobakia ambapo tayari Serikali anayoiongoza imeshaanza kazi hiyo.
Alieleza kuwa tayari ameshawapa
kazi Mawaziri wake watatu pamoja na Kamati yao ya Makatibu Wakuu kufuatilia hali
hiyo kwani tayari kwa upande wake hivi karibuni aliagiza shughuli za uchimbaji
wa mchanga kusisitiswa.
Aliongeza kuwa Serikali imefanya
hivyo si kama inawakomoa wananchi wake bali inatafuta utaratibu wa kufanya ili
rasilimali hiyo iwasaidie wananchi wote kwani tayari kuna wafanyabiashara
wameshahodhi mchanga katika maeneo yao ya biashara hasa wale wanaofanya
biashara ya matofali.
Rais Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kuwataka waandishi wa habari waliokuwepo katika eneo hilo na wale
waliokuwa hawapo katika ziara yake hiyo kuwaeleza wananchi ukweli juu ya uhaba
wa rasilimali hiyo ambayo wao wenyewe hali hiyo wameiona.
Akiwa katika eneo la Kiombamvua,
Dk. Shein alipata maelezo kutoka kwa uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili,
Mifugo na Uvuvi pamoja na kutoka kwa Sheha wa Shehia ya Kiombamvua Mohamed Ali
Ame ambaye aliomba aondolewe mchanga uliokusanyika kondeni kwake ili aendelee
na kilimo ambapo mchanga ulipelekwa na maji na jumla ya tani 2,020
zilichukuliwa na Kampuni ya CRJ kwa ajili ya matumizi ya mradi wa ujenzi wa
misingi ya maji ya mvua.
Katika majumuisho yaliokwenda
sambamba na mazungumzo na viongozi wa CCM wa Wilaya hiyo huko katika hoteli ya
“SeaCliff” Kama Wilaya ya Kaskazini B, Dk. Shein alisema kuwa wapo
wafanyabiashara wa matofali wameuficha mchanga kwenye maeneo yao hali ambayo
imekuwa usumbufu kwa wananchi wanaotaka kujenga.
Akieleza historia ya uuzaji wa
mchanga, udongo, mawe na kifusi ulivyokuwa hapo zamani, Dk. Shein alisema kuwa
kunatofauti kubwa na biashara hiyo inavyofanywa hivi sasa hali ambayo inachangia
uhaba wa rasilimali hiyo.
Alisema kuwa katika shimo la
mchanga la Pangatupu mchanga umemaliza na zimebaki tani 50,000 tu za mchanga
ambao haufiki hata miezi miwili ambapo mchanga wa CheChele nao umebaki tani
2000 tu ambao umewekwa kwa ajili ya miradi ya Serikali.
Alisema kuwa jengo la Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) limesita ujenzi wake
kutokana na ukosefu wa mchanga na kupelekea mafundi wa ujenzi kutoka kampuni ya
Hainan International kutoka China kukaa bila ya kazi.
Alieleza kuwa licha ya Serikali
kusimamia rasilimali hiyo hivi sasa ambapo hatua hizo zilianza mnamo mwezi
Machi na Novemba mwaka jana 2017 bado kumetokea wananchi ambao wanahoji na kusema
kuwa Serikali inawachukulia mchanga wao.
Alisisitiza kuwa ni vyema
wananchi wakaelewa kuwa ardhi yote ya Zanzibar ni mali ya Serikali hivyo
rasilimali ya mchanga yote ni mali ya Serikali kwa mujibu wa Sheria na Katiba
ya nchi na yeye ndie msimamizi wa ardhi hiyo.
Pia, alieleza kuwa jambo jengine
lililochangia kwa kiasi kikubwa kutokea uhaba wa rasilimali hiyo ni pamoja na
kutofuatwa kwa sheria za nchi kwani tayari kila kitu kina sheria yake huku
akieleza kuwa baadhi wa viongozi na wananachi wa Wilaya hiyo wamechangia
kutokea kwa athari hiyo iliyopelekea uhaba wa mchanga.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa
juhudi za makusudi zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuzungumza na wananchi wa
maeneo yanayochimbwa mchanga yakiwemo maeneo ya Donge ambapo aliwatuma Mawaziri
wake waende kuzungumza nao ili watambue hali iliyopo hivi sasa.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali
imo katika kufanya utaratibu ili mchanga mchache uliopo uweze kutumika vizuri
na uwafae wananchi wote na wala haikusudii kuwasumbua wananchi wake juu ya
matumizi ya rasilimali hiyo hapa Zanzibar.
Aidha, alisema kuwa Serikali ina
kazi kubwa ya kuwaelimisha na kuwaeleza wananchi juu ya hali ya mchanga ilivyo
hivi sasa hapa Zanzibar.
Alisema kuwa wapo baadhi ya
wafanyabiashara walitaka kuruhusiwa waagize rasilimali hiyo kutoka Tanzania
Bara lakini Serikali imekataa huku akisisitiza kuwa kwa upande wa kisiwa cha
Pemba rasilimali hiyo ipo lakini bado inatosheleza kwa wananchi wa kisiwa
hicho.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya
Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mariam Juma Abdalla Sadalla alieleza kuwa
uchimbaji chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Serikali ulianza katika mwezi
Machi 2017 katika eneo la Donge Chechele na baadae mnamo mwezi wa Novemba 2017
kuhamia eneo la Pangatupu ambalo lilikuwa shamba la miwa chini ya Kiwanda cha
Sukari Mahonda.
Alieleza kuwa eneo la Pangatupu
lenye hekta 64 limebaki tani 50,000 tu za mchanga huku akieleza kuwa baada ya
Wizara hiyo kusimamia kiasi cha TZS Bilioni 11 zimepatika ambazo hugaiwa kwa
Halmashauri,Wizara na Hazina.
Katibu Mariam alieleza kuwa
jitihada imekuwa ikifanyika ya kupanda miti ikiwemo mikeshia na mihojoro ambapo
tayari hekta 56 zimepandwa miti ipatayo 2000 kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka huu
wa 2019 na kueleza kuwa eneo hilo limetoa ajira 700 ambalo lina Jumuiya mbili
ikiwemo ya Madereva na Jumuiya ya Wapakizi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni