Jumatatu, 11 Februari 2019

NDG.TUNU AENDELEA NA ZIARA YAKE UWT WILAYA YA MFENESINI.

  
 NAIBU Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Tunu Juma Kondo akiwahutubia Wajumbe wa Kamati Tekelezaji ya Umoja huo Wilaya ya Mfenesini.

 MWENYEKITI wa UWT Mkoa wa Magharibi Ndugu Zainab Ali Maulid akizungumza katika hafla hiyo.

 MWENYEKITI wa UWT Wilaya ya Mfenesini Ndugu Majuto Juma Haji akifungua Kikao hicho.

 KATIBU wa UWT Wilaya ya Mfenesini Ndugu Pili Issa Juma akisoma taarifa ya Umoja huo.

 WAJUMBE wa Kamati Tekelezaji wa UWT Wilaya ya Mfenesini.

 NAIBU Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Tunu Juma Kondo akikabidhi kadi ya UWT kwa Wanachama wapya.



 NAIBU Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Tunu Juma Kondo akikabidhiwa zawadi ya mayai na umoja huo.

 NAIBU Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Tunu Juma Kondo akikabidhiwa zawadi ya Kuku.

 NAIBU Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Tunu Juma Kondo akikabidhiwa zawadi ya mkate wa mayai.


NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Zanzibar ndugu Tunu Juma Kondo amewatahadharisha Akina Mama wa Umoja huo kuepuka kutumiwa na wanachama wasiokuwa waadilifu wanaosaka nafasi za Uongozi ndani ya CCM kabla ya muda wake.

Tahadhari hiyo ameitoa leo katika mwendelezo wa ziara ya kujitambulisha kwa Kamati Tekelezaji ya UWT Wilaya ya Mfenesini iliyofanyika Welezo Unguja.

Amesema UWT itachukua hatua kali za kimaadili kwa mwanachama yeyote wa Umoja huo atakayebainika kutumiwa na wasaka madaraka kabla ya muda wa Kikatiba.

Amesema Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi ni waadilifu,waaminifu na wenye misimamo imara ya kusimamia mambo mema ya kuimarisha UWT na CCM hivyo mtu yeyote atakayewashawishi kutengeneza makundi ya kufanya kampeni za kusaka ungozi kwa sasa wamkatae na kutoa taarifa sehemu husika.

Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo, amefafanua kuwa muda wa kufanya kampeni za kusaka nafasi za uongozi kupitia CCM kwa sasa bado haujafika hivyo watu wanaosaka nafasi za Urais, Ubunge,Uwakilishi na Udiwani  wavumilivu na kuwaachia wenzao wamalize muda wao bila usumbufu.

Kupitia ziara hiyo Tunu, aliwambia Akina Mama hao ambao ni Wajumbe wa Kamati Tekelezaji ya UWT Wilaya hiyo kuendelea kuwa wabunifu wa miradi mbali mbali ya kujiingizia kipato ili kwenda sambamba na Sera ya CCM ya Siasa na Uchumi.

Aidha amesema kwamba CCM bado ina matumaini makubwa na wanachama hao katika kutekeleza kwa vitendo jukumu la msingi la Chama chochote cha siasa kwa kuhakikisha taasisi hiyo inashinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa Dola mwaka 2020.

Pamoja na hayo amewapongeza viongozi wakuu wa  Chama Cha Mapinduzi  Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein kwa juhudi zao za kuwaletea maendeleo wananchi sambamba na kuwaamini Wanawake na kuwapatia fursa za kiutendaji na kiuongozi.

Ndugu Tunu amewakumbusha Akina Mama hao kuwa Katiba ya UWT inasisitiza kufanyika kwa vikao vya mara kwa mara ili kupanga masuala mbali mbali ya kuimarisha umoja huo kwa maslahi ya Chama Cha Mapinduzi.

Naye Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Magharibi Unguja, Ndugu Zainab Ali Maulid ameeleza kuwa maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu huyo watayafanyia kazi ili kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya kiutendaji ndani ya Chama na Jumuiya zake.

Amesema anajivunia kuwa na Jeshi kubwa la wanawake ndani ya Mkoa huo ambao muda wote wamekuwa mstari wa mbele kutekeleza majukumu mbali mbali ya umoja huo ili kwenda sambamba na matakwa ya zama za sasa katika siasa za ushindani.

Awali akisoma Taarifa ya UWT Wilaya ya Mfenesini Katibu wa Umoja huo,ndugu Pili Issa Juma amesema kwamba umoja huo umeendelea kufanya kazi za Chama na Jumuiya kwa nia ya kuweka mazingira rafiki ya kila mwanamke kunufaika na fursa zinazomzunguka.

Ameeleza kuwa Umoja huo unapongeza Baraza la Mawaziri la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Dk.John Pombe Magufuli kwa maamuzi yao yenye busara ya kusamehe malimbikizo ya VAT ya umeme uliokuwa ikidaiwa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO).

Amesema umoja huo umeendelea kuwa ni chachu ya maendeleo ya kuwaunganisha wanawake wa rika mbali mbali ili wawe na nguvu za pamoja katika kusimamia na kuendeleza ustawi wa maendeleo ya CCM na Jumuiya hiyo.

Katiba ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu Tunu, amepokea wanachama wapya na kuwakabidhi kadi za uanachama.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni