Ijumaa, 26 Aprili 2019

DK.MABODI ATANGAZA NEEMA KIJIJI CHA KIKOBWENI, MHE.NADIR AELEZA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM 2016-2017.


 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi akizungumza katika Mkutano wa Jimbo wa Jimbo la Chaani wa  kuelezea Utekelezaji wa Ilani ya CCM.
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi(kulia) akimsikiliza Mkaazi wa Kijiji cha Kikobweni Ndugu Hassan Nganja(kushoto) aliyetoa maoni yake juu ya kuwepo na upungufu wa huduma za Maji Safi katika Kijiji hicho.

 MWAKILISHI wa Jimbo la Chaani Unguja Mhe.Nadir Abdul-Tif Yussuf akizungumza na Wananchi katika Mkutano wa Jimbo hilo katika uwanja wa Mpira wa Kijiji cha Kikobweni Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja.

 BAADHI ya Wananchi wa Jimbo la Chaani wakisikiliza kwa makini taarifa mbali mbali za Utekelezaji wa Ilani katika Jimbo hilo.


NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk.Abudlla Juma Saadalla Mabodi amesema CCM itachimba Kisima cha Maji Safi na Salama kwa muda wa wiki mbili ili kuondosha changamoto ya ukosefu wa nishaji hiyo kwa Wananchi wa Kijiji cha Kikobweni Jimbo la Chaani Wilaya ya Kaskazini  'A' Unguja.

Ahadi hiyo ameitoa katika Mkutano wa Jimbo la Chaani wa kueleza utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Chama na Serikali,ambapo baadhi ya Wananchi wa kijiji hicho wamedai kuwa na upungufu wa huduma za maji ambapo kwa sasa wanatumia maji kisima cha zamani ambacho hakikidhi mahitaji ya huduma hiyo kwa wananchi hao.

Dk.Mabodi amesema kwa hatua ya awali anatoa kiasi cha shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya maandalizi ya uchimbaji wa kisima hicho ili wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani wapate huduma hiyo kwa wakati hasa katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuanzi hivi karibuni.

Amesema  wananchi wana haki ya kueleza changamoto zinazowakabili kwa viongozi wao waliowapa ridhaa ya kuwaongoza katika ngazi mbali mbali za kiuongozi katika Chama na Serikali.

Amesema  CCM ni Taasisi ya Kisiasa inayoahidi na ikatekeleza kwa vitendo na kwa wakati mwafaka na haitoi ahadi za kuwalaghai Wananchi kama vinavyofanya baadhi ya vyama vya upinzani kuwa wataijenga Zanzibar kwa Siku 100 iwe kama Nchi ya Singapore.

Amesema  Maendeleo hayana itikadi wala misimamo ya kisiasa kwani inapotekelezwa Ilani ya CCM kwa kuwafikishia wananchi huduma za maji,Umeme,Bababara na Vituo vya Afya fursa hizo hazitumiwi na Wanachama wa CCM pekee yao bali wananufaika wananchi wote.

Ameeleza  kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa sasa inatekeleza Ilani ya CCM kwa kujenga Barabara yenye kiwango cha Lami katika Mkoa wa Kaskazini Unguja ili kurahisisha huduma za Usafiri kwa Wananchi wa Mkoa huo.

Katika maelezo yake Dk.Mabodi amewambia Wananchi wa Jimbo la Chaani kwamba Serikali ipo katika hatua za kutekeleza Mradi mkubwa wa Maji Safi na Salama ambapo ukikamilika utamaliza changamoto ya upungufu wa huduma za maji Mkoani humo.

Kupitia Mkutano huo Dk.Mabodi ameeleza kuridhishwa kwake na Utekelezaji  wa Ilani ya CCM katika Jimbo hilo, licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo zinazotafutiwa ufumbuzi wa kudumu na viongozi wa jimbo hilo.

Amewataka Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo hilo watatue changamoto zilizopo katika maeneo mbali mbali ya jimbo hilo ili Chama kishinde bila vikwazo katika  Uchaguzi Mkuu ujao.

Amesema  CCM inapozungumzia ushindi wake wa Kihistoria katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020, ni kutokana na utekelezaji mzuri wa ahadi zilizotolewa kupitia Uchaguzi Mkuu uliopita.

Pamoja na hayo amewasihi wananchi wa Jimbo hilo kuthamini miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwani kuna baadhi yao wamekuwa wakihujumu miradi hiyo kwa makusudi hali inayokwamisha baadhi ya fursa za kimaendeleo.

" Nimeshuhudia katika Mkoa huu inahujumiwa miondombinu ya Maji Safi na Salama kwa kuiba vifaa vya umeme,kuharibiwa kwa Gari ya wagonjwa na matukio mengine ya kukatisha tamaa na yote hayo yanatekelezwa na watu wachache wapinga maendeleo.",ameeleza Dk.Mabodi.

Amewaonya  baadhi ya Watendaji na Viongozi wa Ngazi za Majimbo katika Wilaya ya Kaskazini 'A' Unguja, wanaojihusisha na mipango ya kuwaandaa  Wagombea wa ngazi mbali mbali za Uongozi kabla ya muda wa kufanya hivyo kufika kwani kufanya hivyo ni kukiuka Katiba ya CCM ya mwaka 1977 na miongozo yake.

Pamoja na hayo amesema  CCM itaendelea kulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa gharama yeyote na atakayejaribu kubeza atakuwa ni msaliti na adui wa Taifa.

Akitoa Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe.Nadir Abdul-Tif Yussuf amesema kwa kipindi cha mwaka 2016-2017 alitekeleza masuala mbali mbali yakiwemo kuvipatia fedha za mitaji vikundi vya ujasiriamali,alinunua Gari maalum la Wagonjwa,kuweka Taa za umeme za kuwasha usiku Viwanja Vitatu,kujenga visima vya Maji Safi na Salama pamoja na kununua mashine za Kilimo za Power Tiller kwa ajili ya shughuli za Kilimo.

Miradi mingine iliyotekelezwa ni pamoja na matengenezo ya Ofisi mbali mbali za CCM,ununuzi wa Dawa za Binadamu katika Vituo vya Afya mbali mbali mbali pamoja na ununuzi wa Vyarahani 10 kwa ajili ya vikundi vya Jimbo.

Mhe.Nadir  ametoa  tahadhari kwa baadhi ya Watu wanaotengeneza makundi ya kuwagawa na kuwafitinisha viongozi wa Jimbo hilo uku wakipanga wagombea kinyume na utaratibu na kuongeza kwamba watu hao hawakitakii mema Chama Cha Mapinduzi.

Wakizungumza kwa wakati tofauti Wananchi wa Jimbo hilo mara baada ya Mkutano huo,wameeleza kwamba wamenufaika sana na miradi inayotekelezwa na fedha za Mfuko wa Jimbo wa Mwakilishi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni