NA IS-HAKA OMAR, PEMBA.
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT) Taifa Ndugu Gaudencia Kabaka amewataka wanachama wa CCM kisiwani Pemba, kuendelea kuonyesha njia za mafanikio kwa kubuni na kuanzisha miradi endelevu ya kuisaidia jamii.
Rai hiyo ameitoa leo katika ziara yake ya mwanzo kisiwani humo ya kujitambulisha na kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 katika miradi inayotekelewa na UWT pamoja na CCM kwa ujumla.
Akizungumza mara baada ya kushiriki ujenzi wa shule ya sekondari ya Kangagani Wete Pemba inayojengwa kwa nguvu za CCM pamoja na wananchi wa kijiji hicho,Gaudencia ameeleza kuwa CCM imekuwa ni taasisi bora ya kisiasa inayotekeleza miradi endelevu inayogusa maisha ya wananchi wa ngazi zote katika jamii.
Amesema kitendo cha Wana CCM kujitolea kujenga madarasa ya shule ya sekondari Kangagani ni hatua kubwa inayochochea harakati za maendeleo katika kuimarisha sekta ya Elimu Zanzibar.
Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo amesema maamuzi ya wananchi hao ya kujenga shule hiyo ambayo wanafunzi watapa elimu bora kupitia mazingira rafiki ya miundo mbinu bora ya majengo yanayoendana na hadhi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ndugu Gaudensia ameeleza kuwa CCM imeendelea kupiga hatua kubwa ya kuanzisha miradi mbali mbali ya kiuchumi na kijamii kwa lengo la kutekeleza kwa ufanisi ahadi zilizotolewa katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.
Wakati huo huo, Bi.Gaudensia ametembelea nyumba ya kuwatunza Wazee katika kijiji cha Dimbani Pemba amesema CCM inathamini na kuwaenzi wazee ambao ndio chimbuko la maendeleo ya nchi.
Amesema Wazee wamefanya kazi kubwa ya kujenga maendeleo ya nchi katika nyanja mbali mbali za kisiasa,kiuchumi na kijamii hivyo lazima watunzwe na kuishi katika mazingira bora.
Ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Idara ya Wazee na Ustawi wa Jamii Pemba kwa kuwatunza wazee, wanaoishi katika mazingira mazuri kwa kupata huduma bora za mavazi, malazi na huduma za afya.
Naye Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa ndugu Thuwaiba Kisasi, amesema kuwa wanawake nchini wameendelea kujitokeza kwa wingi katika masuala mbali mbali ya kuimarisha CCM na Jumuiya zake.
Katika ziara hiyo Mwenyekiti huyo Bi.Gaudensia Kabaka amefuatana na viongozi mbali mbali wa UWT wakiwemo Katibu Mkuu wa UWT Taifa Mwl.Queen Mlozi, Makamu Mwenyekiti wa UWT ndugu Thuwaiba Kisasi,Naibu Katibu Mkuu wa UWT Tanzania bara ndugu Jesca Mbogo,Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanibar ndugu Tunu Juma Kondo pamoja na Wajumbe wa Kamati Tekelezaji ya UWT Taifa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni