Jumanne, 30 Aprili 2019

DK.MABODI-ASEMA MUUNGANO NI CHIMBUKO LA MAENDELEO YA ZANZIBAR NA TANZANIA BARA.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi (wa kwanza kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Bomba FM Radio Munir Zakaria (wa pili kulia) na Mhariri Mkuu wa Bomba FM Radio Mwinyi Saadalla (wa kwanza kushoto) wakiwa katika Mahojiano Maalum ya Miaka 55 ya Muungano wa Zanzibar na Tanganyika pamoja na Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa upande wa Zanzibar.


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’  amesema CCM inaamini kuwa Muungano wa Serikali mbili ya Zanzibar na Tanganyika ndio chimbuko la Maendeleo endelevu yaliyofikiwa katika Nyanja za Kiuchumi, Kijamii na Kisiasa.

Amesema Siri ya kudumu kwa Muungano huo  hadi kufikia miaka 55 ni kutokana na kujikita katika Undugu wa Damu badala ya Maslahi binafsi ya kila Nchi, hali iliyopelekea kuwepo kwa kuaminiana, kushauriana na kuheshimiana katika kutatua changamoto za Muungano huo.

Ufafanuzi huo ameutoa leo katika Mahojiano Maalum  ya Miaka 55 ya Muungano  na Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 yaliyorushwa Mubashara (Live) kupitia Kituo cha Redio ya Bomba FM iliyopo Uwanja wa Ndege Zanzibar.

Dk.Mabodi ameeleza kuwa huwezi kuutaja Muungano huo bila kueleza Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 pamoja na Uhuru wa Tanganyika wa mwaka 1961, ambavyo ndio chachu ya Ukombozi,Utu na Ustawi wa kijamii kwa Wananchi wa pande zote za Muungano.

Amesema Waasisi wa Muungano huo ambao ni Marehemu Mzee Abeid Aman Karume na Hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere waliamua kuunda Mfumo huo kwa kutafakari kwa kina maendeleo na fursa za Kijamii za Wananchi waliowaongoza kwa wakati huo.

Amesema haikuwa kazi rahisi Nchi ndogo ya Zanzibar kukubali iungane na Nchi kubwa ya Tanganyika lakini kupitia mashauriano ya Vikao vya Wazee na ridhaa ya Wananchi wenyewe yalizaa matunda ya kufikia mwafaka wa kuingia katika Mfumo huo ili kushirikiana katika masuala ya Kiuchumi,Kisiasa, kimaendeleo na kijamii.

Naibu Katibu Mkuu huyo wa Zanzibar Dk.Mabodi alisema Muungano huo ulikuwa na changamoto zaidi ya 15 zilizotatuliwa hatua kwa hatua ambapo hivi sasa zimebaki nne na 11 tayari zimetafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

Amewapongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kwa kusimamia ipasavyo utatuazi wa changamoto hizo za Muungano hatua iliyoendelea kuleta ufanisi katika masuala ya Kiuchumi.

Amesema changamoto nne zilizobaki nazo zikitafutiwa ufumbuzi zitaibuka zingine kutokana na asili ya maisha ya binadamu kwani kila siku Watu wanazaliwa na mahitaji yanaongezeka kutokana na mahitaji ya wakati husika.

“Katika Utawala wa Serikali ya Awamu ya Saba ya Dk.Shein  na Awamu ya Tano ya Dkt.Magufuli changamoto hizi zimetatuliwa kwa kasi kubwa sana na zilizobaki zitatuliwa wakati wowote kwa njia ya Vikao vya pande zote mbili.

Wananchi waendelee kuamini kwamba Serikali zao zipo makini sana katika kusimamia maslahi yao na masuala mbali mbali ya Kitaifa,Kikanda na Kimataifa chini ya Muungano wetu huu wa Serikali mbili”,alisema Dk.Mabodi.

Amesema kuna baadhi ya Watendaji wasiokuwa waaminifu wanaohudumu katika Sekta za Umma wamekuwa wakichafua hadhi ya Muungano kutokana na vitendo vyao vya Rushwa na Urasimu usiokuwa na sababu za msingi katika utoaji wa Huduma.

Aliziutaja sababu za kuwepo kwa Muungano huo kuwa ni Ulinzi na Usalama wa Nchi zote mbili pamoja na kutoa Uhuru kwa Wananchi wa pande zote mbili kuishi sehemu yoyote ya Muungano bila kusumbuliwa.

Ameeleza kuwa kwamba msimamo wa Serikali zote mbili ni kulinda kwa gharama yoyote Tunu hiyo ya Muungano dhidi ya maadui wanaopambana uvunjwe ili wao wapate njia ya kupenya katikati na kurudisha utawala Kikoloni na Kisultani.

Akizungumzia Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Zanzibar Dk.Mabodi amesema ahadi walizoahidiwa Wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu uliopita zimetatuliwa kwa zaidi ya asilimia 97 za kabla ya 2020 zitakuwa zimetatuliwa kwa kiwango kikubwa.

Amesema Serikali ya awamu ya Saba chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein zimeimarishwa kwa kiwango kikubwa Sekta za Afya, Elimu,Maji Safi na Salama, Uvuvu,Kilimo pamoja na Miundombinu ya Babaraba Anga na Nchi Kavu.

Alieleza kwamba katika awamu hiyo Dk.Shein ameasisi Sera ya Elimu bure na Afya bure kwa lengo la kuwapunguzia mzigo Wananchi wa Visiwa vya Zanzibar katika kulipia matibabu na Elimu ili Sekta hizo zipate kuimarika.

Aidha  katika maelezo yake Dk.Mabodi amemtaja  Dk.Shein kuwa ni Shujaa wa maendeleo kwani kwani ameandika Historia mpya katika Nchi za Afrika Mashariki ya kuwalipa Pencheni ya Shilingi 20,000 kila mwezi Wazee wote  wenye umri wa kuanzia miaka 70 bila ya kujali tofauti zao za Kisiasa.

Pamoja na hayo amewaomba Wananchi kupima na kutathimini shughuli zinazofanywa na Vyama vya Siasa vinavyopewa Ruzuku na Serikali vinashughulikia kwa kiasi gani Changamoto za Wananchi na hatimaye wafanye maamuzi sahihi ya kutoa ridhaa kwa CCM ili iendelede kuongoza Dola kupitia Uchaguzi wa mwaka 2020.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni