Jumapili, 24 Machi 2019

DK.MABODI: AVIONYA VYAMA VYA SIASA VINAVYOHATARISHA AMANI, MHE,JAMAL AKABIDHI GARI LA MILIONI 29.5.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akiwahutubia Wananchi wa Jimbo la Magomeni kupitia Mkutano wa Ndani wa CCM.


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewaonya baadhi ya Viongozi wa kisiasa wanaotumia vibaya uhuru wa kidemokrasia kuhatarisha hali ya amani ya nchi.

Kimewataka viongozi wa siasa wa chama cha ACT-Wazalendo na CUF kutotumia mipasuko na migogoro ya ndani ya vyama vyao kuhatarisha hali hiyo ya amani na kwamba wazanzibar na Watanzania hawapo tayari kuingia katika machafuko ya kisiasa kwa sababu ya maslahi binafsi ya watu wachache.

Onyo hilo limetolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Sadala 'Mabodi',wakati akizungumza katika Kikao cha ndani kilichoambatana na hafla ya kukabidhi gari la aina ya basi kwa uongozi wa Jimbo la Magomeni mjini Unguja lililotolewa na Mbunge wa Jimbo hilo Jamal Kassim Ali.

Naibu Katibu Mkuu huyo amesema CCM haina muda wa kushughulikia sera za vyama vingine na kwamba itaendelea kusimama imara na kupaza sauti inapoona baadhi ya watu wachache wanavunja sheria za nchi kwa makusudi bila ya kujali misingi ya utu na haki za binadamu.

Ameongeza kuwa mpasuko wa kisiasa ulioko baina ya viongozi wa CUF na ACT-Wazalendo baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF,Seif Sharif Hamadi kufukuzwa ndani ya chama hicho na kujiunga na ACT-Wazalendo ambapo imeshuhudiwa namna wa wafuasi wa Chama cha ACT-Wazalendo wakifanya vitendo vya uvunjifu wa sheria kwa makusudi.

Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa wanachama wa ATC-Wazalendo wamefanya uharibifu wa mali za chama cha CUF ikiwemo kuchoma nguo za chama hicho,bendera, kung'oa samani zilizoko katika Ofisi mbali mbali sambamba na kutumia dini katika harakati za Chama hicho.

Naibu Katibu Mkuu huyo amesema mambo yote hayo ni ishara za wazi zinazochochea vurugu na migogoro baina ya wanachama wa vyama hivyo viwili, zinazoweza kuingiza nchi katika athari kubwa ya machafuko.

Hata hivyo,Dk.Mabodi amevitaka  vyombo vya ulinzi na usalama nchini kuchukua hatua stahiki mapema, kwani dhana ya hali ya amani na utulivu wa nchi haviuzwi katika maduka kama bidhaa bali imeletwa na sera bora za CCM.

Amesema nchi zilizoingia katika machafuko ya kisiasa na vita vya wenyewe kwa wenyewe zilianza taratibu huku Taasisi na Mamlaka zenye dhamana ya ulinzi na usalama zikipuuza kuchukua hatua katika hali hizo na badala yake mataifa hayo yamejikuta yakingia katika vita hivyo kwa kipindi cha muda mrefu.

Naibu huyo Katibu Mkuu aliongeza kuwa CCM itaendelea kushindana kwa sera za maendeleo na kuwapelekea wananchi mahitaji muhimu ya msingi na si kujiingiza katika siasa za ubabe na uharibifu wa mali za umma.

"Wito wangu kwa viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa nchini tuwaongoze na kuwaelekeza mambo mema wanachama wetu, kwa kuwajengea mazingira ya kuamini ushindani wa sera na badala ya Siasa za Ovyo na machafuko", amesema Naibu Katibu Mkuu.

Katika maelezo yake Dk.Mabodi amemsihi Msajili wa Vyama vya siasa nchini, kuchukua hatua za haraka za kuhakikisha Chama kinachovunja Sheria na Katiba za nchi na ambavyo vikienda kinyume na masharti ya usajili wa Vyama vya Siasa wachukuliwe hatua za kisheria.

Pia, amemtaka Msajili huyo wa vyama vya siasa kuwa anatakiwa kufanya uhakiki wa michango ya fedha za wahanga wa mafuriko Zanzibar zilizokuwa zikichangishwa na viongozi wa CUF chini ya Seif Sharif Hamad na kutolewa ufafanuzi wa kina juu ya matumizi yake kama ziliwafikia walengwa.

Amesema kwamba kuna baadhi ya vyama vya siasa nchini vinajiendesha kupitia mifumo haramu ya ufisadi, utapeli na migogoro kwa lengo la kukidhi maslahi ya watu wachache ambao ni viongozi wa ngazi za juu za vyama hivyo.

Dk.Mabodi amesema vyama vya aina hiyo havitakiwi kupewa nafasi wala kuaminiwa na wananchi kwani haviwezi kuwakilisha na kusimamia maslahi ya wanachama wao badala yake wanajinufaisha wenyewe.

Naibu Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kupuuza kauli za Seif Sharif Hamad za kudai kuwa migogoro ya vyama vyao inachochewa na Serikali jambo ambalo si kweli bali anaendeleza ulaghai na Siasa za fitna.

"Niwaweke wazi kwamba mfumo wa siasa za ujamaa na Kujitegemea ndio chimbuko la maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kwani, unawawezesha wananchi kujikomboa katika hali ya umaskini uliokithiri na kuwa katika hali ya maendeleo na kujitegemea wenyewe kiuchumi na kijamii,"amesema Dk.Mabodi 

Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM, aliwapongeza Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wa Jimbo la Magomeni Unguja kwa kasi kubwa ya kutatua kero za wananchi ndani ya Jimbo hilo na maeneo yake.

Dk.Mabodi amesema kuwa kibali cha kuirejesha CCM madarani mwaka 2020 ni kutekeleza ahadi zote zilizoahidiwa katika uchaguzi wa mwaka 2015 na kwamba kila kiongozi wa Serikali na Chama anayejua kuwa amepewa dhamana ya kutimiza dhamira hiyo wanapaswa kutekeleza kwa wakati ahadi hizo.

Amewataka baadhi ya Wabunge,Wawakilishi ambao wanashindwa kutekeleza vyema ilani ya uchaguzi wanapaswa kutambua kuwa CCM haitokuwa haibu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kwamba itatoa fursa kwa watu wanaotekeleza ilani na miongozi ya CCM kwa vitendo.

"Leo tunakumbushana tu kuwa wananchi wanahitaji maendeleo sio porojo hivyo kama wewe unajijua upo Serikali au katika Chama na tulikupa dhamana ya kuwatumikia wananchi na hukutekeleza dhamana hiyo, basi ujue kuwa utang'oka utake usitake.", amesema.  

Dk.Mabodi ametoa agizo kwa viongozi wa majimbo nchini wakiwemo Wabunge na wawakilishi kufanya mikutano ya ndani ya kuwaeleza wana-CCM na wananchi kwa ujumla utekelezaji wa ilani unaofanywa na Serikali ili waone mafanikio yaliyofikiwa katika nyanja za kijamii,kichumi na kisiasa.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Magomeni,Jamal Kassim Ali, amesema basi hilo limegharimu sh.milioni 29.5 ni miongoni mwa sehemu ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa kuwaondoshea kero za usafiri wananchi wa jimbo hilo.

Amesema kwa kipindi cha miaka mitatu ametatua kero za ukosefu wa maji safi na salama kwa kuchimba visiwa tisa ambavyo vinatoa huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya Shehia zote za Jimbo hilo. 

Mbunge huyo ameongeza kuwa kwa kushirikiana na Mwakilishi wa Jimbo hilo wameanzisha kituo cha mafunzo ya amali kinachotoa mafunzo ya ujasiriamali na ufundi kwa vijana wa jimbo hilo.

Amesema sakata la Seif Sharif Hamad kufukuzwa ndani ya CUF, inatokana na dhambi zinazomtafuna za usaliti,uchu wa madaraka pamoja na visasi na chuki.

"Kwani alidai kusema kuwa yeye anaongoza mapambano ndani ya CUF inayofuata falsafa za mfumo wa Kiliberali ili kuin'goa CCM inayofuata mfumo wa Kijamaa aliodai umepitwa na wakati,"ameeleza. 

Jamal amesema kuwa anashangaa kumuona kiongozi huyo aliyetamba kwa mbwembwe na kukashifu mfumo wa ujamaa anajiunga na ACT-Wazalendo kinachofuata mfumo huo wa ujamaa.

"Mimi nawambia wananchi hasa ambao bado ni mateka wa kifkra kwa Seif kuwa waamke na kujikomboa na utumwa wa mwanasiasa huyo wajiunge na CCM kwani hajali maisha ya watu bali anajali maslahi yake."amesema Jamal.

Naye Mwakilishi wa Jimbo hilo,Rashid Makame Shamsi amesema kuwa ameshiriki katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya jimbo kwa kununua vifaa vya samani vya ofisi na kukarabati Ofisi za Makatibu wa matawi ya chama yalioko katika Jimbo hilo.  

Amesema katika kutatua changamoto ya usafiri siku za hivi karibuni amenunua gari aina ya Fuso kwa ajili ya shughuli mbalimbali za wananchi wa jimbo hilo na kwamba amechimba visima na kusambaza mipira ya maji.

Mwakilishi huyo amesema kuna ushirikiano mkubwa kati yake viongozi wenzake wakiwemo Mbunge na Madiwani wa Jimbo hilo katika shughuli mbalimbali za maendeleo ili kumaliza changamoto za wananchi wa jimbo hilo. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni