RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesisitiza suala zima
la maadili kwa viongozi ikiwa ni pamoja na kujua wajibu wao na wanao waongoza.
Rais Dk. Shein aliyasema katika Majumuisho ya ziara yake ya Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini
Magharibi yaliyofanyika katika ukumbi wa Kariakoo mjini Zanzibar ambapo
viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Mke wa Rais wa Zanzibar Mama
Mwanamwema Shein.
Katika hotuba yake
Rais Dk. Shein alieleza kuwa kiongozi anapaswa kuwa na maadili mazuri ili iwe
rahisi katika utendaji wake wa kazi hatua ambayo itawasaidia mpaka wale
anaowaongoza kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi kwa taarifa ya Wilaya ya Mjini pamoja na kuwapongeza
Mkuu wa Mkoa huo pamoja na Mkuu wa Wilaya wake kwa juhudi wanazozichukuwa
katika Wilaya hiyo na kusema kuwa Wilaya hiyo inakwenda vizuri.
Akieleza miongoni mwa
changamoto zilizomo katika Wilaya ya Mjini ni pamoja na ongezeko kuwa la watu
katika Wilaya hiyo ambapo idadi ya watu wake ni sawa na idadi ya watu wa
Zanzibar mnamo mwaka 1964.
Aidha, Rais Dk. Shein
alieleza changamoto ya ukosefu wa ajira hapa Zanzibar na kueleza juhudi
zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali licha ya wanaohitaji ajira kuwa wengi.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa ujenzi wa matangi ya maji ambayo hayajawahi kujengwa katika nchi yoyote
katika Bara la Afrika yatakuwa ni ya kihistoria kwa Zanzibar kwani yataondosha
changamoto ya maji kwani ni mradi wa uhai wa wananchi wa Zanzibar.
Aliwanasihi viongozi
wa Wilaya ya Mjini kuendelea kufanya kazi kwa pamoja kwa kushauriana ili wazidi
kupata mafanikio katika shughuli zao za kuwaletea maendeleo wananchi.
Alisema kuwa Zanzibar
itaendelea kupambana na umasikini wake kwa hali na mali na haitokuwa tayari
kuyumbishwa.
Alieleza mafanikio ya
ziara zake ikiwemo ile aliyoifanya katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu
ambapo hivi karibuni ulikuja ujumbe wa Khalifa Fund kutoka Abudhabi ambao
umeahidi kutoa fedha za kwa ajili ya vijana ili waweze kujiajiri wenyewe ambapo
fedha hizo ziko njiani, na kusisitiza kuwa vijana kamwe hawatotupwa.
Alieleza kuwa kwa
upande wa Indonesia tayari washakubaliani na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
katika zao la mwani na matarajio yake kuwa akina mama wanaolima zao hilo
watafaidika kwani utakuwa na bei nzuri
kwani hatua hiyo pia itanyajua sekta ya ajira.
Alieleza jitihada
zitafanywa ili kuhakikisha vijana wanapata ajira, na kueleza kuwa hilo halitofanikiwa ikiwa hakuna maadili,
kwani maadili ni suala muhimu.
Aidha, alisisitiza
suala zima la kupambana na rushwa na kuwatanabaisha viongozi kuwa wasije
kuteleza na kuingia katika balaa hilo.
Kwa upande wa sekta ya
elimu, Rais Dk. Shein alisema kuwa kuna jambo baya sana limeibuka la kughushi
mitihani jambo ambalo ni baya sana na kuutaka uongozi wa Wilaya kushirikiana na
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kupambana na jambo hilo.
Alisema kuwa tayari
ameshaagiza kutafutwa watu ambao wanawaharibia watoto masomo yao na kuutaka uongozi
wa Wilaya zote kushirikiana na Wizara hiyo ya Elimu katika kupambana na janga
hilo.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa Serikali imeahidi kutoa vifaa bure na kueleza kuwa tayari baadhi ya vifaa
vimeshaanza kutolewa bure maskulini yakiwemo
mabuku huku akisisitiza kuwa hata huduma za afya zimekuwa zikitolewa bure hapa
Zanzibar kwani hayo ndio malengo ya Mapinduzi chini ya uongozi wa Marehemu Mzee
Karume.
Alieleza kuwa kuwepo
kwa amani na utulivu hapa Zanzibar kumeweza kuwavutia wageni kutoka nchi mbali
mbali duniani kuja kuitembelea Zanzibar na kusisitiza haja ya kulindwa na
kuenziwa ili Zanzibar izidi kupata mafanikio ikiwemo kuongezeka kwa watalii.
Rais Dk. Shein
alitumia fursa hiyo kuutaka uongozi wa Wizalaya ya Mjini ambao bado unaendelea
kukodi nyumba ya Ofisi kwa ghara za TZS Milioni 4.8 kwa mwezi, kuharakisha
kujenga jengo lao ili kuepuka matumizi hayo ya makubwa ya fedha.
Kwa upande wa miradi
katika Wilaya ya Mjini, Rais Dk. Shein alisema kuwa tayari miradi 13
imekamilika na miradi 14 imo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na 9 kati
ya hiyo bado haijaaza ikiwemo barabara ya Shauri Moyo hadi Mboriborini na
kutaka kuhakikisha miradi hiyo inafanyiwa kazi.
Alisema kuwa wakati
Serikali ikitekeleza kujenga mtaro mkubwa wa maji ameshtuka na baadhi ya
wananchi kutoa lawama zisizo na msingi na kuwataka viongozi wa Mkoa na Wilaya
kutoa elimu kwa wananchi juu ya miradi ya maendeleo ili wawache kulaumu.
Alisema kuwa Serikali
inafanya kazi kwa ajili ya wananchi hivyo, aliwataka wasiwe mbali na wananchi
ili wawape elimu juu ya miradi yao.
Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za
Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir alieleza
mikakati iliyowekwa na Serikali katika kuendeleza suala zima la Ugatuzi.
Akitoa neno la
shukurani, Mkuu wa Mkoa Mjini Mgharibi Ayoub Mohammed Mahmoud alimuhakikishia
Dk. Shein kuwa watakahikisha suala zima la maadili linafayiwa kazi katika
Wilaya hiyo kuanzia ngazi zote zikiwemo Shehia, Wilaya hadi Mkoa na kuahidi
kutekeleza dhamira hiyo ya Dk. Shein.
Mkuu wa Mkoa huyo
alisema kuwa na wale wote ambao watakwenda kinyume na maadili taratibu na hatua za kisheria zinafuatwa.
Alieleza mikakati
iliyowekwa na Mkoa wake kupitia Wilaya zake ikiwa ni pamoja na kujifunza kwa
ajili ya kuendeleza Manispaa zake.
Alieleza kuwa Ofisi
yake inadhamiria katika Bajeti ijayo ya mwaka 2019-2020 kama fedha zitakuwepo
basi Manispaa zao ziweze kuchangia asilimia 5 badala ya asilimia 2, ambapo
katika mgao asilimia 2 zisaidie vijana asilimia 2 zisaidie akina mama na
asilimia moja isaidie makundi maalum.
Alisisitiza kuwa mambo
yote yaliyokuwa kinyumme na tamaduni za Kizanzibari yatafanyiwa kazi katika kuyatokomeza na kueleza kuwa
wanachukua maelekezo ya kutoa elimu ya miradi na dhamira ya Serikali kwa ajili
ya miradi hiyo na kuwaeleza Sera za nchi hii sasa ni maendeleo kwa wananchi.
Ayoub alitumia fursa
hiyo kutoa pongezi kwa Serikali kwa kuiwezesha kinyenzo Wilaya hiyo katika
suala zima la ulinzi wa kisasa, na kueleza haja ya kuenezwa vifaa hivyo katika
maeneo mengine ya mjini kwani imethibitika kwamba vifaa hivyo vinasaidia kwa
kiasi kikubwa kuwakamata wahalifu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni