Jumatatu, 15 Juni 2020

MAKADA WAWILI WA CCM WAFUNGUA MILANGO ZA KUCHUKUA FOMU YA URAIS ZANZIBAR


MAKADA wa wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliojitokeza leo  katika ofisi Kuu za Chama zilizopo Kisiwandui mjini Unguja kuchukua fomu za kuomba kupewa ridhaa na Chama kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar.

Waliojitokeza miongoni mwa makada hao katika kuchukua fomu hizo ni Waziri wa Vijana, Utamaduni,Sanaa na Michezo Balozi Ali Abeid Karume pamoja na Mbwana Bakari Juma.

Juma ni moja wa kada hao aliyekuwa wa kwanza kufungua pazia la uchukuaji wa fomu kwa Katibu wa Idara ya Organizesheni CCM Zanzibar, Cassian Galos Nyimbo katika ofisi za CCM Kisiwandui Zanzibar.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo Juma amesema endapo CCM ikimpatia ridhaa ya kugombea nafasi hiyo ya urais amejitathimini, ametafakari kwa kina kutokana na kuwa urais si kazi rahisi ni ngumu.

Juma amesema urahisi ni kazi ngumu na kwamba inahitaji msaada mkubwa kutoka kwa mwenyezi Mungu hata hivyo kazi hiyo inahitaji uadilifu,unyenyekevu na moyo wa kujitolea.

Katika maelezo yake kada huyo amesema amekaa na kutafakari kwa kina kuwa ikitokea chama kitaridhia kusimamisha kuwa mgombea pekee wa kiti cha urais kupitia CCM na wananchi wa Zanzibar wakamchagua kuwa rais wa Zanzibar ataangalia maslahi mapana ya Tanzania.

Amesema kwa upande wa Zanzibar ataanzia atakapoishia Rais Dk.Ali Mohamed Shein ambapo kiongozi huyo amefanya kazi vizuri ikiwemo kuwaunganisha wanzanzibar pamoja na kujenga umoja wa Tanzania.

Juma aliongeza kuwa Rais Dk.Shein ametekeleza ilani ya uchaguzi wa CCM kwa asilimia 100 ama zaidi na kwamba iwapo ikitokea chama kikampa ridhaa na wananchi wakamchagua kuwa rais atafanya mambo mengi yatakayoendelea  kuipaisha Zanzibar kiuchumi. 

Amesema atahakikisha anashirikiana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maslahi ya wananchi wote wa pande mbili za Muungano.

Amesema atapiga vita umaskini,maradhi na ujinga ili wananchi wawe na maisha mazuri na kwamba nia yake ni kuwasaidia wanzanzibar.  

ilipofika majira ya saa nane mchana Waziri wa Vijana, Utamaduni,Sanaa na Michezo Balozi Ali Abeid Karume amewasili katika ofisi za CCM kuchukua fomu hizo za kuomba ridhaa kugombea nafasi ya urais.

Baada ya kuchukua fomu Waziri Karume alidhuru kaburi la Mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar  Marehemu Abeid Amani Karume ambaye ndiye Rais wa kwanza wa serikali ya Mapinduzi na badala ya hapo alizungumza na waandishi wa habari.

Akizungumza na waandishi wa habari Waziri Karume amesema iwapo atapewa ridhaa na CCM na kupata ridhaa ya wananchi anatarajia kuendeleza dhamira ya mapinduzi ya Zanzibar kwa kuyalinda,kulinda muungano na kuendeleza sera za Chama.

Amesema atahakikisha anaendeleza mazuri yaliyofanyika nchini yakiwemo afya bure,elimu bure,ugawaji wa ardhi kwa wananchi na ujenzi wa mkaazi bora na kwamba Rais Dk.Ali Mohamed Shein akishirikiana na Baraza la Mapinduzi amefanya kazi ya kupigiwa mfano katika kuendeleza sera zilizoainishwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

 Waziri huyo amesema iwapo atapata ridhaa hiyo atahakikisha analeta usawa wa kijinsia,kuwalinda watoto,kuwatunza wazee na kuwapa vijana elimu ya kujitegemea.

Alisema ni mara ya pili kuchukua ambapo alishawai kuchukua mwaka 2010 na akaambiwa kuwa amekosa nafasi hiyo kutokana na kuwepo na mtu ambaye amemzidi sifa na kwamba mtu huyo si mwingine alikuwa Rais Dk.Shein.

 Amesema  miongoni mwa sifa za mtu anayetakiwa ni kiwango cha elimu na kwamba kiwango chake cha elimu ni kizuri na pia ni mwanadiplomasia wa muda mrefu.

Aliongeza kuwa amewahi kutumikia nafasi mbali mbali ndani na nje ya Chama zikiwemo  kuwa Balozi katika nchi mbali mbali pamoja na kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Kusini Unguja,Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM wilaya ya Kati Unguka pia nishawahi kuwa Mkurugenzi wa ZSTC Zanzibar.

 Balozi Karume amesema aliwahi kuwa Mkuu wa mabalozi wa Tanzania katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2008 na Naibu Balozi Washington DC-Marekani na Naibu Balozi Brussels Belgium.


Waziri Karume amezaliwa Kisima Majongoo mjini Unguja  24 Mei mwaka 1950 ambapo alipata elimu ya chuo kikuu cha Columbia mjini New York nchini Marekani na kitaaluma ni mchumi na mwanadiplomasia wa kimataifa.



 Katibu wa NEC,Idara ya Oganazesheni CCM Zanzibar Cassian Galos Nyimbo (kushoto), akimkabidhi fomu Kada wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Ndugu Mbwana Bakari  Juma (kulia) anayeomba ridhaa ya Chama kumchagua kuwa Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama chake ,katika hafla iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kiwandui Zanzibar.
  Katibu wa NEC,Idara ya Oganazesheni CCM Zanzibar Cassian Galos Nyimbo (kushoto), akimkabidhi fomu Kada wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Balozi Ali Abeid Amani Karume (kulia) anayeomba ridhaa ya Chama kumchagua kuwa Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama chake ,katika hafla iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kiwandui Zanzibar.
 KADA wa Chama Cha Mapinduzi Balozi Ali Abeid Amani Karume aliyechukua fomu ya kuomba ridhaa ya CCM kumchagua kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar alionyesha Mkoba wenye fomu hizo baada ya kukabidhiwa katika hafla iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.
 KADA wa Chama Cha Mapinduzi Balozi Ali Abeid Amani Karume aliyechukua fomu ya kuomba ridhaa ya Chama kumchagua kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar, akiomba dua katika Kaburi la Mwasisi wa Mapinduzi na Rais wa kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi marehemu Mzee Abeid Amani Karume, mara baada ya kuchukua fomu hiyo.

  KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Mbwana Bakari Juma aliyechukua fomu ya kuomba ridhaa ya CCM kuchaguliwa kuwa Mgombea Urais wa Zanzibar  kupitia Chama, akipewa maelekezo  na Afisa Mwandamizi wa Idara ya Oganazasheni Ndugu Abdi Mahmoud Abdi (kulia)  baada ya kukabidhiwa fomu ya kuwania Urais wa Zanzibar ambapo kushoto ni Katibu wa NEC,Idara ya Oganazesheni CCM Zanzibar Cassian Galos Nyimbo.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni