Ijumaa, 1 Februari 2019

NDG.TUNU: AWAPIGA MSASA WAJUMBE WA MABARAZA YA U.W.T WILAYA ZA AMANI NA MJINI,APOKEA WANACHAMA WAPYA.

   NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi UWT Zanibar Ndugu Tunu Juma Kondo akikabidhi kadi za UWT kwa wanachama wapya wa Umoja huo.


 NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.


Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi(UWT) Tanzania anayefanyia kazi zake Zanzibar Ndugu Tunu Juma Kondo   amewataka Akina mama wa Umoja huo kuendeleza utamaduni wa kusoma kanuni,miongozo na machapisho mbali mbali ya UWT na CCM ili wajue kwa upana majukumu yao yakiwemo ya kusimamia na kutekeleza kazi zao za kila siku.  

Rai hiyo almeitoa katika ziara yake ya kujitambulisha kwa Wajumbe wa Mabaraza ya ya UWT Wilaya za Mjini na Amani za Mkoa  kichama katika ukumbi wa CCM amani  Mkoa,amesema Umoja huo una miongozo na kanuni zake zinazotakiwa kusomwa na viongozi na wanachama ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.

Amefafanua kwamba kila kiongozi ndani ya umoja huo akijua ipasavyo muundo wa sahihi wa majukumu yake, mipaka na wajibu itasaidia kuondosha migongano ya kutegeana kimajukumu na badala yake itaongeza ari na juhudi za kiutendaji ndani ya umoja huo.

Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo, Ndugu Tunu amesisitiza kuwekwa utaratibu wa kudumu kwa Viongozi na Watendaji wa Taasisi hiyo kufanya ziara za mara kwa mara katika maeneo mbali mbali ya akina mama kwa nia ya kubaini changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati.

Aidha amewasihi wajumbe hao kuepuka kujiingiza katika makundi yasiyofaa yayoweza kuhatarisha umoja huo na kusababisha migogoro kwa UWT na Chama cha Mapinduzi kwa ujumla.

Aidha amesema wanawake wa UWT ndio ni jeshi kubwa la kisiasa la CCM hivyo wajipange kisaikolojia kila mmoja kwa nafasi yake kwa kuhakikisha Chama kinashinda kwa kishindo uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Amesema Ibara ya Tano ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 imewaelekeza viongozi na wanachama kuhakikisha CCM inashinda kwa kila uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu wa dola , na UWT itakuwa mstari wa mbele kutekeleza matakwa hayo ya Kikatiba.

Katika hatua nyingine amewakumbusha juu ya kujitokeza kwa wingi kushiriki shamrashara ya wiki ya maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM inayotimiza miaka 42,ambapo Chama na Jumuiya zake wanaendelea kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.

Amewasihi wanawake kuwa karibu na watoto wao kwa kuwafunza uzalendo na kuwalea katika misingi ya malezi bora kwa lengo la kuandaa makada imara watakaoweza kurithi mambo mema ya viongozi wa sasa nao wakayaendeleza kwa ufanisi.

Pamoja na hayo aliwapongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa juhudi zao za kusimamia vizuri utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 pamoja na kulinda tunu za Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Ndugu Tunu ameeleza kwamba juhudi za viongozi hao zinatakiwa kuthamini kwani hivi karibuni kupitia Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamesamehe Deni la umeme kwa Zanzibar iliyokuwa ikidaiwa tozo la VAT ya zaidi ya shilingi bilioni 22.

Awali akisoma risala ya Umoja huo, Katibu wa UWT Mkoa wa Mjini Ndugu   Stahamili Omar amesema  umoja huo umejipanga vizuri katika kutekeleza shughuli mbali mbali za kitaasisi sambamba na kupuni miradi mbali mbali ya ujasiria mali itakayoweza kukuza uchumi wa jumuiya na Chama kwa ujumla.

Ameitaja miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na  kuwainua kiuchumi Akina mama kwa kuwapatia mafunzo ya ujasiriamali ili wajikimu kimaisha.

Katika ziara hiyo ya Naibu Katibu Mkuu wa UWT, alipokea mamia ya wanachama wapya wa umoja huo waliojiunga kutokana na Sera imara za Visiwani Zanzibar UWT.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni