Jumapili, 31 Machi 2019

MANISPAA YA MAGHARIB 'B' YAAHIDI NEEMA KWA VIJANA, YASIFU UZALENDO WA UVCCM JIMBO LA M/KWEREKWE.


MKURUGENZI wa Baraza la Manispaa ya Magharib ‘B’ ndugu Ali Abdallah Said Natepe akizungumza mbele ya Vijana wa UVCCM mara baada ya kukamilisha zoezi la Usafi wa mazingira katika soko la Mwanakwerekwe.



NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR

VIJANA nchini wameshauriwa kuanzisha vikundi vya usafi wa mazingira ili wanufaike na fursa zilizowazunguka katika mazingira wanayoishi zikiwemo kujiajiri wenyewe kupitia vikundi hivyo.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa ya Magharibi 'B' Ali Abdalla Said Natepe mara baada ya kukamilika zoezi la Usafi katika soko la Mwanakwerekwe Zanzibar.

Amesema kuwa vijana wengi wamekuwa wakilalamikia changamoto ya ukosefu wa ajira hali ya kuwa bado hawajatumia vizuri fursa za ajira hasa zile zilizowazunguja zikiwemo za kufanya usafi na masuala mbali mbali ya ujasiriamali.

Amesema Manispaa ya Magharibi 'B' ipo tayari kufanya kazi na vijana kwa kuwapatia nyenzo za kufanyia kazi zikiwemo vifaa vya usafi pamoja na ruzuku ndogo ya kujikimu ili washiriki katika harakati mbali mbali za kusafisha maeneo mbali mbali ya manispaa hiyo.

Amebainisha kuwa endapo vijana hao wa UVCCM wataunda vikundi rasmi vinavyotambulikana kisheria uongozi wa Manispaa hiyo utahakikisha unawapa ushirikiano kwani kundi la vijana ndio nguvu kazi ya Taifa.

Katika maelezo yake Mkurugenzi huyo Natepe, ameeleza kuwa dhana ya vijana kujiajiri wenyewe kupitia vikundi vya usafi imeasisiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mhe.Ayoub Mohamed Mahmoud anayeagiza vijana waunde vikundi kisha wapewe nyenzo za kufanyia kazi, lakini bado muamko wa kundi hilo ni mdogo na hauridhishi.

Mkurugenzi huyo, amewashukru wadau mbali mbali wakiwemo wanachana na viongozi wa UVCCM na CCM kwa kushiriki katika zoezi muhimu la ujenzi wa taifa la kufanya usafi katika soko la Mwanakwerekwe sehemu inayotumiwa na wananchi wote kutafuta riziki zao za kujikimu kimaisha.

Ametoa wito kwa wananchi kufanya usafi wa kina katika maeneo wanayoishi kwani mvua za masika zimeanza kunyesha hali inayotakiwa jamii kuchukua tahadhari juu ya maisha yao hasa katika suala zima la kutunza mazingira.

Akitoa salamu za Chama cha Mapinduzi Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ased Nyonje, amesema CCM itaendelea kuwa Taasisi bora ya kisiasa kwani wanachama wake wakikuwa wakitekeleza kwa vitendo falsafa ya ujamaa na kujitegemea kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii.

Amewataka vijana kufanya kazi kwa juhudi kubwa hasa kushiriki katika matukio muhimu ya ujenzi wa Taifa ili CCM iendelee kuaminiwa na jamii hatimaye ifikapo mwaka 2020 wananchi waichague kwa kura nyingi CCM ibaki madarakani.

Naye Mjumbe wa Baraza Kuu UVCCM Taifa kupitia Mkoa wa Magharib kichama Kassim  Hassan Haji, ameeleza kuwa vijana wa UVCCM wamekuwa mstari wa mbele katika kushiriki katika masuala mbali ya kijamii kwa nia ya kuwasaidia wananchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Jimbo la Mwanakwerekwe Fatma Ramadhan Hussein amesema zoezi hilo la usafi ni sehemu ya kampeni ya kizalendo ya AMSHA AMSHA inayoratibiwa na Vijana wa Jimbo hilo kwa lengo la kuwahamasisha vijana wenzao na jamii kwa ujumla kushiriki katika masuala ya ujenzi wa Taifa.

Akizungumza Mjumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi Taifa, Zahoro Saleh amesema usafi ni jambo muhimu katika maisha ya mwanadamu hivyo wananchi wanatakiwa kutekeleza zoezi hilo katika maeneo yao bila ya kushurutishwa.

Ameeleza kuwa kutokana na umuhimu wa usafi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amekuwa akihimiza jamii ijenge utamaduni wa kuweka mazingira ya nchi katika hali ya usafi hadi serikali ikaamua kutenga siku za kila mwisho wa mwezi kufanyika usafi nchi nzima.

Fatma   a meongeza kuwa kampeni hiyo inaambata na upandishaji wa Bendera za CCM katika maskani na maeneo mbali ya Mabalozi wa CCM,kuzindua madarasa ya Itikadi, kuwatembelea wazee na watu wenye mahitaji maalum sambamba na kupokea wanachama wapya wenye nia ya kujiunga na CCM pamoja na Jumuiya zake ili wanufaike na Siasa zenye Tija.

Naye mshiriki katika zoezi hilo Jamila Hamza  amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele kufanya usafi katika mazingira wanayoishi kwani ni wadau muhimu wa maendeleo ya kijamii.

Aidha amesema suala la usafi ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwani ni sehemu muhimu ya masuala ya Afya ya jamii.




Maoni 3 :

  1. Uvccm oyeeeee
    Vjina wa mwanakwerekwe tunasema "tumethubutu na tumeweza na bado tutasonga mbele mbele zaid"

    JibuFuta
  2. Maoni haya yameondolewa na mwandishi.

    JibuFuta
  3. CCM mbele kwa mbele oyeee

    JibuFuta