Alhamisi, 28 Machi 2019

MHE.NDUGAI ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM MKOA KUSINI UNGUJA.


 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Ndugu Job Ndugai akiangalia ulazaji wa mipira katika mradi mkubwa wa Maji unaojengwa katika Kijiji hicho kwa lengo la kumaliza tatizo la maji safi na salama,katika ziara yake Mkoa wa Kusini Unguja.


SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Job Ndugai amesema ameridhishwa na utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi(CCM) ambao unaofanywa kwa upande wa maeneo ya visiwani humu.

Amesema kwa upande wake akiwa mlezi wa CCM wa mikoa ya Kaskazini Unguja na Kusini Unguja ameridhishwa na mipango ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ) inavyofanywa katika maeneo ya Cheju na Chwaka ikiwemo katika kuhakikisha inawaletea maji na kuimarisha kilimo cha mpunga.

Kauli hiyo ameitoa jana wakati akitembelea maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kusini ambapo alisema katika upande wa kilimo amejionea mwenyewe kuwa serikali ya SMZ  imeweka mipango mizuri ya kuhakikisha kiwango cha kilimo cha umwagiliaji kinaongezeka.

Alisema Serikali ya SMZ imeweka mpango mzuri kupitia mradi wa kilimo cha umwagiliaji cha pamoja(PADEPU) wa zao la mpunga ambapo kilimo hicho kinatumia eneo dogo,mbegu ndogo kwa kuzalisha kiwango kikubwa cha zao hilo.

"Mpango huu ni mzuri kutokana na kuwa utawezesha Zanzibar kuwa na uwakika wa kujitegemea wa chakula cha mpunga na kuacha kuagiza kutoka nje ya visiwa hivi vya Zanzibar,"alisema

Katika maelezo yake alisema mbali na hatua hiyo,pia ameridhishwa na matumizi ya fedha za mfuko wa jimbo unavyotumika kwa kufanya maendeleo makubwa katika maeeneo ya mkoa huo.

"Ninaomba uongozi wa CCM kufuatilia kwa karibu fedha za mfuko wa jimbo ili kujua namna fedha hizo zinavyotumika na kwamba haipendezi kuona fedha hizo zinatumika vibaya lakini ninardhishwa na utekelezaji wa mipango ya ilani ya CCM kwa SMZ na matumizi ya fedha za jimbo,"alisema Spika Ndugai.

Alisema kwa upande wa sekta ya maji Serikali ya SMZ inatekeleza vyema ilani ya uchaguzi kwa kuhakikisha wananchi wa maeneo ya jimbo la Chwaka wanapata maji safi na salama ya uwakika kutoka katika kisima cha Bambi.

"Ninaomba utandikaji wa bomba za maji katika maeneo ya Chwaka ambao ni urefu wa kilomita 7 umalizike kwa wakati ili wananchi hawa wapate maji kutokana na kuwa ni muda mrefu wamekuwa hawapati maji safi na salama na badala yake wamekuwa wakitumia maji ya chumvi hivyo kama CCM ilivyohaidi katika ilani yake hakuna haja ya kutekeleza kwa wakati,"alisema Ndugai

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo,Mifugo Maliasili na Uvuvi, Dk.Makame Ali Ussi alisema katika mradi huo wa PADEPU unatarajia kuwezesha Zanzibar kuongeza kiwango cha shughuli za kilimo cha umwagiliaji wa zao la mpunga ambapo katika mradi huo kutakuwa na visima 44 vya maji kuhakikisha maji ya kutosha yanakuwepo.

Alisema hatua hiyo ni sehemu ya ilani ya uchaguzi ya ibara 72 kifungu C ambapo CCM inaelekeza serikali ya SMZ kuongeza hekta 1500 za uzalishaji wa kilimo cha mpunga katika maeneo ya visiwani humu ikiwemo Cheju.

"Tunaendelea na mpango huu wa kuongeza kiwango cha shughuli za kilimo cha umwagiliaji ambapo mpaka sasa katika kipindi cha miaka 10 tumeweza kupiga hatua kubwa ya kuongeza uzalishaji wa kilimo cha umwagiliaji cha mpunga,"alisema

Aliongeza kuwa Serikali ya SMZ itaendeleza mapinduzi ya kilimo cha umwagiliaji kwa kipindi chote kama ilivyokuwa katika mipango yake na ya Chama tawala.





















Hakuna maoni:

Chapisha Maoni