Jumatano, 10 Juni 2020

VIJANA JITOKEZENI KWA WINGI MAJIBONI




JUMUIYA ya Vijana ya Chama cha Mapinduzi(UVCCM),Zanzibar imewataka wanachama wa jumuiya hiyo kujitokeza kwa wingi majimboni katika kugombea nafasi mbambali za Uwakilishi na Ubunge wakati ukifika wa uchaguzi na kwamba wasijikite kwenye nafasi za viti maalum.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Gymkhana mjini Unguja Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM, Mussa Hassan Mussa ambapo alisema wasijikite zaidi kwenye kugombea nafasi za vitimaalum katika mikoa mbalimbali kama ilivyokawaida ya utaratibu wa jumuiya hiyo.

Naibu Katibu Mkuu huyo aliwataka vijana wajumuiya hiyo kutambua kuwa wana nafasi nyingi kwenye kugombea katika nafasi za vitimaalum katika jumuiya za Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) na Jumuiya ya Wazazi ya CCM.

"Kikubwa zaidi nitafarajika zaidi kuona vijana wanajitokeza kwa wingi kwenda kugombania nafasi za majimbo nafasi za Uwakilishi na Ubunge lakini pia nafasi za udiwani kutokana na kuwa hizi nafasi hazina watu maalum ni za watu wote,"alisema

Katika maelezo yake alisema kila mwanachama wa jumuiya ana haki ya kugombea nafasi hizo na kwamba wakati utakapofika vijana wakachukue fomu za kugombea.

"Na sisi tukiwa kama viongozi wenu tutahakikisha tunasimama imara kuhakikisha nafasi hizo vijana wanazipata ili ndani ya vyombo vya dola kuna kuwa na mabadiliko chanya kwa taifa letu kupitia vijana,"alisema

Aliongeza kuwa intambulika kuwa hakuna kiongozi bora atakayepatikana kama hajapitia kwenye tanuri la UVCCM na kwamba jumuiya hiyo ndio inayoandaa vijana wa kesho na wa siku zijazo.

"Kijana yeyote wa UVCCM hasisite kujitokeza wakati ukifika kwa kufikiri kuwa hana msaada wowote wa UVCCM na kwamba vijana wanatakiwa kutambua kuwa sisi viongozi wao tuko tayari kupambana mpaka wanapata nafasi hizo ili mradi wafuate sifa na utaratibu ambao CCM imeuweka,"alisema

Alisema endapo vijana wakienda kinyume na utaratibu ambao CCM umeuweka ikiwemo kuanza mapema kampeni na kujikita kwenye vitendo vya rushwa na kwamba viongozi wa UVCCM  watahakikisha wanasimamia jina la watu hao kutopita.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema Vijana wanapaswa kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za majimbo wakati ukifika na jambo lingine wanapaswa kufuata utaratibu ambao CCM watautoa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni