Ijumaa, 22 Februari 2019

WANANCHI WASEMA DK.SHEIN NI SHUJAA WA MAENDELEO


BARABARA ya Mkanyageni-Kangani  Wilaya ya Mkoani Pemba.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

BAADHI ya Wananchi wa Wilaya ya Mkoani Pemba wamepongeza juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miundo mbinu ya Barabara ndani ya Wilaya hiyo.

Wameeleza kuwa Serikali ya awamu ya saba chini ya uongozi wa Dk.Shein, imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutatua matatizo sugu yaliyowathiri wananchi wa wilaya hiyo kwa miaka mingi kabla na baada ya  Mapinduzi ya mwaka 1964.

Wakizungumza kwa wakati tofauti baadhi ya wananchi hao, mara baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein kuweka Jiwe la Msingi katika Barabara ya Mkanyageni -Kangani (KM5), wamesema barabara hiyo itakuwa ni mkombozi kwa wananchi wa wilaya hiyo na maeneo jirani.

Mkaazi wa Kijiji cha Mkanyageni Juma Faki Hamad(45), amesema barabara ni moja ya kichocheo cha maendeleo kwa wananchi waoishi vijijini kwani wanapata kusafirisha mazao na bidhaa mbali mbali kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

Naye Mkaazi wa Kijiji cha Mkanyageni Fatma Masoud Kombo( 50) amempongeza Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein kwa juhudi zake za kutengeneza barabara hiyo itakayokuwa mkombozi kwa Akina mama wajawazito kufika kwa wakati katika Vituo vya Afya.

Katika maelezo yake Bi.Fatma amemtaja Dk.Shein kuwa ni shujaa wa maendeleo anayeasisi maendeleo ya kuvinufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Ameeleza kwamba Dk.Shein amekuwa ni kiongozi muadilifu anayejali maisha ya wananchi wa kipato cha chini kwa sasa amewafanya wamekuwa na hadhi kutokana na kuimarika kwa huduma mbali mbali za kijamii na kiuchumi.

Naye Zuwena Hiji Kombo(65), amesema mtu yeyote anashindwa kushukru na kuthamini huduma za kimaendeleo zinazotekelezwa na Serikali, mtu huyo atakuwa hana uzalendo na hastahiki kuishi katika jamii ya watu wanaopenda maendeleo ya Zanzibar.

Said Nassor Mjaja(39), amewataka wananchi wa Wilaya ya Mkoani kuendeleza utamaduni wa ustarabu na kuachana na siasa zilizopitwa na wakati za kuharibu miundombinu mbali mbali inayotekelezwa na Serikali kwani wanaonufaika ni wananchi wote.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni