Ijumaa, 15 Februari 2019

DK.SHEIN AAGIZA OFISI ZA MATAWI YA CCM NCHINI ZIFUNGULIWE.



 MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein  akiwahutubia wanachama na viongozi wa CCM Wilaya ya Dimani.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akizungumza na Wanachama hao wa CCM Wilaya ya Dimani.
 BAADHI ya Wanachama wa CCM wa Wilaya ya Dimani walioudhuria katika Mkutano wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali mohamed Shein.


NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein ameagiza Viongozi wa taasisi hiyo kufungua Ofisi za Matawi ya Chama kwa wakati ili watekeleze shughuli za Chama kwa ufanisi mkubwa.
Agizo hilo amelitoa katika mwendelezo wa ziara yake katika Wilaya ya Magharibi ’B’,alipozungumza na viongozi na watendaji wa CCM Wilaya ya Dimani pamoja na Kamati ya Siasa ya Mkoa huo  huko katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini Zanzibar.
Dk.Shein amesema kuna baadhi ya Ofisi za Matawi ya Chama cha Mapinduzi hayafunguliwi jambo ambalo ni hatari katika ustawi wa Siasa ya CCM.
Ameeleza kuwa  toka enzi za ASP na TANU shughuli mbali mbali za kuimarisha Chama Cha Mapinduzi zilifanyika katika Ofisi za  Matawi na  Maskani  hivyo ni jambo la busara viongozi wa CCM wakaendeleza utamaduni huo.
Amesema Ofisi inapofungwa muda wote inawakosesha fursa wanachama kupata sehemu sahihi ya kujadili masuala mbali mbali ya kuijenga taasisi na hasa vikao vya kikatiba.
Amesema kuanzia sasa nchini Matawi yote ya CCM yanatakiwa kufunguliwa mara kwa mara na viongozi husika wawepo kwa lengo la kuratibu masuala mbali mbali ya kisiasa na kijamii.
Katika maelezo yake Dk.Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, amewataka viongozi ,watendaji pamoja na wanachama wa CCM wafanye kazi za kuimarisha Chama ili 2020 kazi ya kupata ushindi iwe ni rahisi.
Aidha amesema kuwa kiongozi yeyote ndani ya CCM anayejiona kuwa hawezi kwenda na kasi ya mabadiliko ya kiutendaji ndani Chama, aachie ngazi na kuwapisha wengine wenye uwezo ili Chama kisonge mbele kimaendeleo.
Dk. Shein amesisitiza Umoja,mshikamano ndani ya chama hicho ili kujenga chama bora kitakachoshinda katika uchaguzi mkuu ujao na kuendelea kuongoza dola kwa mafanikio zaidi.  

Amesema nguvu za chama hicho ni umoja, hivyo akawataka wanachama kuendelea kushikamana  na kuepuka mifarakano na utengano, huku akiwataka wanachama kufuata maadili ya chama hicho katika kushajiisha umoja.


Amesema Serikali ya Mapinduzi inayoongozwa na CCM ilianza maadalizi ya uchaguzi huo mara tu baada ya uchaguzi wa marudio wa 2016 kwa kuandaa mpango wa utekelezaji wa Ilani,

Amesema serikali imejitahidi kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa Ilani kwa kufanikisha miradi mbali mbali ya maendeleo, ikiwemo sekta za maji, barabara, afya na elimu.

Amesema baadhi ya viongozi ikiwemo Wabunge na Wawakilishi hawana habari kabisa na utekelezaji wa Ilani, hivyo akawataka kuwa imara na kutekeleza kwa vitendo ilani ya chama hicho.

Aidha, aliwataka kutumia vyema muda uliobaki kwa kutekelza ahadi walizozitowa kwa wapiga kura.
Naye  Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,  Abdalla Juma Saadalla ‘Mabodo’ amesema CCM inamima vizuri utekelezaji wa Ilani.

Amesema CCM imezidi kuimarika kutokana na ushirikiano na uchapakazi baina ya viongozi wa Chama na Serikali katika Wilaya hiyo.

Aidha, taarifa ya Chama Wilaya hiyo, imebainisha wanachama 27,272 wameandikishwa Wilayani humo, huku asilimia sita ya wanaachama hao wakiwa tayri wamelipa ada za uanachama zilizofikia zaidi ya shilingi Milioni 2.5

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni