Ijumaa, 8 Machi 2019

BI.GUDENSIA ATOA WITO WA MANUFAA KWA WANANCHI WA PEMBA



Mwenyekiti wa UWT Taifa Bi.Gaudensia Kabaka akiwa Kangani Pemba. 


NA IS-HAKA OMAR,PEMBA.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewasihi wananchi wa kisiwa cha Pemba, wanaoamini mfumo bora wa siasa za CCM kuwa ndio chimbuko la maendeleo ya nchi wafanye maamuzi sahihi ya kujiunga na taasisi hiyo.

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa UWT Taifa Bi.Gaudensia Kabaka katika mwendeleo wa ziara yake, huko Wilaya ya Mkoani mara baada ya kushiriki shughuli za ujenzi wa Tawi la CCM Kangani Pemba.

Bi.Gaudensia amesema wapo maelfu ya wananchi kisiwani Pemba wanakipenda na kukiamini Chama Cha Mapinduzi lakini wamekuwa wakitishwa na kuwekwa katika hali ya hofu na baadhi ya Vyama vya upinzani, jambo ambalo ni kinyume na misingi ya Demokrasia pamoja na haki za binadamu.

Amesema kila mwananchi hana haki ya kujiunga na Chama chochote cha kisiasa bila kulazishwa,kutishwa,kuharibiwa mali zake kwani hiyo ni moja ya haki yake ya msingi ya kiraia.

Mwenyekiti huyo ameeleza kwamba CCM haitovumilia baadhi ya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu vikiwemo kupigwa, kunyanyaswa, kutengwa katika shughuli za kijamii, kung'olewa mazao na vipando, kuchomwa nyumba pamoja na kutishiwa maisha wanavyofanyiwa baadhi ya wanachama wa CCM kisiwani humo.

Katika maelezo yake Bi.Gaidensia ameeleza kuwa CCM itaendelea kuwa balozi wa amani na mtetezi namba moja wa haki za wananchi wa makundi yote bila kujali dini,kabila rangi na tofauti za kisiasa.

Ametoa  wito kwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kuendeleza siasa za kistaarabu bila ya kuwabagua wapinzani na pindi panapotolewa huduma za kijamii zitolewa kwa wananchi wote.

"Fahari ya CCM ni pale Serikali zake mbili zinapotoa huduma zote za kijamii,kisiasa na kiuchumi bila ubaguzi kwani suala la maendeleo halina Chama bali ni haki ya wananchi wote.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amekuwa mstari wa mbele kuwapelekea wananchi maendeleo endelevu, sambamba na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli naye amekuwa kinara wa maendeleo na mtetezi wa haki za wanyonge.", amefafanua Bi.Gaudensia na kuongeza kuwa CCM inaahidi na kutekeleza kwa vitendo na kwa wakati mwafaka.

Kupitia ziara yake hiyo ya kukagua Utekelezaji wa Ilani, Mwenyekiti huyo amewapongeza Viongozi mbali mbali wa CCM na Jumuiya zake kwa ushirikiano wao mzuri wa kujenga Tawi la Kisasa la Kangani linaloendana na hadhi ya CCM.

Amebainisha kwamba ziara yake hiyo imekuwa ni sehemu ya kujionea miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na CCM pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanibar katika maeneo ya mijini na vijijini Pemba.

Amesema siasa za maji taka,migogoro na machafuko tayari zimepitwa na wakati na badala yake vyama vya kisiasa vinatakiwa kushindana kwa Sera za maendeleo zenye lengo la kutatua kero za wananchi.

Amesema katika mabadiliko ya kimaendeleo katika siasa za zama za sasa wanawake wamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kwa kunufaika na fursa mbali mbali katika nyanja za uongozi,utumishi,siasa pamoja uchumi.

Katika ziara hiyo aliwasihi Wana CCM wa Visiwa vya Pemba hasa Wanawake wa rika mbali mbali bila kujali tofauri za kisiasa wajitokeze kwa wingi katika kongamano lililoandaliwa na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania litakalofanyika Machi 9,mwaka 2019 katika uwanja wa Tibirinzi Wilaya ya Chake Chake kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 9:00 mchana.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni