Jumanne, 30 Juni 2020

MHE.SAMIA AANZA ZIARA YA KUIMARISHA CHAMA KUSINI UNGUJA.


 MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kusini Unguja, katika ziara yake ya kuimarisha Chama,Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa SUZA Tunguu.
 WAJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa kusini Unguja,wakifuatilia maelekezo yanayotolewa na mgeni rasmi Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mhe.Samia Suluhu Hassan.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan,amewasihi Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kusini Unguja kuendelea kuwa wamoja na kushikamana katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Dola mwaka huu.

Rai hiyo ameitoa wakati akizungumza na wajumbe hao huko katika ukumbi wa Mikutano wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar(SUZA),amesema ushindi wa Chama Cha Mapinduzi utatokana na ushirikiano baina ya viongozi hao na wanachama wote.

Mhe.Samia alisema licha ya mkoa huo kuwa ngome ya Chama bado wanatakiwa kulinda heshima hiyo kwa kujipanga vizuri kuhakikisha Chama kinashinda.

"Nakuombeni tufanye kazi kwa mashirikiano makubwa kwani ushindi wa Chama chetu hautopatikana kwa maneno bali kwa juhudi za kila mmoja wetu", alisema Mhe.Samia.

Katika maelezo yake Mhe.Samia, aliwasihi wajumbe hao kufuata miongozo na kanuni za Chama wakati wa kufanya uteuzi wa wagombea wa nafasi mbali mbali za uongozi katika Mkoa huo.

Pamoja na hayo alikemea vitendo vya rushwa na makundi ya kukigawa kwani vitendo hivyo vinapelekea kupatikana kwa viongozi wasiokuwa na sifa za uongozi.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kupongeza mkoa huo kwa juhudi zao za kiutendaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kichama.

Alitoa pole kwa wananchi wa mkoa huo kwa kukumbwa na majanga mbali mbali yakiwemo ugonjwa wa corona pamoja na mafuriko na kuwasihi kuendelea kuchukua tahadhari.

Alisisitiza wananchi kuendelea kutunza mazingira ili kuepuka majanga mbali mbali yakiwemo mafuriko.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa huo Ramadhan Abdallah Ali,alimpongeza Mjumbe wa Kamati kuu Mhe.Samia kwa utendaji wake na kuwa karibu na mkoa huo kwa kutoa nasaha za kujenga Chama.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa huo Suleiman Mzee Suleiman,akisoma taarifa ya utekelezaji ya Chama kuanzia Januari hadi Machi 30 mwaka huu,alisema wamejipanga vizuri na watahakikisha wanashinda majimbo yote yaliyomo ndani ya mkoa huo.

Kupitia taarifa hiyo waliwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni