Jumatano, 13 Februari 2019

DK.SHEIN AWEKA JIWE LA MSINGI KITUO CHA AFYA KIANGA.



 RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiweka udongo katika Mti alioupanda katika Kituo Cha Afya cha Kianga alichokiwekea Jiwe la Msingi leo.

  RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akikagua vyumba vya kituo cha Afya cha Kianga.

 BAADHI ya Wananchi na Wanafunzi mbali mbali walioudhuria katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi katika Kituo hicho.

 VIJANA wa Chama Cha Mapinduzi wakiimba na kuhamasisha katika hafla hiyo.

 NAIBU Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mihayo Juma Nhunga akizungumza katika hala hiyo.

 Naibu Katibu Mkuu, (WN) Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Abdalla Hassan Mitawi akitoa tathimini ya ujenzi wa Kituo hicho kilichojengwa na TASAF kwa kushirikiana na wananchi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi wa shehiya ya Kianga, Wilaya Magharibi 'A' kukitunza Kituo cha Afya ili kitoe huduma bora kwa jamii.
Wito huo ameutoa katika hafla ya Uwekaji wa Jiwe la msingi la Kituo cha Afya cha Kianga, kilichojengwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF kwa mashirikiano na Wananchi na Kianga.
Amesema suala la upatikanaji wa huduma bora za Afya nchini halina mbadala, hivyo kuna kila sababu za kukitunza kituo hicho ili wananchi wa shehiya jirani wanufaike.
Amesema wananchi kuendelea na tamaduni za kupata huduma za afya kupitia njia za jadi, kuna umuhimu mkubwa wa kukitumia ipasavyo kituo hicho, ambacho kitaendeshwa kupitia afya ya msingi chini ya mfumo wa Ugatuzi.
Aidha Dk. Shein ameiagiza Wizara Afya kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya Magharibi "A" kuhakikisha kituo hicho kinakuwa katika mazingira bora, ikiwa pamoja na kukipatia wataalamu wa kukihudumia.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza wnanachi wa Kianga kwa uamuzi wao uliolenga kupatiwa huduma za afya, ili kuondokana na kadhia ya muda mrefu ya kufuata huduma hizo katika vituo vya afya vilivyopo masafa marefu.
Amezungumzia historia ya huduma za Afya nchini, Dk. Shein amesema Mapinduzi ya 1964 yamekuja kuwakomboa Wazanzibari wanyonge kuondokana na kadhia ya kukosa huduma bora za afya.
Alisema kabla ya Mapinduzi, huduma za Afya (kama ilivyo kwa elimu), zilitolewa kwa misingi ya ubaguzi kuambatana na uwezo wa mtu, hivyo Wazanzibari walio wengi walikosa huduma hiyo muhimu.
Katika hatua nyengine Dk. Shein amewapongeza watendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF Zanzibar, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais  pamoja na wananchi wote waliofanikisha ujenzi wa kituo hicho.
 Awali, Waziri wa Nchi, (OR), Tawala la Mikoa na Serikali za Mitaaa na Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir alipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Rais, Dk. Shein pamoja na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Magufuli za kuimarisha mfuko huo kifedha kupitia Benki ya Dunia (World Bank).
Amesema ni haki ya wana CCM kuendelea kutembea kifua mbele, kutokana na mafanikio makubwa yaliopatikana katika  utekelezaji wa Ilani ya CCM, kupitia sekta tofauti ikiwemo Afya.
Waziri Kheir, ameahidi kushirikiana kikamilifu na Wizara ya Afya kwa kuandaa mikakati  ili  kupata wataalamu bora wa kukiendeleza kituo hicho.
Nae, Naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mihayo Juma Nhunga, amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutawaondolea usumbufu wananchi wa Kainga wa kufuta huduma za Afya katika vituo vya Kizimbani na Bumbwi sudi.
Ameeleza kuwa hatua hiyo itafungua milango ya maendeleo kwa wananchi wote wa Jimbo la Mwera.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu, (WN) Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Abdalla Hassan Witawi, alisema ujenzi wa kituo hicho ulioanza Julai, 2018 umegharimu zaidi ya shilingi Milioni 104 hadi sasa, ukifikia asilimia 85 ya ujenzi wote.
Mitawi alizipongeza Ofisi za Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi, na Wilaya Magharibi 'A' pamoja na Kamati ya Uongozi wa Shehiya ya Kianga kwa mashirkiano yao yaliofanikisha vyema ujenzi wa kituo hicho.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni