Jumatano, 27 Machi 2019

MHE.NDUGAI: AANZA ZIARA YAKE MKOA KASKAZINI UNGUJA,ATAKA USHINDI WA MAJIMBO YOTE 2020.

 MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja  Mhe.Job Ndugai akiwahutubia Wanachama na Viongozi wa Mkoa huo katika ziara yake ya kujitambulisha katika Mkoa. 


 NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

MLEZI wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kichama ndugu Job Ndugai, amewataka Wana CCM wa Mkoa huo kutambua kuwa njia pekee ya kulinda Mapinduzi ya mwaka 1964 ni kuhakikisha CCM inashinda na kubaki madarakani kwa kila Uchaguzi wa Dola.

Amesema kila mwanachama atumie nafasi yake kuhakikisha CCM inaendelea kustawi kisiasa, kiuchumi na kijamii na kukubalika kwa wananchi wote.

Kauli hiyo ameitoa katika ziara yake ya kujitambulisha na kuimarisha Chama katika Mkoa huo anaoulea akiwa ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa.

Amesema  suala la ushindi wa CCM sio mzaha bali ni jambo linalotakiwa kupewa kipaumbele kwa lengo la kulinda heshima,hadhi na urithi uliotukuka wa Waasisi wa Muungano na Mapinduzi ya mwaka 1964.

Ameeleza kitendo cha CCM kukosa jimbo moja la uchaguzi ni sawa na kusaliti juhudi za viongozi waliokomboa nchi kutoka kwenye kiza cha ukoloni,utumwa,udhalilishaji na kuiweka katika mwaka wa maendeleo,mafanikio chini ya falsafa ya ujamaa na kujitegemea.

Amewataka viongozi waliopewa dhamana na CCM katika Mkoa huo wafanye kazi kwa bidii na kuufuta upinzani ndani ya eneo hilo ambalo ni ngome ya CCM.  

Ndugai ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,amesema hatokuwa tayari kufanya kazi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wa mkoa huo ambao watakuwa wazembe katika ulezi wake.

Amesisitiza kuwa katika ulezi wake hatoweza kukubali kufanya kazi na wanachama hao na kwamba atakuwa mkali zaidi.

Mlezi huyo amesema  kuna baadhi ya watu hao wamekuwa wakibebwa huku wakishindwa kufanya kazi ipasavyo ya kuisaidia chama na hatimaye kusababisha kuangusha utendaji wa CCM katika maeneo ya mkoa huo.

Amesema katika nafasi yake ya kuwa mlezi atahakikisha anaendelea kuimarisha mkoa huo wa Kaskazini kuwa ngome ya CCM ili kushika nafasi za ngazi za udiwani,ubunge na uwakilisha.

Amefafanua kuwa kwa upande wa Wabunge na Wawakilishi ambao wanatoka katika maeneo ya mkoa huo wanapaswa kutekeleza hadi za utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa CCM na kwamba kufanya hivyo ndio njia pekee ya kuirejesha CCM madarakani.

Spika Ndugai amesema hata hivyo jukumu la utekelezaji wa hadi ya ilani ya uchaguzi linahitaji ushirikiano wa karibu na wanachama pamoja na kamati za wajumbe wa CCM kupitia Baraza la Wawakilishi na kamati za wajumbe wa CCM kupitia Bunge.

Amesema historia ya Zanzibar itakuwa na manufaa kwa vizazi vijavyo endapo watu viongozi wa sasa watafanya mambo ya maendeleo yenye kuacha alama bora ya uongozi wenye tija.

Katika maelezo yake,Ndugai amewasihi Wazazi na walezi wa Mkoa huo kujenga utamaduni ya kuwaruhusu vijana wao wachangamkie fursa mbali mbali za kimaendeleo zilizopo katika maeneo mbali mbali ya Tanzania bara na Afrika mashariki.

Amewataka baadhi ya viongozi na wanachama ambao bado wanaendekeza makundi yasiyofaa ya kukigawa chama waache tabia hiyo na badala yake washikamane kuleta maendeleo endelevu ndani ya taasisi hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Mkoa huo Iddi Ali Ame amesema kaskazini ni ngome ya CCM na kwamba watahakikisha hawapotezi jimbo hilo kuanzia ngazi ya udiwani,Uwakilishi hadi Ubunge.

Amewataka wanachama wa Mkoa huo wanapaswa kuwa mstari wa mbele  kwa kukijenga chama na kwamba kuna mambo mengi yameaidiwa katika kutatua kero mbalimbali za wananchi.

"Bado tunasafari ndefu tunatakiwa tukiimarishe chama kwa vitendo katika kutatua kero za wananchi na mambo tulioyahaidi katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015,"alisema



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni