NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk.Abdulla
Juma Saadalla ‘Mabodi’ amesema Chama hicho kimejizatiti kutatua changamoto za Wananchi pamoja na kusimamia Demokrasia kwa kukemea vitendo viovu vinavyohatarisha
Amani na Utulivu wa Nchi.
Kauli hiyo ameitoa katika ziara yake ya kukagua Uhai wa
Chama na Utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Jimbo la Makunduchi Wilaya ya
Kusini Unguja, amesema vipaumbele vya CCM ni kutekeleza kwa kasi ahadi
zilizotolewa na Taasisi hiyo kwa wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu uliopita.
Amesema Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kuaminiwa,kupendwa na
kuthaminiwa na Mamilioni ya Watanzania kutokana na usimamizi mzuri wa
utekelezaji wa Sera zake, kwa kutatua changamoto za kijamii kwa wakati mwafaka.
Aidha amesema katika kusimamia dhana ya Demokrasia CCM
haitosita kukemea vitendo viovu vinavyoashiria kuvunja Sheria za Nchi, hasa
vinavyotekelezwa na baadhi ya Vyama vya upinzani.
“Tumekubali kuingia katika mfumo wa Vyama vingi ili
tushindane kwa Sera na sio kushindana kwa vituko na vurugu ni muhimu kila
mwanasiasa kujitathimini juu ya mwenendo wake kwa jamii anayoiongoza.”, ameeleza Dk.Mabodi.
Amesema katika zama za CCM mpya imekuwa imekuwa ni kimbilio
la wananchi wanaoamini katika siasa za maendeleo ambao wametelekezwa na Vyama
vyao na kupokelewa vizuri ndani ya CCM ili
wanufaike na Demokrasia iliyotukuka.
Amewataka Viongozi na Watendaji wa CCM kutowawekea vikwazo
Wananchi wanaotaka kujiunga na Chama na
badala yake wapewe fursa hiyo bila masharti magumu sambamba na kuwasomesha miongozo
na itikadi za kitaasisi.
Amewaagiza Wabunge,Wawakilishi na Madiwani kufanya mikutano
katika maeneo yao ya kuwaeleza Wananchi mafanikio yaliyofikiwa katika
utekelezaji wa Ilani ili wananchi hao wawe Mabalozi wa kufikisha taarifa hizo
kwa jamii.
Amewambia wananchi kuwa CCM imesimamia kwa ufanisi miradi
ya maendeleo ukiwemo wa TASAF ambao upo katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020,
ambao umewaondosha wananchi katika wimbi la umasikini na kuwa na kipato cha
kati.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa mbali mbali vikiwemo
Runinga (Television) pamoja na Fedha kwa vikundi 11 vya Saccos ya Shehia ya
Mzuri katika Maskani ya CCM ya Kisonge Makunduchi Dk.Mabodi amesisitiza kuwa
uhai wa Taasisi hiyo ya kisiasa unaanza kuimarishwa kuanzia ngazi ya mashina.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi Mhe.Haroun Ali
Suleiman amesema tayari Ilani ya CCM ndani ya Jimbo hilo imetekelezwa kwa
asilimia 90, na kwa sasa wanaendelea kutatua baadhi ya changamoto ili
kuzimaliza kabla ya 2020.
Mhe.Haroun amesema kwa kushirikiana na Kamati ya Siasa ya
Jimbo hilo wamefanya ziara katika Shehia 13 za Jimbo kwa kuratibu
changamoto zinazowakabili wananchi na nyingi zimetatuliwa sambamba na kueleza
fursa na miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Serikali.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Ameir Haji Timbe ameeleza kuwa maendeleo yaliyopatikana katika Jimbo hilo yametokana na ushirikiano mkubwa
uliopo baina ya viongozi na wananchi.
Akizungumza Mwenyekiti wa Maskani ya CCM ya Kisonge iliyopo
Makunduchi Abdallah Hassan Haji amesema wanaendelea kuvuna wanachama wapya
kutoka vyama vya upinzani huku wakijipanga kufuta masalia ya upinzania ndani ya
Jimbo hilo.
Naye Mwenyekiti wa Maskani ya CCM ya Hapa Kazi Tu Yussuf
Abeid Haji, akizungumza katika uzinduzi wa Maskani hiyo amefafanua kuwa eneo la maskani
yao litatumika kuwa chachu ya kujenga umoja,mshikamano pamoja na kuwa kituo
mbadala cha kubuni miradi mbali mbali ya maendeleo kwa maslahi ya Wana CCM.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni