Jumatatu, 18 Februari 2019

NDG.ALI AMEIR MOHAMED ASEMA CCM IMERUDI KATIKA MSTARI, AMPONGEZA DK.MABODI.


NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi(kulia), akimfariji Naibu Katibu Mkuu mstaafu ndugu Ali Ameir Mohamed(kushoto) huko nyumbani kwake Donge.


NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar kimeahidi kuendelea kuthamini kwa vitendo mchango wa waasisi na viongozi wa zamani waliohudumu katika CCM na Serikali kwa ujumla.

Ahadi hiyo ameitoa wakati alipomjulia hali Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Zanzibar ndugu Ali Ameir Mohamed nyumbani kwake Donge Wilaya ya Kaskazini Unguja.

Dk.Mabodi amesema kwamba mafanikio yaliyofikiwa ndani ya CCM yametokana na juhudi kubwa za kiutendaji zilizoasisiwa na viongozi hao waliolitumikia taifa kwa uzalendo mkubwa na kuacha alama bora za uongozi uliotukuka.

Amesema bado CCM ina mipango endelevu ya kuwashirikisha viongozi hao wa zamani katika kushauri na kuelekeza masuala mbali mbali ya kiutendaji ndani ya Chama na Serikalini.

Ameeleza kwamba taasisi hiyo ni miongoni mwa Chama pekee chenye azna na rasilimali watu ambao ni viongozi wastaafu wengi waliosaidia katika kutumia maarifa,weledi na kutoa maelekezo mbadala yanayosaidia kuimarisha CCM.

Naibu huyo Dk.Mabodi amesema Naibu Katibu huyo mstaafu ndugu Ali Ameir amekuwa ni mfano bora wa viongozi waastaa ambao mpaka sasa bado wanatumia vyema uzoefu wao kukishauri chama cha mapinduzi katika masuala mbali mbali ya kiungozi.

Naye Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Zanzibar ndugu Ali Ameir Mohamed, amempongeza Dk.Mabodi kwa kasi yake ya uongozi kushuka katika ngazi mbali mbali za wanachama kusikiliza changamoto zao kasha kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Ameeleza kwamba heshima na hadhi ya CCM kwa sasa imerudi katika mstari kutokana na juhudi za kiutendaji na uongozi bora zinazotekelezwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt.John Pombe Magufuli pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein.

Pamoja na hayo ndugu Ameir ambaye pia amewahi kushika nafasi ya Waziri wa Mambo ya ndani  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameishauri CCM kuendelea kuwatumia vizuri viongozi wastaafu hasa katika kuandika historia ya kumbukumbu ya mambo mbali mbali yanayohusu historia halisi ya Zanzibar kabla na baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Ameeleza kwamba CCM ina utajiri wa wazee wenye uwezo mkubwa katika masuala mbali mbali ya kisiasa,kijamii na kiuchumi hivyo wakiendelea kushirikishwa katika kushauri masuala mbalimbali nchi itaendelea kustawi kimaendeleo.

Ndugu Ameir amezipongeza Serikali zote mbili ya Zanzibar nay a Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ustadi wao wa kutekeleza kwa ufanisi Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 ambayo ndio kipimo sahihi cha kisiasa katika ulimwengu wa ushindani wa kisiasa katika misingi ya Demokrasia.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni