MWENYEKITI wa UWT Taifa Ndugu Gaudensia Kabaka akikagua bidhaa zilizotengenezwa na wajasiriamali wa Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja. |
MWENYEKITI wa UWT Taifa Ndugu Gaudensia Kabaka akimkabidhi kadi mwanachama mpya wa UWT. |
WANACHAMA wapya wa CCM na UWT wakila kiapo cha Uanachama mara baada ya kukabidhiwa kadi hizo katika Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja. |
MWENYEKITI wa UWT Taifa Ndugu Gaudensia Kabaka akizungumza na Wanachama wa CCM katika ziara yake Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja. |
WANACHAMA na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya ya U.W.T wakisikiliza kwa makini nasaha za mgeni rasmi Ndugu Gaudensia Kabaka alipokuwa akihutubia Wilayani humo. |
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
WANACHAMA, Viongozi na Watendaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameshauriwa kudumisha umoja na mshikamano katika kusimamia maslahi ya CCM kwa kila ngazi ya kiutendaji na kiuongozi.
Ushauri huo ametolewa na Mwenyekiti wa UWT Taifa Ndugu Gaudensia Kabaka katika ziara yake Wilaya ya Kaskazini 'A' Mkoa wa Kaskazini Unguja katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Mwaka 2015/2020 Wilaya humo.
Amesema endapo wanachama hao watashirikiana kwa kila jambo na kufuata miongozo ya Kikatiba na Kikanuni iliyowekwa na CCM, hatua hiyo itasaidia kupunguza Changamoto za kisiasa ndani ya Wilaya hiyo.
Ameeleza ushirikiano ndio chimbuko la maendeleo ya taasisi yoyote hivyo wanachama wa mkoa huo wanatakiwa kudumisha tunu hiyo ili kuimarisha maendeleo ndani ya CCM.
Ndugu Kabaka, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetatua shida na kero za wananchi kwa kiwango kikubwa kupitia mambo mbali mbali yaliyorajwa katika muongozo wa Ilani ya Uchaguzi.
Amesema Serikali ya Zanzibar wananchi wamejengewa Vituo vya Afya na Hospitali za Kisasa katika maeneo mbali mbali nchini, hatua inayopunguza usumbufu kwa akina mama juu ya upatikanaji wa huduma bora za Afya.
Amesema Dk.Shein amekuwa ni kiongozi bora anayejali wanawake kwani katika kipindi cha uongozi wake wanawake wameteuliwa kushika nafasi za juu za kiuongozi.
Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo ameongeza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein imetekeleza kwa ufanisi mambo mbali mbali ya kimaendeleo,kiuchumi na kisiasa zaidi ya asilimia 95.
Akizungumzia dhana ya Siasa na Uchumi ndani ya CCM, Mwenyekiti huyo alisema taasisi hiyo imefanikiwa kuweka nidhamu ya fedha kwa kuweka utaratibu maalum wa matumizi ya fedha kwa kila ngazi ndani ya Jumuiya na CCM kwa ujumla.
Ameongeza kwamba utaratibu huo utasaidia CCM kuendelea kuimarika kiuchumi kwani vyanzo vyake vya fedha na miradi ya maendeleo itatumika kwa utaratibu unaotambulikana katika masuala ya usimamizi wa fedha.
Ametoa tahadhari juu ya baadhi ya Wana CCM wanaoendeleza makundi tasiyofaa ya uchaguzi uliopita ambayo kwa sasa hayana tena nafasi kwani CCM inajipanga na uchaguzi wa mwaka 2020.
Akizungumza Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa Ndugu Thuwaiba Kisasi,aliwasihi Akina Mama wa Umoja huo katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kuhakikisha wanafuta upinzani kwa kuiwezesha CCM ishinde katika majimbo yote ya Mkoa huo mwaka 2020.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa UWT Taifa Mwl. Queen Mlozi, amesisitiza umuhimu wa jamii kulinda haki za msingi za watoto wa kike kwani wamekuwa wakikatishwa masomo yao bila sababu za msingi jambo ambalo ni hatari kwa kaendeleo yao na jamii kwa ujumla.
Mwl. Queen amewataka wazazi na walezi kutofumbia macho ndoa za u mdogo pamoja na mimba za utotoni kwani tabia hizo zisipothibitiwa zinakuwa ni miongoni mwa vikwazo vya kuharibu maisha ya watoto wa kike.
Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Ndugu Tunu Juma Kondo amesema Umoja huo umekuwa karibu zaidi na wananchi wa makundi yote kwa lengo la kudumisha umoja na mshikamano.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa UWT anayefanyia kazi zake Tanzania bara Ndugu Jesca Mbogo, amewataka Wananchi wa Wilaya hiyo kuchukia tabia za udhalilishaji wa kijinsia kwa Wanawake na Watoto kwani vitendo hivyo vinaacha maumivu na mateso ya kudumu kwa watu waofanyiwa uhalifu huo.
Amesema ni wakati mwafaka Akina Mama wa UWT katika Wilaya hiyo kushikamana na kulaani vikali vitendo vya hivyo kwa kuhakikisha vinaripotiwa katika vyombo vya kisheria na kufuatilia mwenendo wa kesi hizo ili zitolewe hukumu stahiki.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa Kaskazini Unguja Ndugu Mariam Muharami Shomari alisema Umoja huo umejipanga vyema katika kuelimisha wanawake na vikundi vya vijana ili wajiunge na CCM sambamba na kupiga kura ili Chama kishinde kwa kura nyingi katika uchaguzi Mkuu ujao.
Akisoma Risala ya Wilaya hiyo Katibu wa UWT Ndugu Ine Ame Machano, ameelezan kuwa Umoja huo umekufanya ziara mbali mbali za kuhamasisha wanawake wajiunge na CCM na Jumuiya hiyo sambamba na kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi mbali mbali vya Wilaya hiyo.
Jumla ya Wanachama wapya 600 wamekabidhiwa kadi za CCM na UWT katika Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni