NAIBU KATIBU MKUU WA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) ZANZIBAR DK. ABDULLA JUMA MABODI. |
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka Wananchi visiwani hapa kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga dhidi ya ugonjwa hatari wa virusi vya Corona ambao ulianzia nchi za nje na hivi sasa tayari umeripotiwa kuingia Tanzania.
Mbali na hilo, CCM imezitaka Ofisi zote za Chama,Jumuiya,matawi na maskani za Chama kutoa elimu na ufafanuzi wa kina kwa wanachama juu ya maelekezo yaliyotolewa na chama ngazi ya taifa dhidi ya kujikinga na ugonjwa huo.
Kauli hiyo ameitoa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla "Mabodi", Ofisini kwake Kisiwandui mjini Unguja ambapo alisema ugonjwa huo ni janga la kiafya dunia nzima.
Amesema kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi zinazopokea raia wengi wa kigeni kupitia sekta ya utalii, hivyo ni lazima mamlaka husika kufanya kazi ya ziada ya kuhakikisha maeneo yote yanayotumika kama njia za kuingia visiwani humu wanakuwepo wataalamu wa afya kwa ajili ya kufanya vipimo vya ugonjwa huo.
Amesema ni wajibu wa kila mwananchi bila kujali tofauti za kisiasa, kidini, kikabila na rangi kuanza kuchukua hatua stahiki za kujikinga dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona.
Dk.Mabodi, amesema Wanachama wanatakiwa kuheshimu maamuzi yote yaliyofikiwa na Chama kwa ngazi ya Taifa ya kusitisha shughuli mbalimbali za kichama, zinazotengeneza mkusanyiko wa watu unaoweza kusababisha maambukizi ya ugonjwa huo.
Pia, Dk. Mabodi amepongeza hatua zilizochukuliwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania(SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar(SMZ), chini ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli na Rais Dk.Ali Mohamed Shein kwa kusitisha baadhi ya shughuli za kitaifa kwa lengo la kudhibiti ugonjwa huo.
Katika maelezo yake,Naibu Katibu Mkuu huyo aliitaka Serikali kuendelea na juhudi za kuchukua hatua mbalimbali za kujikinga na ugonjwa huo, ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi na kuandaa vifaa tiba vya dharura vitakavyosaidia kuwa kinga wananchi dhidi ya Corona.
Naibu Katibu Mkuu huyo aliwataka wananchi kutoa taarifa pindi watakapobaini uwepo wa watu wenye dalili za ugonjwa huo ili mamlaka husika ziweze kuchukua hatua za haraka kwa mujibu wa taratibu za kiafya.
Pamoja na hayo Naibu Katibu Mkuu huyo amewasihi Wanachama wa CCM na Wananchi kwa ujumla, kuepuka mikusanyiko mbalimbali kutokana na kuwa ugonjwa huo unasamba kwa njia ya hewa na hata kugusana baina ya mtu na mtu.
Amevitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama kudhibiti bandari bubu na njia mbalimbali zisizo rasmi za kuingia katika visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ili kuzuia baadhi wa watu wanaotumia njia hizo kuingia nchini wasilete ugonjwa huo.
Naibu Katibu Mkuu huyo Dk.Mabodi, ameongeza kwa kutoa wito kwa waumini wa dini mbalimbali nchini, kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya pindi wanapokusanyika kwa ajili ya ibada ikiwemo Makanisani na Miskitini.
Pamoja na hayo alivitaka Vyombo vya Habari nchini kutoa taarifa na elimu sahihi kwa umma, huku serikali ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na janga hilo.
Amesema itolewe elimu ya Afya ya jamii juu ya kinga ya Corona hasa Vijijini na Maskulini kwa njia ya vipeperushi, Matangazo kwa njia ya mabomba.
Dk.Mabodi, ameshauri wataalamu wote wa tasnia ya Afya waliostaafu na walio makazini pamoja na sekta nyingine waungane na kutengeneza timu moja, itakayosaidia katika mapambano dhidi ya maradhi haya ya Corona.
Aidha, amewataka Viongozi,Wanachama na Makada wa ngazi mbalimbali wa CCM kuendelea kuiamini Serikali yao kuwa itachukua hatua madhubuti za kuhakikisha wananchi wote wanabaki salama dhidi ya ugonjwa huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni