Jumanne, 23 Juni 2020

RASHID, MASAUNI,RC AYOUB NA BHAA NAO WAJITOSA MBIO ZA URAIS ZNZ



MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwemo mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni baadhi ya wanachama waliochukua fomu, kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM katika nafasi ya urais wa Zanzibar.

Wa kwanza aliyefika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui baada ya kufunguliwa ofisi hizo saa 2:00 asubuhi ni Mwakilishi wa Jimbo la Amani, Rashid Ali Juma (54).

 Alikabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa Idara ya Oganaizesheni, Cassian Gallos Nyimbo ambaye alimtaka kutafuta wadhamini 250 katika mikoa mitano ya Unguja na Pemba.

 Akizungumza na waandishi wa habari, Juma ambaye ni mchumi katika masuala ya kodi akiwa mwanzilishi wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), aliipongeza CCM kwa kuweka utaratibu mzuri katika uchukuaji wa fomu, kwa kutoa ruhusa kwa kila mwanachama kutumia demokrasia yake.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, aligombea jimbo la Amani na kuibuka na mshindi na kuteuliwa na Rais Dk Ali Mohamed Shein kuwa Waziri wa Habari, Utalii na Utamaduni na baadaye kuhamishiwa katika Wizara ya Kilimo,Maliasili, Mifugo na Uvuvi.



 Mwingine aliyefika kuchukua fomu ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yussuf Masauni aliyeambatana na mkewe. Masauni ni Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni na aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).

Alikabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa Idara ya Oganaizesheni ya CCM, Gallos Nyimbo. Akizungumza na waandishi wa habari, Masauni alisema akipewa ridhaa kuongoza Zanzibar, atahakikisha anaendeleza mambo yote mazuri, yaliyofanywa na Rais wa Zanzibar, Dk.Shein na Rais John Magufuli katika mapambano dhidi ya rushwa na wahujumu wa uchumi.



 ‘’Leo mimi sina cha kusema kwa waandishi wa habari...lakini nikipewa ridhaa ya kuongoza nchi nitahakikisha nafuata nyayo za watangulizi wangu na Rais Shein katika mapambano dhidi ya rushwa na wahujumu uchumi,”alisema.



Aidha, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Khamis Mussa Omar alijitokeza na kuchukua fomu kuomba ridhaa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar.

Mussa ni msomi wa masuala ya kodi na amekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa miaka 14 sasa.

Pia aliwahi kuwa Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2002. Ni miongoni mwa waanzilishi wa Mamlaka ya Uwekezaji nchini (ZIPA) mwaka 2005-2006. 

 ZIPA ndiyo iliyoweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta mbalimbali, ikwemo uwekezaji wa hoteli za kitalii. ‘’Nimechukua fomu kuomba ridhaa ya nafasi ya urais wa Zanzibar, lakini si kwa gharama yoyote na sitanuna kama sitachaguliwa kushika wadhifa huo,’’alisema.

 Mwingine aliyechukua fomu ya kuomba ridhaa kupeperusha bendera ya CCM ni Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Mmanga Mjengo Majawiri.



Mjawiri alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SUZA). ‘’Nimejitathmini kwa makini sana kwa kuzingatia kauli ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Rais Magufuli kwa wale wanaokusudia kuchukua fomu na ndiyo maana nimechukua fomu hii,’’alisema Mjawiri, ambaye ni Mwakilishi wa jimbo la Mkoani katika kisiwa cha Pemba.



 Waziri mwingine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) aliyechukua fomu ya ni Mohamed Aboud Mohamed, anayeongoza Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, inayoratibu shughuli mbalimbali ikiwemo za Muungano.

Aboud amechukua fomu ya urais wa Zanzibar huku akisema “Hatukuja kushindanishwa wagombea katika kinyang’anyiro hicho.

Nimekuja kuchukua fomu kwa ajili ya kutekeleza demokrasia pana katika Chama Cha Mapinduzi” alisema.



Mwingine aliyechukua fomu ni kada wa CCM ambaye ni Mhadhiri wa vyuo mbalimbali nchini, Bakari Rashid Bakari (56).

Alikipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kufungua milango ya kuchukua fomu na kuweka mazingira mazuri kwa kila mwanachama wa chama hicho mwenye sifa na uwezo.


Mwingine aliyechukua fomu ya CCM kuwania urais wa Zanzibar ni Hussein Ibrahim Makungu maarufu kama ‘’Bhaa’’.

Aliahidi kufanya mambo makubwa yenye maslahi kwa wananchi wa Zanzibar, ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 ‘’Nimefurahishwa na demokrasia iliyotukuka ndani ya Chama cha Mapinduzi, yenye kutoa fursa kubwa kwa kila mwanachama mwenye sifa na uwezo,’’alisema.

 Kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari, Hussein alizuru kaburi la Rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati Shehe Abeid Amani Karume.

Hussein ni Mwakilishi wa Jimbo la Mtoni. Kabla ya hapo alikuwa mwakilishi wa Jimbo la Bububu huku akiwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitia nafasi tano za Baraza la Wawakilishi.

 Mtu mwingine aliyechukua fomu ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohammed.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni