KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hashim Salum Hashim leo amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kugombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM.
Kada huyo amewasili katika Ofisi
za Afisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Kisiwandui Zanzibar majira ya saa 6:10
mchana na kupokelewa na maafisa wandamizi wanaoshughulikia mapokezi ya makada
hao.
Hashim alikabidhiwa fomu hiyo na Katibu
wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Cassian Gallas
Nyimbo, na kumtaka atafute wadhamini 250 wa Chama Cha Mapinduzi.
Akizungumza na waandishi wa
habari mara baada ya kukabidhiwa fomu hizo Hashim, amesema endapo atapewa
ridhaa na Chama atahakikisha kipaumbele chake ni kuimarisha sekta ya michezo
nchini.
Amesema yeye ni mwanamichezo na
amehudumu katika sekta hiyo kwa muda mrefu hivyo atahakikisha serikali inatoa udhamini wa ligi kuu ya soka Zanzibar kwa asilimia 100.
Amefafanua kuwa ligi hiyo
inaendeshwa bila udhamini kwa muda mrefu toka kampuni ya Grand Malta isitishe
udhamini wake mwaka 2013.
Ameongeza kwamba mbali na michezo
pia ataendeleza maendeleo yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 10 ya
Serikali ya awamu ya saba chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein.
“Nampongeza Rais wetu Dk.Shein
kwa kasi yake ya kuwaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo endelevu hasa katika
sekta za afya,elimu, miundombinu ya umeme na barabara, maji safi na salama
pamoja na sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii”,amesema.
Pamoja na hayo kada huyo ambaye ni
mtumishi wa SMZ katika Idara ya Mazingira amesema ataimarisha maendeleo katika Nyanja
za kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya wananchi wote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni