Jumamosi, 30 Machi 2019

MHE.RAMADHAN: ATAKA USAFI WA MAZINGIRA UPEWE KIPAUMBELE JANG'OMBE, MHE.SAID ATAJA MIKAKATI YA MANISPAA YA MJINI.

 MKURUGENZI wa Manispaa ya Mjini Unguja (wa tatu kutoka kushoto),Mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe Mhe.Ramadhani Hamza Chande(wa Nne kutoka kusho),Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Talib Ali Talib(wa pili kutoka kushoto), Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mjini Kamaria Nassor (wa kwanza kushoto) wakikabidhi mfuko wa Sabuni ya kufulia nguo na vifaa vya usafi Katibu wa Hospitali ya Kidongo Chekundu Bi.Bhai Ibrahim mara baada ya kukamilika zoezi la usafi wa mazingira.

 VIONGOZI wa UVCCM Wilaya ya Mjini wakifanya Usafi katika Chumba cha Wagonjwa Wanawake wenye matatizo ya Akili katika Hospitali ya Kidongo Chekundu.

 VIONGOZI mbali mbali wa CCM,UVCCM na Baraza la Manispaa wakifanya usafi katika Jengo la kupumzikia Wagonjwa wa kiume wa matatizo ya Akili  katika Hospitali ya Kidongo Chekundu.
 VIJANA wa UVCCM wakifanya usafi wa mazingira katika Hospitali ya Wagonjwa wa Akili Kidongo Chekundu Zanzibar.


NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

WANANCHI wa Jimbo la Jang’ombe wametakiwa kufanya Usafi wa Mazingira mara kwa mara ili kuepuka madhara yanayosababishwa na uchafu yakiwemo maradhi ya miripuko.

Rai hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe Zanzibar Mhe.Ramadhan Hamza Chande katika shughuli ya kufanya usafi katika Hospitali ya Matibabu ya Wagonjwa wa Akili ya  Kidongo Chekundu Zanzibar.

Amesema kila mwananchi ana jukumu la kufanya usafi katika mazingira anayoishi kwa kuhakikisha yanakuwa safi muda wote kwa lengo la kuepuka maradhi yakiwemo kipundupindu,kichocho na malaria.

Ameeleza kuwa  lengo la kufanya usafi katika eneo hilo la hospitali ni kutoa msaada wa kijamii wa kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum ambao ni wagonjwa wa akili wanaohitaji huduma muhimu za kijamii zikiwemo zikiwemo kuishi katika mazingira safi.

Ameongeza kuwa zoezi hilo la usafi ni sehemu ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 iliyoainisha utekelezwaji wa mambo mbali mbali katika sekta ya Afya ikiwemo usafi na ulinzi wa mazingira.

Katika maelezo yake Mwakilishi huyo Ramadhan, amebainisha kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu na kutekelezwa kwa hatua mbili ambazo hatua ya kwanza ni kutoa elimu kwa jamii na hatua ya pili ni kuhamasisha wananchi wafanye usafi kwa hiari.

“Naomba wananchi watambue na kuamini kuwa ‘usafi’ ni tabia hivyo tubnatakiwa kuweka safi mazingira yetu na yale wanayoishi watu wenye mahitaji maalum ili nao waishi kwa amani,utulivu na usalama wa afya zao kama wanavyoishi watu wengine.”,amesema Chande.

Ameshauri Serikali kupitia Baraza la Manispaa ya Mjini kuhakikisha wanasimamia Sheria ndogo ndogo za ulinzi wa usafi wa mazingira ili watu wanaochafua mazingira watozwe faini za papo kwa papo kwa lengo la kubadilisha jamii kitabia kutambua umuhimu wa kulinda mazingira.

Ametaja  mikakati ya Jimbo la Jang’ombe katika kusimamia suala la usafi alifafanua kuwa wana mipango ya kuanzisha mashindano ya kuimarisha usafi katika shehia zote za jimbo hilo kwa kila shehia kuipatia zawadi ili kuhamasisha jamii kusafisha mazingira wanayoishi.

Akizungumza katika zoezi hilo Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa ya Mjini Mhe.Said Juma Ahmada, amesema Baraza hilo linasimamia shughuli za usafi katika maeneo mbali mbali ili kuhakikisha Mji unakuwa Safi na unaoendana na hadhi ya Zanzibar.

Amewambia wananchi hao kuwa wanatakiwa kuheshimu sharia za Manispaa kwa kuhakikisha maeneo ya mjini yanakuwa safi muda wote ili kurejesha sifa ya Zanzibar ya kuwa mjini safi na wenye watu wastaarabu katika kulinda na kutunza mazingira yaliyowazunguka.

Amesema lengo la Manispaa hiyo ni kufikia kiwango cha Mji wa Zanzibar kutajwa katika miji Safi, Kimataifa, Kikanda na Kitaifa kama inavyotajwa miji baasdhi ya Miji ya Tanzania bara fano Arusha na Mwanza.

Amesema kupitia mipango endelevu iliyowekwa na Manispaa hiyo mji wa Zanzibar utakuwa miongoni mwa orodha ya miji safi Duniani kwani baadhi ya maeneo wananchi wameanza kuelimika.

Katika maelezo yake Mkurugenzi huyo, amesema Baraza hilo linaendelea kutekeleza kwa ufanisi Ilani ya CCM kwa kuviwezesha vikundi mbali mbali vya kijamii vinavyofanya shughuli za usafi wa mazingira kwa kuvipatia misaada mbali mbali ya vifaa ikiwa ni sehemu ya kurejesha faida ya mapato yanayokusanywa na Manispaa kwa jamii.

“Nawapongeza sana UVCCM na CCM  Jimbo la Jang’ombe kwa ubunifu wao wa kufanya usafi katika maeneo haya ya Hospitali ambayo ni sehemu muhimu kijamii kwani watu wanaoletwa kupatiwa matibabu katika maeneo haya wanatoka katika jamii zetu."amesema Said.

Aidha ametoa wito kwa Vijana mbali mbali katika Manispaa hiyo kuanzisha Vikundi rasmi vya usafi wa mazingira ili wapewe nyenzo za usafi na wanufaike na miradi ya usafi inayoratibiwa na Taasisi hiyo ili kuepuka kujiunga na vikundi viovu vinavyopelekea kuharibu maisha yao.

Amesema wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari kubwa ya kuweka mazingira katika hali ya usafi hasa katika kipindi hichi cha mvua za masika ambacho,hujitokeza maradhi mengi yanayotokana na uchafu pamoja na kufanya usafi katika mitaro ya kusafirisha maji taka.

Katibu wa Siasa na Uenezi CCM Jimbo la Jang’ombe, Ali Ahmad Ibrahim ‘Abeid’, amesema licha ya Chama Cha Mapinduzi kuwa Taasisi y Kisiasa kimeendelea kuwa mdau mkubwa wa kushiriki,kulinda,kutetea na kutoa miongozo ya uhamasishaji wa jamii kujenga utamaduni wa wananchi kuweka mazingira wanayoishi katika hali ya usafi.

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mjini, Kamaria Suleiman Nassor alisema suala la usafi halina itikadi za kisiasa bali linawahusu wananchi wote hivyo ni muhimu vijana wote kuungana na kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kwa kuhakikisha mazingira wanayoishi yanabaki salama.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Mjini, Hudhaima Mbarouk Tahir amewashukru vijana na wadau mbali mbali walioshiriki katika zoezi hilo la usafi, kueleza kuwa huo ni mwanzo wa maandalizi ya shughuli za kijamii za Umoja huo katika Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Majimbo yote ya Wilaya hiyo.

Kwa upande wake Katibu wa UVCCM wa Jimbo hilo,Zainab Hassan King amesema jimbo hilo limejipanga kufanya shughuli mbali mbali za kimaendeleo zitakazoisaidia jamii zikiwemo masuala ya usafi.

Naye Katibu wa Hospitali ya Kidongo Chekundu, Bhai Ibrahim amewashukru wadau walioshiriki zoezi la usafi pamoja na kutoa msaada wa vifaaa vya usafi na kueleza kuwa wamesaidia kuweka katika hali ya usafi mazingira ya hospitali hiyo.

Zoezi hilo la usafi limetekelezwa na UVCCM na CCM Jimbo la Jang’ombe kwa kushirikiana na Baraza la Manispaa ya Mjini ambao wametoa mchango wa Vifaa mbali mbali vya Usafi katika Hospitali hiyo.Hakuna maoni:

Chapisha Maoni